in

England: Wazuri au bado?

THREE Lions

THREE Lions – Timu ya Taifa ya England wameangukia pua kwa kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mataifa baada ya kupigwa 2-0 na Ubelgiji ugenini.

Lakini kwa kutazama mechi yenyewe, England ndio walicheza vyema zaidi ya wapinzani wao wakimiliki mpira zaidi, kujaribu zaidi langoni mwa wapinzani hao, kona nyingi na pasi zaidi, lakini mwishoni waliondoka bila chochote kwa maana ya matokeo.

Naam, soka ni mchezo wa namba bila kujali umiliki wa mpira au pasi na yale majigambo ya chenga za maudhi, na mwishoni mwa mchezo, nahodha wa Three Lions, Harry Kane aliishia kusema kwamba kwa uhakika waliutawala mchezo lakini wakaupoteza.

Inamaanisha nini? Twaweza kusema kwamba England sasa ni wazuri kuliko awali? Kulikoni washindwe kufuzu kwenye mashindano hayo? Walishindwa kwa kiasi kikubwa kwenda sawa na uzoefu na ufanisi wa Ubelgiji waliofunga mabao katika kipindi cha kwanza wakitumia makosa ya England waliyofanya karibu na eneo la golikipa Jordan Pickford.

Baada ya kuikamilisha kazi, au Wazungu wanavyosema ‘to kill the game’, walirudi nyuma, wakawa hawana shinikizo bali kuwadhibiti wachezaji wa England wasiwe na madhara, bila kujali majina yao makubwa, wakawa na tabu ya kurudisha mabao mawili hayo. Hilo laweza kuchukuliwa kama somo kwenye soka ya kimataifa ambayo vijana wa Gareth Southgate wanatakiwa kubaki nalo.

Namna nyingine ya kulitazama hilo ni jinsi kambi ya England ilivyokuwa – walijitahidi, wakacheza vyema, wakatengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao na yale waliyofungwa kwa hakika huwezi kusema ni uzembe mkubwa na pengine unaweza kusema bahati haikuwa yao.

Unaweza kusema kwamba matokeo yale yalikuwa ya ‘kinyama’ au ya kughushi kama alivyopata kudai kocha wa zamani wa Chelsea na Manchester United enzi hizo, Jose Mourinho ambaye kwa sasa yupo na Tottenham Hotspur juu ya matokeo mabaya dhidi ya timu yake.

Tanzania Sports
Harry Kane

Ukitazama jinsi mshambuliaji wa Aston Villa, Jack Greealish alivyokuwa akicheza, akikata dimba na kutumbukiza vitu vikali kuelekea kwa wapinzani wao, inakuwa ngumu kuamini matokeo hayo kama ni kwa kusoma tu ubaoni.

Kwa hiyo, kipi ni kipi? Matokeo au utawalaji wa mchezo? Southgate alisisitiza baadaye kwamba kwake kikubwa ni kutawala mchezo na ufanisi badala ya matokeo, kwa sababu ufanisi ndio huleta matokeo mazuri, lakini safari hii haikutokea. Pengine ni bahati mbaya.

Anasema kwamba utendaji wa ujumla wa hiyo juzi ulikuwa mzuri kwao kuliko hata walipowafunga Ubelgiji 2-1 nyumbani Wembley mwezi uliopita. Hakika ilikuwa utamu kuwatazama England kwenye kichapo hiki kuliko kwenye ushindi ule mwembamba, lakini ndio hivyo.

Lakini, wakati huo huo, lazima kukiri kwamba hawakuwa wakamilifu la sivyo hawangeruhusu mabao mawili na kushindwa kufunga hata moja. Inabidi kuwaweka England pamoja kwa uzuri ili kusudi kule mbele mabao yapatikane, viungo wafanye kazi yao vizuri na ukuta usiruhusu mabao.

Utakosaje mabao kwa mfano ukiwa na ushirika wa utatu wa Kane wa Spurs, Marcus Rashford wa Manchester United na Raheem Sterling wa Manchester City wanaochanua vyema kwenye klabu zao? England wanatakiwa kuwa wazuri zaidi kwa maana ya matokeo ya kila mechi.

Wanatakiwa kujiamini, tena wakiwa na beki ghali zaidi katika Harry Maguire. Wakiwa na mfumo wa 4-3-3 uliowafanya kuwa wakali zaidi kwenye kufuzu kwa michuano ya Euro, wangeweza pia kufanya vyema hivi.

Kwenye soka ya kimataifa, ikiwa unatazama kwenye mechi moja au katika nusu ya msimu wa mechi za kimataifa, wakati wote lazima kuwapo tofauti ya maoni. Itabidi kusubiri hadi Juni mwakani huko Wembley kwa ajili ya kupata majibu ya baadhi ya maswali haya.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Ben robinson

Ni wakati wa viongozi sahihi kwenye soka

Simba SC

Simba watakumbuka uzoefu waliopata kwa Enyimba?