in , , , ,

NI WAKATI WA LUCHO KUTHIBITISHA UBORA WAKE

 

Lionel Messi atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki saba mbaka nane kufuatia majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Las Palmas hapo juzi. Mshambuliaji huyo hatari aliyenyakua tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya mwezi mmoja uliopita ni mmoja kati ya wachezaji wenye umuhimu uliopitiliza kwenye klabu zao.

Kutokuwepo kwa Messi ni pengo kubwa ambalo linawahitaji wachezaji wa Barcelona kutumia nguvu ya ziada kuliziba. Pia linamuhitaji mwalimu wa FC Barcelona Luis Enrique kubadili ama kuboresha mbinu zake ili pengo hilo lisiwagharimu kwenye michezo yote ambayo Messi atalazimika kukosekana uwanjani.

Kukosekana kwa kipindi hicho cha wiki saba mbaka nane kunamaanisha kuwa Messi atakosa jumla ya michezo nane, mitano ya La Liga na mitatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kuna uwezekano pia Barcelona watashindwa kumtumia mchezaji huyo kwenye mchezo dhidi ya Real Madrid utakaopigwa Novemba 22 Santiago Bernabeu ikiwa atarejea baada ya wiki nane.

Luis Enrique anayefahamika kwa jina la Lucho aliiwezesha FC Barcelona kushinda makombe matatu ‘treble’ msimu uliopita. Sehemu kubwa ya mafanikio hayo yalichangiwa na Lionel Messi ambaye alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo kwa jumla ya mabao 58 huku akitengeneza mengine 26.

Baadhi ya mashabiki na wachambuzi wa soka wanadai kuwa Messi akiwa kwenye kiwango chake kilichozoeleka ni lazima Barcelona watwae mataji hivyo mafanikio ya Barcelona msimu uliopita yalitokana kwa kiasi kikubwa na ubora wa Lionel Messi na si mbinu za Lucho.

Huenda hata Lucho mwenyewe kwa kiasi fulani anakubaliana na madai ya namna hiyo. Baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana Septemba 24 mwaka jana kwenye mchezo wa La Liga dhidi ya Malaga Lucho alikiri kuwa timu yake hufanya vizuri Messi anapokuwa kwenye kiwango chake.

Hata hivyo kwa namna yoyote ile Lucho anastahili kupewa heshima na sifa zake. Ikumbukwe kuwa msimu uliopita ulikuwa ni msimu wake wa kwanza kama kocha wa Barcelona na akaiwezesha timu hiyo kushinda taji la La Liga.

Kuna makocha wengine wanne tu waliowahi kuweka rekodi ya namna hiyo wakiwa na Barcelona. Ni Josep Samitier mwaka 1945, Louis van Gaal mwaka 1998, Pep Guardiola mwaka 2009 na hayati Tito Vilanova mwaka 2013.

Ukiacha La Liga alitwaa na mengine mawili kwenye msimu huo wa kwanza na kukamilisha ‘treble’ kama alivyofanya Pep Guardiola msimu wa 2008/09 ambao kwake ulikuwa wa kwanza pia. Kwenye mafanikio ya kila mmoja wao Messi alikuwa na mchango mkubwa mno.

Inashangaza kuona watu wakimtukuza Guardiola na kumuona Lucho si kitu. Wanasahau kuwa kocha huyo aliposhinda ‘treble’ msimu uliopita aliweka rekodi ya kushinda jumla ya michezo 50 kati 60 msimu mzima wakati Guardiola alishinda michezo 42 tu kati ya 62 wakati anaiwezesha Barcelona kushinda ‘treble’ msimu wa 2008/09.

Nafikiri sasa ni wakati wa Lucho kuthibitisha ubora wake ili washabiki na wachambuzi wa soka wampatie heshima anayostahili. Anatakiwa kuboresha ama kubadili mbinu zake ili aweze kupata matokeo mazuri kwenye michezo mitano ya La Liga ambayo Messi hatakuwemo ili aiwezeshe Barcelona kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Pia anatakiwa kuiwezesha Barcelona kushinda michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mmoja dhidi ya Bayer Leverkusen, na miwili dhidi ya BATE Borisov bila uwepo wa Messi ili nyota huyo atakaporejea uwanjani akute timu hiyo imeshika usukani wa Kundi E.

 

 

 

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Fifa: Warner afungiwa maisha

Tanzania Sports

MAWAKALA WA FORODHA TANZANIA WAJIUNGA NA PSPF