KWA muda mrefu, baadhi ya wachezaji wa Tanzania wamekuwa wakitoroka kwenda kucheza soka ya kulipwa baada ya kufanya makubaliano nje ya klabu zao walizoingia mkataba ya awali.
Hatua hiyo imesababisha wakati mwingine kukwama na hata kurudi nyuma na kuwaangukia viongozi wa timu husika kuwa sasa wamepata timu na wataka ruhusa na ridhaa yao na waweze kucheza soka katika klabu zao mpya zilizowachuwa.
Kucheza soka nje ya nchi ni moja ya hatua kubwa kwa maendeleo ya soka, kwa wachezaji, klabu na nchi.
Kwamba mchezaji anajitengeneza kiuchumi kwa kuwa pato lake litaongezeka, klabu itafaidika kwa kuuzwa kwa mchezaji mwenye na nchi hasa timu ya taifa itapata mchezaji mwenye uzoefu na mikikimikiki ya wachezaji wengine.
Hivi karibuni,Β viongozi wa klabu ya Yanga waliandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kumsitaki kipa wao, Ivo Mapunda kwa kutoroka na kwenda kufanya majaribio katika timu ya St George ya Ethiopia.
Mapunda Aliondoka nchini mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda Addis Ababa.
Barua hiyo ya Yanga, imeitaarifu TFF kuwa Mapunda ameondoka nchini kwenda Ethiopia bila ya kuutarifu uongozi na kutaka shirikisho la soka la Ethiopia lipewe taarifa kuwa Mapunda ni mtoro na lizuie kila mipango ya kucheza soka huko.
Wakati Yanga inafanya hivyo, uongozi wa St George ulituma barua kwa uongozi wa Yanga kuwaomba ruhusa ya kipa huyo aweze kufanya majaribio na timu hiyo. Uongozi wa Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu, Lucas Kisasa ulikiri kupokea barua ya St George.
Hata hivyo, Kisasa alikaririwa akisema kuwa wachezaji wanatakiwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wao Said Maulid ambaye alifuata taratibu zote kwa kuuomba ruhusa uongozi, kuangalia mikataba ya kila upande na sasa anacheza soka Angola bila bughudha.
Kimsingi,Β tunachokiangalia ni kwamba hili la kutoroka halina mantiki na ni ushamba wa kizamaniΒ kwani kuna mengi yanaweza kutokea kwa mchezaji, ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa fedha, kuingia mikataba feki na pengine kupoteza haki za msingi kwa mujibu wa makubaliano yao..
Kwa kuwa tuko kwenye mpito kuelekea kwenye soka ya kulipwa, hata klabu za nje zitakuwa zinatambua kuwa wachezaji wana mikataba na wanatakiwa kufuata taratibu za kuondoka kwao.
Tunashangazwa, na kujiuliza, kwanini mchezaji anakuwa na kiherehere cha kucheza soka nje? Fuateni taratibu, ndipo muondoke.
Itakumbukwa miaka ya nyuma kulikuwa na mitego ya kunasa ama kuwarudisha wachezaji uwanja wa ndege, hayo ni mambo ya kizamani, kinachotakiwa ni mchezaji kufuata taratibu na kupata vibali vyote vinavyoruhusu kucheza soka ughaibuni.
Tukiawaangalia upande wa viongozi, pengine tunaweza kusema hata na wao wanahusika na ndiyo chanzo cha wachezaji kutoroka.
Viongozi wanatakiwa kubadilika. Vitendo vya wao kuwakatalia wachezaji kuondoka, ndivyo hivyo vinavyofanya wachezaji kutoroka.
Wakati mwingine, haiwezekani mchezaji akatoroka vivi hivi, ni kutokana na ukiritiba wa viongozi wa klabu hizo.
Kwa mchezaji kama Ivo Mapunda ambaye ni mchezaji mkubwa na pia kipa mzoefu wa Yanga na Taifa Stars kutoroka kwenda Ethiopia sijui kinafundisha nini kwa wachezaji wengine.
Msisitizo wetu ni kwamba, lazima wachezaji wabadilike kwa kufuata taratibu.
Hivi leo wanasajiliwa na klabu za Ulaya na kwingineko duniani, kweli watatoroka kirahisi namna hii? Huko mikataba ni ya kweli si kama hivi wanavyodhani.
Unasajiliwa Manchester United au Olympique Lyon kesho unapanda ndege unakwenda Uholanzi kuchezea PSV au unakwenda Bayern Munich, kama mchezaji lazima utaonekana una matatizo ya akili.
Kubwa ni kwa kila upande kubadilika na zaidi niΒ viongozi kwa kuwa soka iko katika mpito, uzoefu unaonyesha viongozi wamekuwa hawabadiliki na wakati mwingine ndiyo chanzo cha wao kutoroka.
Kwa mpango huo soka la Tz haliwezi kukua.Ukisikia mtu amekwenda nje ni Ethiopia,kuna mpira gani huko.