Tamasha la Simba limepita mwaka huu, ambapo lilifanyika Septemba 19 kutokana na kuchelewa kumalizika Ligi Kuu Tanzania. Tamasha hilo lilitanguliwa na lile la Yanga maarufu kama Wiki ya Mwananchi. Kwa upande wao Azam FC hawakufanya tamasha lao la Azam Festival kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano ya kimataifa, hivyo wakaenda zao Zambia kujiandaa kwa msimu mpya.
Katika historia ya soka nchini miaka ya nyuma hapakuwepo tamasha la michezo la klabu kongwe za Simba na Yanga, wala la Azam Festival. Lakini chini ya uomgozi wa Hassan Dalali, Simba walianzisha tamasha lao maarufu la Simba Day mnamo mwaka 2009.
Ndipo watani wao wa jadi Yanga nao walikuja na Yanga Day ambayo sasa ni maarufu kama ‘Wiki ya Mwananchi.’ Baada ya matamasha ya Simba na Yanga kuna jingine la mabwanyenye wa Chamazi, Azam fc liitwalo Azam Festival. Tamasha kama hilo pia linafanyika jijini Mbeya ambako likikutanisha timu zote za mkoa huo, Mbeya City, Mbeya Kwanza,Ihefu,Tanzania Prisons na nyingi za madaraja ya chini.
MOTISHA KWA MASHABIKI
Hili ni jambo la kwanza. Matamasha hayo yanawapa nafasi washabiki kupata burudani kutoka kwa timu zao. Washabiki kutoka mikoa mbalimbali hufanya safari kuelekea Dar es salaam kwa minajili ya kushuhudia timu zao.
Mashabiki wanatumia matmasha hayo kama sehemu ya mtoko wao, kama vile kwenda disko au sehemu za burudani. Kwahiyo mashabiki huwa karibu zaidi na timu zao na kuongeza bondi kati yao.
MAPATO YA TIMU
Matamasha yote mawili Simba Day na Wiki ya Mwananchi yameuzwa kwa Azam Tv. Kwamba haki za maudhui ya matamasha hayo zimekuwa chanzo cha mapato kwa timu hizo mbili.
Miaka ya nyuma hapakuwa na kitu kama hiki, badala timu zilikuwa zinajindaa na msimu mpya kwa kucheza mechi za kirafiki pekee au kujiandaa na mazoezi mengine. Lakini sasa timu zimetambua haki za maudhui yao ambayo yanavutia televisheni na redio kutoa fedha amabzo zinasaidia timu hizo kufanyia shughuli mbalimbali.
Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 unapotapika mashabiki mfano 40,000 bado inawapa nafasi Simba na Yanga kuvuna mapato ya viingilio ambayo n fedha zinazosaidia shughuli za timu.
FURSA KWA WANAMUZIKI
Wanamuziki wamepata nafasi ya kutumbuiza katika matamasha ya Simba na Yanga. Kwa mfano katika tamasha la Simba kulikuwa na wanaumiziki kama vile Profesa Jay,Mpoki,Meja Kunte,Joh Makini,Lord Eyes,Mario,Mkojani na Tundaman.
Matamasha yaliyopita tumeshuhudia ushindani wa Diamond Platinumz aliyetumbuiza tamasha la Simba mwaka 2020 na Harmonize aliyetumbuiza Wiki ya Mwananchi mwaka 2020 pia. Wanamuziki hao wanapata fursa ya kujiingizia kipato sababu ya matamasha haya, kwahiyo ni sehemu ya fursa kwao kukonga nyoyo za mashabiki wa soka na wale wa muziki.
NYOTA WAPYA
Washabiki wa timu wana kawaida ya kutaka kuwaona nyota wao wapya kwa mara ya kwanza kabla ya msimu mpya wa 2021-2022. Simba wametambulisha nyota wao kama vile Duncan Nyoni,Peter Banda,Kibu Dennis,Pape Ousmanne Sakho,Sadio Kanoute,Israel Mwenda, Abdulswamad Kassim, Yusuf Mhilu,Henock Inonga,Ahmed Teru, Jeremiah Kisubi.
Kwa upande wa Yanga kulikuwa na Djuma Shaban,Yusuf Athuman,Jesus Muloko, Djigui Diarra,Yannick Bangala,Herieter Makambo, Khalid Aucho,Fiston Mayele,
VIONGOZI KIVUTIO
Matamasha hayo yamewavutia viongozi mbalimbali wa kisiasa ambao wamekuwa wakijitokeza mara nyingi kushiriki. Hii ina maana kubwa katika maendeleo ya mchezo huo angalau kwa mazingira ya Tanzania ambayo bado mafanikio yake ni haba.
Kujitokeza viongozi wa kisiasa kama mawaziri,wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya, wanasiasa na wengine ni chachu ya kuongeza mvuto wa matamasha yenyewe.
Mfano tamasha la Simba Day mgeni mwalikwa alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, huku viongozi wengine akiwemo Mkuu wa wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo akinogesha tamasha hilo.
THAMANI IMEVUKA BODA
Chama cha soka nchini DRC kililazimika kufanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu nchini humo ili kuwapa nafasi TP Mazembe washiriki mchezo wa tamasha la Simba Day.
Septemba 19 TP Mazembe walikuwa na ratiba ya kucheza mchezowa Ligi Kuu, lakini chama cha soka DRC kiliamua kuwapa nafasi kusafiri hadi Tanzania kushiriki sherehe za Simba ikiwa na maana ya kuwapa thamani kubwa waandaaji na soka kwa ujumla.
Ni uamuzi unaoonesha kuwa thamani ya Simba Day au mengine kama Wiki ya Mwananchi au Azam Festival matamasha hayo yamepanda thamani na kuwavutia wageni. Haitashangaza kushuhudia kuuzwa kwa haki za maudhui ya televisheni kwa nchi jirani au inakotoka timu mwalikwa.
WACHEZAJI CHIPIKIZI,WANAWAKE
Katika matamasha haya tumeona timu za vijana nazo zikipewa nafasi ya kuonesha umahiri wao, kama ilivyo kwa timu za wanawake. Vijana wa Simba chini ya miaka 20 ilipepetana na JKU ya Zanzibar na kuibuka mshindi kwa bao 1-0. Vijana hao walionesha umahiri na kuwafurahisha mashabiki wa Simba. Vilevile Simba Queens walishiriki tamasha hilo
KUONGEZEKA MVUTO
Matamasha ya timu za soka yanachangia ongezeko la mvuto miongoni mwa wadau,washabiki na baadhi ya kampuni za udhamini. Kama ambavyo kampuni za kubeti zinavyochukua hatamu katika soka ndivyo ambavyo baadhi zimeanza kuingia katika soko la michezo nchini Tanzania.
Hilo lina maana kuwa klabu zinatakiwa kuongeza hamasa kwa mashabiki ambao ndio chachu ya kupatikana wadhamini wengi katika mchezo wa soka na kuuthaminisha zaidi.
TAMASHA NA JAMII
Katika hatua nyingine matamasha hayo yameonesha sura nyingi ya kuhudumia jamii. Yanga walianza wiki ya mwananchi visiwani Zanzibar kwa kushiriki kutoa huduma kwa jamii. Mashabiki wa Simba tawi la Mafinga mkoani Iringa walikabidhi msaada wa magodoro na vitu vingine kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Makalala ikiwa ni mchango wao kwa jamii.
Comments
Loading…