in , , ,

NI LAZIMA MOURINHO ATATUE TATIZO LA POGBA

Ni pengo la alama 16 sasa linalowatenganisha Manchester City na Manchester United kwenye kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya England. Wakati vijana wa Pep Guardiola wakiwaadhibu Leicester City kwa kipigo cha 5-1 Jumamosi, United walikutana na kipigo chembamba kutoka kwa Newcastle waliojinasua kutoka kwenye ukanda wa kushuka daraja baada ya ushindi huo.

Mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi cha Manchester United, Paul Pogba aliondolewa kwenye dakika ya 66 ya mchezo huo wa Jumapili muda mfupi baada ya Newcastle kupata bao la kuongoza kupitia kwa Matt Ritchie. Hii ni mara ya pili kiungo huyu wa zamani wa Juventus kuondolewa uwanjani wakati timu yake ikiwa nyuma katika michezo mitatu iliyopita ya Ligi Kuu ya England.

Jose Mourinho baada ya kipigo cha juzi alikiri wazi kuwa alimbadili nyota huyo kwa sababu za kimbinu na si sababu ya majeraha. Ni maneno yale yale aliyoyasema baada ya kumuondoa mchezaji huyo wiki mbili zilizopita wakati United ilipochezea kipigo cha 2-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur katika dimba la Wembley.

Pogba anaonekana kushindwa kuyamudu majukumu anayokabidhiwa na Jose Mourinho. Anashindwa vita katika eneo la katikati anakotakiwa kushirikiana na Nemanja Matic kutibua mipango ya wapinzani. Ni udhaifu ule ule alioonesha pia kwenye mchezo dhidi ya Spurs. Lakini hili linaweza kuwa sio kosa la Paul Pogba.

Aina ya uchezaji wa Paul Pogba na uwezo alio nao vinamnyima nafasi ya kumudu majakumu anayokabidhiwa na Jose Mourinho. Ni mchezaji mwenye akili na uweo wa kushambulia zaidi na ni dhaifu mno kwenye kulinda. Anahitaji kukabidhiwa majukumu aliokuwa akikabidhiwa akiwa Juventus ambapo aling’ara kiasi cha kufanikiwa kuwemo kwenye kikosi cha wachezaji bora 11 cha FIFA cha 2015.

Ana uwezo mzuri wa kutengeneza nafasi za mabao, uwezo mzuri wa kupiga chenga na pia uwezo wa kufunga apatapo nafasi. Anazo pasi tisa za mabao kwenye EPL mbaka sasa akizidiwa na Kevi De Bruyne na Leroy Sane pekee. Anatakiwa kutumika mbele zaidi au pembeni eneo la kiungo na si kwenye eneo viungo wawili wakabaji. Pengine kila mfuatiliaji wa soka la England analifahamu vizuri hili ukimtoa Jose Mourinho.

Pogba hana uwezo mzuri wa kunyang’anya mipira kama alivyo Nemanja Matic ama Mfaransa mwenzie N’Golo Kante. Huhitaji kuwa mwalimu wa mpira wa miguu kuutambua udhaifu huu wa Pogba. Pia ni hatari mno kumuweka kwenye eneo la ukabaji kutokana na nidhamu yake ndogo. Mbaya zaidi mwenyewe pia anaonekana kutokufurahia kucheza kwenye eneo hilo na hivyo ni ngumu kung’ara akicheza hapo.

Mbabe wa Jose Mourinho kwenye mchezo wa juzi, Rafael Benitez aliwahi kuwa na mchezaji nyota wa namna hii kwenye kikosi chake. Alikuwa Steven Gerrard enzi zile akiwa Liverpool. Tabia ya Gerrard ya kupenda zaidi kushambulia na kusahau ama kuyapuuza majukumu yake ya kulinda kwenye eneo la kati kati yalimfanya Benitez kushindwa kuutumia vyema mfumo huu wa 4-2-3-1 anaoupenda Mourinho.

Benitez aliamua kumtumia kama kiungo wa pembeni na mara nyingine nyuma ya mshambuliaji. Hapa Gerrard aliweza kung’ara kiasi cha kushinda tuzo kubwa kadhaa kama tuzo ya Machezaji Bora wa Soka La England mwaka 2006. Mourinho ni lazima ajifunze jambo hapa.

Bahati mbaya Mourinho huwaachia hata wachezaji wenye uwezo mzuri wadili na madhaifu yao wenyewe na hayuko tayari kuwatumia katika namna ambazo zinaweza kuwang’arisha ikiwa hilo litamlazimu kubadili mbinu au mifumo yake. Aliwahi kuwapuuza namna hiyo Mohammed Salah na De Bruyne. Sasa wachezaji hao wanang’ara mno kwa kuwa wapo na walimu wanaounda timu kwa kuzingatia aina ya uchezaji wa nyota wao.

Pengine Mourinho anaamini kuwa United inaweza kung’ara bila ya Paul Pogba. Lakini ingefaa angetambua wazi kuwa anaipuuza silaha ya maana. Ni vyema akamtoa kafara Jesse Lingard ili Pogba akasimame nyuma ya Lukaku. Pogba ana thamani ya kafara hii. Vinginevyo abadilike na atumie mfumo wa 4-3-3 ili Pogba acheze kama kiungo wa kushoto ambapo aling’ara mno akiwa na Juventus. Ni lazima Mourinho atatue tatizo la Paul Pogba.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SPURS ANA NAFASI YA KUSHINDA DHIDI YA ARSENAL

Tanzania Sports

WILSHERE, KALAMU YENYE FURAHA NA MWANDISHI MWENYE MAUMIVU