Septemba 25 Simba na Yanga zitapepetana kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Pambano la Ngao ya jamii ndilo utangulizi wa kufunguliwa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mpya wa 2021-2022.
KWANINI YANGA NA SIMBA TENA?
Pambano la Ngao ya Jamii linazipambanisha bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa kombe la FA wa msimu uliopita 2020/2022. Lakini kwa vile bingwa alikuwa ni Simba ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kanuni inasema timu iliyoshika nafasi ya pili kwenye kombe la FA ndio itanyukana na bingwa wake kwenye mchezo wa Nago ya Jamii.
HASIRA ZA YANGA
Yanga wana hasira mara mbili kuelekea pambano hili. Kwanza wanakumbuka kipigo cha 1-0 kwenye mchezo wa fainali ya kombe la FA mkoani Kigoma. Mchezo huo unawapa hasira ya kutaka kulipiza kisasi dhidi ya watani wao Simba. Ni chachu ya uzito wa mechi hiyo.
Pili, Yanga wana hasira za kutolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa hatua za awali baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mechi mbili. Jijini Dar es salaam Yanga walikubali kipigo cha 1-0 kisha jijini Port Harcourt wakapokea kipigo kingine cha 1-0 na kuhitimisha safari yao ya mashindano ya kimataifa. Hivyo Yanga wanalazimika kusubiri hadi msimu ujao kujua kama watashiriki Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho.
HASIRA ZA SIMBA
Mabingwa hawa wa Ligi Kuu walizabwa katika mchezo wa tamasha lao. Ni tamasha la Simba Day ambalo mashabiki walishuhudia mabingwa wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe wakioneshana ubavu na timu yao.
Dakika tisisini zilimalizika kwa Simba kukubali kipigo cha 1-0 lililofungwa na Jean Beleke. Kwa kukubali kipigo katika mechi ya tamasha lao kumeibua hasira ambayo ni lazima wajipoze machungu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.
Vile vile Simba wataingia uwanjani kutaka kuendeleza ubabe wao walioonesha mkoani Kigoma kwenye fainali ya Kombe la FA, lakini wataingia uwanjani bila nyota wao waili Cletous Chama aliyeuzwa Berkane na Luis Miquissone aliyouzwa Al Ahly ya Misri.
KUTAMBIANA WACHEZAJI WAPYA
Katika mchezo huo timu hizo zinatarajiwa kutambiana nani amefanya usajili mzuri kuliko mwingine. Simba watakuwa na nyota wao wapya kama vile Jeremia Kisubi, Deennis Kibu, Israel Mwenda, Peter BandaSadio Kanoute, Pape Ousamane Sakho, Jimson Mwanuke, Abdulswamad Kassim, Duncan Nyoni,Yusuf Mhilu, Henock Inonga.
Yanga watakuwa na mastaa wapya, Djigui Diarra,Yannick Bangala,Herieter Makambo,Yusuf Athuman,Jesus Muloko,Dennis Ambundo,Fiston Mayele,Djuma Shaban, Khalid Aucho,Eric Johora.
VITA VYA MAKOCHA
Nasredine Nabi ana kibarua kigumu kuipa ushindi Yanga mbele ya Simba. Didier Gomes ana kibarua kigumu kutetea ubabe wake mbele ya Yanga. Makocha wote wawili wanafahamu uzito wa mchezo unaozikutanisha timu hizo. Kwa vyovyote mechi hii itakuwa na presha kubwa,ubabe,ufundi na maarifa ya kutosha kutoka kwa makocha hao. ni mifumo gani itawafaa kuibuka na ushindi kati ya iliyomo? Hilo litajibiwa katika mchezo husika.
STAA MPYA
Katika mechi kama hizi lazima kuna mchezaji anaibuka kuwa nyota wa mchezo. Staa huyo mpya anakuwa amepachika bao au mabao au ni yule ambaye amefanya vitu adimu vitakavyobaki akilini mwa washabiki. Kwa namna yoyote ile staa mpya ataonekana katika mechi hii. Lakini haijulikani kama atakuwa ni kati ya wachezaji wageni waliosajiliwa na timu zote mbili au atatokea katika kundi la wachezaji waliozoeleka. Ni vigumu kubashiri hapo.
AJALI MCHEZONI
Katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho ilitokea ajali ya mchezo kwa Mukoko Tonombe kulimwa kadiri nyekundu baada ya kumchezea vibaya mshambuliaji wa Simba, John Bocco. Ajali za namna hii za mchezaji kutolewa nje ya mchezo huchangia kwa kiasi kikubwa kubadili mwelekeo,mbinu au upepo wa mshindi kwa timu.
SIMBA KUWEKA REKODI MPYA?
Simba ndio wamechukua ushindi wa mechi za Ngao za Jamii kwa miaka minne mfululizo tangu mwaka 2017 hadi 2020. Rekodi zinaonesha kuwa Yanga wameshinda mara tano. Mwaka 2001 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2002 na 2003 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2004 mechi hiyo haikuchezwa. Mwaka 2005 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2006-2008 mechi hiyo haikuchezwa.
Mwaka 2009 mshindi alikuwa Mtibwa Sugar. Mwaka 2010 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2011 na 2012 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2013 na 2014 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2015 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2016 msindi alikuwa Azam fc.
Takwimu zinaonesha kuwa Simba na Yanga zimewahi kuchukua kombe hilo mara tatu mfululizo. Yanga walifanya hivyo mwaka 2013, 2014 na 2015. Nao Simba wakajibu mapigo kwa kuchukua mara nne mfululizo mwaka 2017, 2018, 2019,2020. Na sasa wanafukuzia taji la tano, na endapo watafanikiwa watakuwa wameweka rekodi ya aina yake tena mbele ya Yanga ambayo haijashinda tangu mwaka 2015.
Comments
Loading…