in

Neymar, Mbappe na Di Maria ni MSN ndani ya PSG

PSG

Kuna wakati maajabu hutokea mara moja tu na huchukua muda mrefu tena hayo maajabu kuonekana tena. Inawezekana maajabu ya kipaji cha Pele yaliyotokea mara moja tu.

Watu wakafurahia kumuona mzee huyu. Wakajuvunia kumtazama na wakamshangilia kila alipokuwa anafunga magoli kwenye mechi mbalimbali. Kipaji chake kilionekana cha maajabu.

Kilionekana ni cha maajabu kwa sababu kabla hukukuwahi kutokea kipaji kikubwa kama kile. Watu wakijivunia sana na maajabu ya kipaji  chake.

Lakini baada ya muda mfupi kipaji chake kilipotoea. Umri ukamlazimisha atumie muda mrefu nje ya uwanja kuliko kutumia muda mrefu ndani ya uwanja.

Kustaafu kwa Pele kulituchukua miaka mingine mingi kumpata mtu ambaye alikuwa anakaribiana na kipaji cha Pele. Mtu mwenyewe ni Diego Maradona.

Kipaji kingine cha maajabu. Kipaji ambacho ni nadra sana kutokea mara kwa mara. Ni kipaji ambacho hutokea mara moja baada ya miaka mingi.

Huyu naye alituburudisha, tukafurahia uwepo wake na tukawa na ushabiki mkubwa juu yake kwa sababu tulihusudu kipaji chake kikubwa.

Kipaji hiki kilipita. Dunia ikakaa miaka mingine bila kushuhudia kipaji kingine chenye maajabu kama Diego Maradona. Wakati dunia ikiwa na upweke Mungu akatutelea Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Bahati nzuri hawa waliletwa kipindi kimoja. Wakabaki kuwa wanashindana wenyewe kwa wenyewe, wakaweka utawala wao katika mpira wa miguu.

Dunia ikagawanyika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza iliitwa Cristiano Ronaldo na sehemu ya pili ikaitwa Lionel Messi. Rasmi wakaweka tawala mbili katika uso wa dunia.

Na kwenye kipindi hiki cha utawala wao walijenga utatu wao mtakatifu kila mmoja. Alianza Cristiano Ronaldo. Huyu alitengeneza utatu wake mtakatifu pale Real Madrid.

Utatu ambao ulikuwa tishio. Vilabu vingi viliogopa kukutana na utatu huu kwa sababu ulikuwa utatu usiokuwa na huruma hata kidogo. Hawakuwahi kumhurumia kipa au beki yoyote.

Utatu huu ulikuwa na miguu ya wanaume watatu ambao walikuwa wakatali sana. Gonzalo Higuan, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo mwenyewe.

Utatu huu katika msimu wa mwaka 2011/2012 ulifanikiwa kumaliza msimu ukiwa na magoli 118 huku ukibeba mpaka michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.

Wakati dunia ukiwa unajiuliza ni lini utapatikana utatu mwingine mtakatifu , Barcelona waliamua kutuletea Neymar kwenye ligi ya Hispania.

Neymar aliwakuta Luiz Suarez na Lionel Messi wakiwa kwenye timu tayari. Kwa pamoja walijenga utatu mtakatifu ambao ulijulikana kama MSN.

Utatu huu ulikuwa wa kutisha zaidi kuliko utatu wa kina Gonzalo Higuan, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo, wakati utatu huu wa Real Madrid ukimaliza na magoli 118 kama msimu wao bora, utatu wa Barcelona ulimaliza msimu ukiwa na goli 122 msimu wa mwaka 2014/2015.

Ndiyo msimu ambao walichukua mpaka ligi ya mabingwa barani ulaya. Lakini kwa bahati mbaya “MSN” ilivunjika baada ya Neymar kwenda PSG ya Ufaransa.

Barcelona ikakosa tena utatu ule wa kutisha. Neymar kwa sasa yupo PSG, jana wamefanikiwa kuingia fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya baada ya kuifunga RB Leipzig ya Ujerumani.

Habari kubwa siyo PSG kuingia fainali yake ya kwanza tangu mwaka 1995. Inshu kubwa hapa ni PSG kuwa na utatu mtakatifu ambao unaonekana tishio kubwa pia.

Utatu huu unammweka kwa pamoja Neymar, Mbappe na Di Maria. Utatu huu unaanza kufananishwa na utatu wa Neymar , Messi na Suarez.

Swali kubwa linalobaki ni kama Neymar,  Mbappe na Di Maria watafanikiwa kuchukua ligi ya mabingwa barani ulaya kama ule utatu wa Barcelona na Real Madrid ulivyofanikiwa kuchukua ?

ReplyForward

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Yanga Simba

Ratiba VPL Simba, Yanga Uso kwa Uso

Ndemla

Simba siyo sehemu sahihi kwa Ndemla