Na isemwe kuwa mfalme mpya ameingia katika Ligi Kuu England, lakini anaelekea kuzitikisa karibia Ligi zote za Ulaya. Swali ambalo msomaji wa TanzaniaSports utakuwa unajiuliza ni kwa namna gani Newcastle wanaweza kutikisa Ligi za Ulaya wakati hawashiriki mashindano ya Europa,Conference League wala Champions League?
Jambo moja unalotakiwa kufahamu ni kuwa mwekezaji yoyote huwa amegawa muda,rasilimali na mipango ya muda mfupi na mrefu. Kwahiyo tajiri mpya wa Newcastle United cha kwanza ni kufanya mipango ya muda mfupi ikiwemo usajili wa nguvu ili kuimarisha timu hiyo ifikapo Januari mwaka 2022.
Swali la pili utakalojiuliza je usajili wa mwezi januari utaisaidia vipi Newcastle United ambayo inasua sua kwenye EPL? Jibu ni kwamba kitu cha kwanza kwa tajiri ni kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu, yaani haishuki daraja, halafu kitu cha pili ni kuhakikisha inakuwa na wachezaji ambao wanaandaliwa kufanya vizuri msimu ujao 2022/2023.
Ripoti mbalimbali kutoka EPL zinaonesha kuwa Newcastle United imepania kuwasajili nyota hasa wa Ligi Kuu Italia, ambako mlengwa wa kwanza anatajwa kuwa Federico Chiesa wa Juventus.
Inaelezwa kuwa kiasi cha pauni milioni 250 kimetengwa kwa ajili ya kusajili nyota wakubwa. Timu hiyo inategemewa kufanya kufuru kwenye usajili kama walivyofanya matajiri wa Manchester City na PSG.
MASTAA WANAOSAKWA NEWCASTLE
Kama nilivyoeleza hapo juu, taarifa za kimichezo zinamtaja Federico Chiesa kama nyota wa kwanza anayewindwa na vibopa wa Newcastle United. Na kwamba vibopa hao wamepania kuivuruga Ligi Kuu Italia kwa kuwanyakua nyota kibao ili waende kwenye dimba la St.Jame’s Park.
Mwingine ni beki kisiki wa Juventus Matthijs de Ligt na Aarn Ramsey ni miongoni mwa mastaa wanaowindwa na Newcastle United. Lakini kibarua pekee kitakuwa kwa Newcastle United kuweza kuwashawishi Juventus kumruhusu beki wake De Ligt kuwahama Kibibi Kizee cha Turin.
Lakini usajili wa Ramsey unaonekana kuwa rahisi kwa sababu anaweza kuondoka kama mchezaji huru ambapo mkataba wake unaelekea ukingoni, huku Juventus wakiwa na uhakika wa kupunguza kiasi cha Euro milioni 7 ambacho kilikuwa kinatumika kama mshahara wa Ramsey.
Nyota wengine wanaosakwa na Newcastle ni wale wanaokipiga katika klabu kongwe ya AC Milan. Mojawapo ni Franck Kessie ambaye mkataba wake unamalizika Juni 2022 na bado hajaingia wala kukubaliana na ofa mpya aliyopewa na AC Milan.
Kwa upande wa Inter Milan nayo haipo salama kwani kuna uwezekano ikapotez anyota wake ambao wanaweza kuelekeza Newcastle United kama mwanzo mpya wa wababe wa soka barani Ulaya. Beki Stefan de Vrij na kiungo Marcelo Brozovic wote kwa pamoja wamekuwa kwenye rada za Newcastle United na uwezo wa kuwang’oa hapo utakuwa ni kiasi cha fedha kitakachotolewa na wanunuzi.
Ukiangalia wachezaji wanaosakwa na Newcastle utagundua wengi wanatoka nje ya EPL, lakini hilo halimaanishi kuwa hakuna wa kununuliwa na klabu hiyo.
Eneo jingine ni kocha mpya wa Newcastle United ambako jina la Riberto Mancini limetajwa mara kwa mara katika ripoti za kimichezo kuonesha kuwa ndiye mtu anaywindwa zaidi na wamiliki wapya.
Kocha huyo amewahi kuinoa Manchester City kabla ya kwenda kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia, ambaye mwezi Julai mwaka huu alifanikiwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Ulaya akiwa na rafiki yake wa miaka takribani 40 hivi Gianluca Vialli.
Mancini anafahamika kama mtu sahihi katika kuanzisha mpango wa maendeleo ya timu, lakini changamoto iliyopo sasa ni kumshawishi kuachana na kibarua cha kuinoa Azzuri kwa sasa.
Hata hivyo orodha ya makocha watakaotamani fedha za Newcastle United ni wengi. Changamoto itakuwa ni kocha gani mwenye uwezo wa kuleta mafanikio kwa muda mfupi, kwa sababu timu zianzonunuliwa na vibopa kwa kawaida huwa na uvumilivu ndani ya misimu miwili tu.
Baada ya hapo kocha kama hajashinda taji lolote lazima afungashiwe virago, kwahiyo fukuza fukuza ni jambo wanalofahamu makocha wengi ila kitakachowapeleka klabuni hapo ni fedha tu. Ni kocha gani atakuwa wa kwanza? Ni mchezaji gani atakuwa wa kwanza staa kutua Newcastle United? Majibu ya maswali haya tutayapata ifikapo Januari mwaka 2022. Sio sasa lakini sio mbali sana.
Comments
Loading…