in , , ,

Newcastle inauzwa

Newcastle

Hatua za mchakato wa mauzo ya klabu ya Newcastle zinaonekana kusogea mbele kwa kiasi kikubwa.

Tayari nyaraka zinaonesha kwamba mmiliki Mike Ashley ameingia kwenye mpango huo wa kutia saini na mnunuzi mtarajiwa, Amanda Staveley. Mwanamama huyu anaongoza kwenye dili ya zabuni inayowahusisha mfuko wa Saudia Arabia na Reuben Brothers.

Inaaminika kwamba klabu hiyo inauzwa kwa pauni milioni 300 na nyaraka zenyewe za mikataba ya kuuziana zina kurasa 31, ikielezwa kwamba muda mfupi baadaye zingewasilishwa Companies House, ikiwa ni kuweka mchakato mzima katika msingi wa kisheria kwa ajili ya dili zima kukamilishwa.

Nyaraka hizo zinajumuisha mpango wa pauni milioni 150 kuhusiana na kampuni ya Staveley – PCP, Capital Partners na suala zima la shauri la muda mrefu dhidi ya benki moja kubwa. Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) nayo imejulishwa juu ya uwezekano wa kufanyika kwa dili hilo, na inatambulika sasa kwamba kuna michakato mingine iliyoanza tayari kuhakikisha mambo yanakwenda shwari.

Awali, dili hilo linaelezwa kwamba lilikuwa linafikia kima cha thamani ya £340m, lakini mambo yakabadilika. Kwa mwenendo wa sasa, washabiki wa Newcastle watafurahi kuona Ashley akiondokana na klabu yao aliyoichukua tangu 2007.

Washabiki wamekuwa wakimlalamikia kwa kutotoa fedha za kutosha kuiimarisha kwa kununua wachezaji, jambo lililomsababisha kocha wao, Rafael Benitez kuondokana naye, wakivutana kwenye msimu wa usajili.

Kadhalika washabiki wanamlalamikia tajiri huyo kwa jinsi alivyoshughulikia masuala ya klabu tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu. Klabu tayari wameshawatoza washabiki kwa ajili ya tiketi za msimu ujao wakati msimu huu wenyewe kuna utata wa jinsi utakavyomalizika, ikidhaniwa mechi 92 zilizobaki zitachezwa bila washabiki.

Katika utaratibu wake wa kawaida kuhakikisha kwamba matumizi yanakuwa kidogo, Ashley aliamua kuwaweka wafanyakazi wasiokuwa wachezaji katika mpango wa kuwa likizo ya lazima ili kupata fungu kutoka serikalini, wakati huu klabu na wachezaji wakiomba kuchangia kiasi cha gharama za janga hili kubwa.

Habari za mfuko huo wa Saudi Arabia kutaka kuchukua klabu hii zilianza tangu Januari. wakati huo ilidaiwa kwamba mazungumzo yalikuwa yakifanyika, lakini mwafaka haukuwa karibu kutokana na mkanganyiko fulani, ikiwa ni pamoja na rekodi ya Saudia juu ya haki za binadamu iliyotolewa na Amnesty International.

Mtaalamu w masuala ya fedha katika michezo, Kieran Maguire anasema kwamba hatua zinazochukuliwa sasa ndizo hufanyika wakati wa kuuza klabu na kwamba inaelekea mambo yanakwenda.

Hata hivyo, Maguire anasema kwamba tatizo na Ashley ni kwamba huwezi kusema mambo yanakamilika hadi uone nyaraka za mwisho kabisa, vinginevyo inakuwa bado ni mpango, kwa sababu Ashley anaweza ‘kuchomoa’ muda wowote ule

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mabosi Arsenal wajitolea

Tanzania Sports

Klabu EPL hali mbaya