in , , , ,

Mwisho wa awamu ya tatu ya GALACTICO, tusubiri awamu ya nne ya GALACTICO

Kipi kinachokuja kichwani mwako ukisikia neno GALACTICO?, Hapana shaka ni Real Madrid ndiyo inayokuja kichwani kwako.

Klabu kubwa duniani, ndiyo klabu ambayo wachezaji wengi huiona kama sehemu ya kwenda kufanya HIJA ya dini inayoitwa MPIRA.

Ndiyo klabu ambayo wachezaji wengi hutamani kuvaa jezi yake. Leo hii Pierre-Emirick Aubameyang yupo Arsenal lakini moyo wake unalia sana.

Kila akifikiria umri wake wa miaka 29 huwa anaona kuna kitu ambacho hajakifanya akiwa kwenye dunia hii ya mpira.

Kuna kitu ambacho kinamfanya aumie sana mpaka sasa hivi. Ndoto yake kubwa ilikuwa kuichezea Realmadrid, lakini hapana shaka ndoto yake kwa sasa ni ngumu kutimia.

Kitu hiki Eden Hazard hataki kukiona kikitokea kwenye maisha yake kwa sasa. Anatamani sana kutimiza kuchezea klabu yake ya moyoni.

Hatamani kuona muda umeenda bila yeye kuvaa jezi zenye rangi nyeupe kama ambavyo Pierre-Emerick Aubameyang alivyofanya.

Hataki kabisa kuifanya hii dhambi ndiyo maana haogopi kusema hadharani kuwa ana ndoto ya kuchezea Realmadrid.

Anaongea ukweli, ukweli unaouma. Inawezekana mashabiki wa Chelsea wakawa wanaumia na kauli za Eden Hazard.

Lakini hakuna chochote ambacho wanaweza kukifanya ili kuuziba mdomo wa Eden Hazard. Mdomo unaokera sana kwao wao.

Lakini ndiyo mdomo ambao unaongea ukweli unaotoka moyoni. Ukweli ambao ulianza kuumbwa na neno MAPENZI. Yalianza kuzaliwa mapenzi kwanza kwenye moyo wa Eden Hazard ndiyo maana leo hii anaongea hivo.

Mapenzi haya yalianza kujengwa tangu miaka ya 1960 na miaka 1980 na mtu muhimu katika klabu ya Realmadrid. Mtu mwenyewe ni Santiago Bernabeau.

Mtu ambaye ni nembo kubwa sana katika klabu ya Realmadrid. Ndiyo maana haikuwa ajabu kwa Real madrid kuupa uwanja wao jina la Santiago Bernabeau.

Gwiji wa zamani wa Real madrid, mshambuliaji hatari na nahodha imara wa Real madrid. Nahodha ambaye alifanikiwa kuiongoza Realmadrid ndani na nje ya uwanja.

Ingawa mafanikio yake nje ya uwanja ndiyo yalikuwa nguzo kuu ya Real madrid. Huyu ndiye aliyeifanya Real madrid itazamike hivi kama inavyotazamika Leo.

Huyu ndiye aliyeifanya Realmadrid iwe kama Hijja ya mpira kila mchezaji kutamani kwenda kufanya ibada ya soka ya ku-Hijji.

Huyu ndiye aliyewafanya hata kina Eden Hazard wawe wanaonesha hisia zao waziwazi kwa Realmadrid bila kujali waajiri wao watawafikiriaje.

Kwa kifupi huyu ndiye aliyesababisha leo hii likitajwa neno Galactico taswira inayokuja kichwani mwake iwe Real madrid.

Huyu ndiye aliyeuaminisha ulimwengu kuwa Realmadrid ni sehemu ambayo wachezaji wakubwa wenye vipaji kubwa ndiyo wanastahili kuvaa jezi ya timu hii.

Kwa kifupi ndiye aliyeanzisha utaratibu wa kusajili wachezaji nyota kwenye klabu ya Realmadrid. Utaratibu ambao ulileta mafanikio makubwa kwenye klabu ya Real madrid.

Wakati akiwa raisi wa Realmadrid,Santiago Bernabéu aliwasajili Alfredo Di Stéfano, Ferenc Puskás, Raymond Kopa, José Santamaría na Francisco Gento.

Wachezaji ambao waliiwezesha Realmadrid kubeba vikombe sita vya ulaya na kumi na mbili vya La liga katika kipindi chake cha uongozi.

Aliibeba Realmadrid na kuiweka kwenye eneo la juu kabisa kisoka duniani. Miaka 35 ilimalizika, miaka ambayo ilimpa nafasi yeye ya kuitumikia Realmadrid.

Miaka ambayo ilileta utambulisho wa neno Galactico katika mpira. Tukaifahamu Real madrid katika upekee huo.

Akili za Florentino Perez zilikuwa na Galactico awamu ya pili na ya tatu. Galactico ya kisasa. Wakati Florentino Perez anafikiria namna ya kuwa raisi wa Real madrid njia pekee aliyoitumia ni kutumia neno Galactico.

Sawa kipindi cha Lorenzo Sanz , Real madrid iliweza kubeba kombe la ulaya mwaka 1998 na 2000, lakini kuna kitu kilikuwa kinapelea kwa raisi Lorenzo Sanz.

Kitu chenyewe ni Realmadrid kutokuwa na wachezaji nyota, hapa ndipo alipopaona Florentino Perez ili aweze kupitia.

Alitoa ahadi ambayo ilikuwa na ukichaa mkubwa ndani yake. Ahadi ambayo ilikuwa ngumu kutekelezeka kwa akili ya kawaida.

Kwa Florentino Perez hakuna kinachoshindikana kwenye dunia ya mpira. Aliwaahidi kumleta Luiz Figo. Mchezaji ambaye kwa kipindi kile alikuwa nyota.

Siyo kuwa nyota tu, alikuwa mchezaji wa Barcelona. Kitu ambacho ndicho kilikuwa kinaleta ugumu kwenye biashara hii.

Yani Barcelona wakuuzie mchezaji wao nyota tena kipenzi tena kwa adui yao mkubwa?, yani ni sawa kwa sasa Lionel Messi auzwe Realmadrid.

Ni kitu kigumu kutokea na ni kitu ambacho hakiwezi kufikirika kabisa, lakini Florentino Perez aliwalazimisha watu wafikirie kuwa inaweza kutokea.

Kweli, tukawaza kuwa inaweza kutokea. Kazi ikabaki kwake tu nayo ni kumleta Luis Figo kwenye nyasi za Santiago Bernabeau.

Alifanikiwa kwenye hilo. Luiz Figo akavunja ada ya uhamisho ya dunia. Akawa mchezaji ghali duniani kwa kipindi hicho.

Florentino Perez akavunja benki yake tena akamleta Zinedine Zidane, ambaye alivunjwa rekodi ya uhamisho ya Luiz Figo.

Hakukomea hapo, akamleta Ronaldo De Lima, akamvuta sharobaro wa England David Beckham.

Timu ikawa imara ndani na nje ya uwanja. Ndani wakachukua kombe la klabu bingwa barani ulaya kwa goli la kukumbukwa la Zinedine Zidane.

Nje wakauza sana jezi. Utaachaje juuza jezi wakati una mtu kama David Beckham? Mtu pekee ambaye alikuwa anacheza mpira kwa kutumia uso wake na siyo miguu yake kama wengi wanavyofanya.

Awamu ya tatu ilifika, Perez alileta kina Kaka , mchezaji bora wa dunia kipindi hicho, akaja Ronaldo , wakafuata kina Modric, Rodriguez, Di Maria, Kroos, Ozil, Bale na wengine.

Kizazi hiki ndicho kilichobeba kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya mara tatu mfululizo chini ya Zinedine Zidane.

Tayari kinaelekea mwisho wake. Realmadrid wanakilazimisha tu kwa sasa kuendelea kuwepo kwenye nyasi za Santiago Bernabeau.

Tamati yake inaonekana kabisa, na hitaji la Galactico awamu ya nne inaonekana. Awamu ambayo itakuja na kizazi kipya na siyo hiki ambacho kinaonekana kufikia mwisho.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mambo ya Monaco yamwendea kombo Thierry Henry

Tanzania Sports

Simba walikuwa sahihi kupeleka kikosi cha kwanza MAPINDUZI