*AFCON iliyoanza Sudan 1957 yaenda Afrika Kusini
*Mataifa matatu yalianza kushiriki, leo fainali ni 16
Michuano ya 29 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inaanza Januari 19.
Kwa mara ya pili, Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa michezo hiyo itakayofanyika jijini Johannesburg, na miji mingine mikubwa ya Afrika Kusini.
Baada ya mwaka 1994 kuondokana na siasa za ubaguzi wa rangi zililoitenga, Afrika Kusini chini ya Rais Nelson Mandela iliandaa michezo hiyo mwaka 1996.
Hii ni michezo iliyoanza 1957, ikiandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambapo wenyeji wa kwanza walikuwa Sudan, michuano ikafanyika Khartoum.
Enzi hizo ni nchi tatu tu zilishindana, nazo zilikuwa ni wenyeji Sudan, Misri na Ethiopia. Afrika Kusini waliokuwa wameshajumuishwa, walizuiwa ushiriki kutokana na siasa yao.
Haya ni mashindano ambayo hufanyika kila baada ya mwaka mmoja. Hata hivyo, mwaka jana yalifanyika Gabon na Guinea ya Ikweta na mwaka huu yanafanyika tena, lengo likiwa kubadili yasiangukie
mwaka wa Kombe la Dunia la FIFA linalofanyika kila baada ya miaka minne.
Michuano hii imetoka mbali, ambapo imepita kwenye awamu ya kukutanisha mataifa manne, sita kabla ya kuwa ya mataifa manane mwaka 1968 nchini Ethiopia.
Nchini Senegal mwaka 1992, michuano hii ilishirikisha mataifa 12, lakini tangu mwaka 1996 kule nchini Afrika Kusini, zinashiriki nchi 16.
Hata hivyo, katika fainali hizo za 1996, licha ya timu 16 kufuzu, zilishiriki 15 kwa sababu mabingwa watetezi – Nigeria – walijitoa.
Walijitoa wakati wa mkesha wa ufunguzi, kwa sababu ya msigano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya utawala wa kijeshi wa hayati Jenerali Sani Abacha na wa mzee Madiba.
Ni kwa bahati mbaya pia, michuano ya 27 iliyofanyika Angola mwaka 2010 ilishirikisha timu 15 badala ya 16, kwani Togo walijitoa siku chache kabla ya uzinduzi.
Walichukua hatua hiyo kutokana na kile walichoita kiwewe na mshituko baada ya msafara wa timu yao kushambuliwa, wawili wao kuuawa kwa risasi walipokuwa wakikatiza mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola.
Inaweza kusemwa kwamba historia ya michuano hii inazigusa zaidi timu tatu; Mafarao wa Misri, Black Stars wa Ghana na Simba Wasiofugika wa Cameroon.
Katika michuano 28 iliyopita, nchi tatu hizo zimefanikiwa kutwaa kombe mara 15 kati yao; Misri mara saba, kati ya hizo tatu mfululizo, wakiwa pia wameandaa mara nne.
Ghana wameshinda mara nne na wameandaa mara nne kadhalika, lakini ushindi na uandaaji havikufungamana.
Cameroon walikuwa wenyeji katika michuano ya nane tu, yaani mwaka 1972 na Simba wake wametwaa kombe mara nne.
Walitawazwa kuwa wafalme nchini Cote d’Ivoire mwaka 1984, ilipofanyika Moroco mwaka 1988, kule Ghana na Nigeria mwaka 2000 na nchini Mali mwaka 2002.
Mabingwa waliopita na waliokuwa wakipewa nafasi kubwa kutwaa tena, Cameroon, Misri na Cameroon walishangaza wengi kwa kushindwa kufika fainali za mwaka jana.
Ni ajabu bado, kwamba Mafarao wa Misri na Simba Wasiofugika wa Cameroon mwaka huu hawashiriki nchini Afrika Kusini, na wametolewa hatua za awali na nchi zilizodhaniwa kuwa ni vibonde.
—————————————————————————————————————-
Group Stages:
Sat 19 Jan South Africa V Cape Verde 1600gmt Jo’burg
Sun 20 Jan Ghana v DR Congo 1500gmt Port Elizabeth
Tues 22 Jan Ivory Coast v Togo 1500 gmt Rustenburg
Thurs 24 Jan Ghana v Mali 1500 gmt Port Elizabeth
Fri 25 Jan Zambia v Nigeria 1500gmt
Mon 28 Jan DRC v Mali 1700gmt Durban
Quarter Finals:
Sat 2 Feb 1500g Port Elizabeth
Sat 2 Feb 1830g Durban
Sun 3 Feb 1500g Rustenburg
Sun 3 Feb 1830g Nelspruit
Semi Finals
Wed 6 Feb 1500g Durban
Wed 6 Feb 1830g Nelspruit
Final
Sun 10 Feb 1800g Jo’burg
Comments
Loading…