Pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/2022 linafunguliwa rasmi Septemba 27 mwaka huu kwa mchezo wa kati ya Mtibwa Sugar na Mbeya Kwanza utakaochezwa saa nane kamili mchana mjini Morogoro. Baada ya mchezo huo ifikapo saa 10 jini Namungo FC watawakaribisha wageni wa Ligi hiyo Geita Gold, huku Coastal Union wakipepetana na Azam FC.
Mechi zenye mvuto Ligi Kuu Tanzania
TANZANIASPORTS inakuleta uchambuzi wa mechi kali ambazo zinatarajiwa kuwasisimua washabiki wengi wa kandanda nchini Tanzania katika msimu wa 2021/2022.
WAGENI KUFUNGUA DIMBA
Kwa mujibu waratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeonesha kuwa timu mbili ngeni yaani ambazo zimepanda msimu huu, Geita Gold na Mbeya Kwanza zitatupa karata zao ugenini. Ni wageni wa Ligi ambao watakuwa ugenini katika mechi zao za kwanza. Wakati Mbeya Kwanza watakuwa Morogoro, wenzao Geita Gold watatoana jasho na Namungo huko mkoani Lindi. Mechi za wageni hao zinatarajiwa kuwa kivutio zaidi kuliko Coastal Union dhidi ya Azam FC.
MBEYA CITY vs TANZANIA PRISONS
Ukisikia mechi ya kibabe basi hii ni kiongoni mwake. Wababe wawili kutoka jijini Mbeya watakuwa na shughuli moja tu kuonesha nani ni mwamba wa kandanda katika jiji hilo. Ndani ya dimba la Sokoine kutawaka moto, ambapo Wajelajela Prisons watakuwa wageni wenye kazi ya kupambana na mabosi wa jiji yaani Mbeya City saa 19 jioni ifika Septemba 28 mwaka huu. Itakuwa mechi ya kufungua pazia la Ligi Kuu kwa jiji la Mbeya.
BIASHARA UNITED vs SIMBA
Saa kumi jioni ya Septemba 28 mwaka huu mabingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2020/2021 watakuwa na kazi ya kutetea ubingwa wao mbele ya wenyeji wao Biashara United mkoani Mara. Utakuwa mchezo wa kwanza ambao Simba watataka kuanza vizuri, huku Biashara United wakitaka kumaliza ubabe wa wekundu wa msimbazi. Kumbwa zaidi timu zote mbili bado zipo katika mashindano ya kimataifa, ambapo Biashara United imeingia hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho, huku Simba wakisubiri kuchuana na mpinzani wao katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni mechi inayotarajiwa kuwa na mvuto zaidi kuliko nyingine ya siku hiyo hiyo kati ya Dodoma Jiji na Ruvu Shooting.
KAGERA SUGAR vs YANGA
Yanga wataanza kampeni ya kusaka taji la 28 la Ligi Kuu Tanzania bara wakiwa ugenini kwenye dimba la Kaitaba mkoani Kagera. Wenyeji wao Kagera Sugar watakuwa chini ya kocha Francis Baraza ambapo watakuwa na kazi moja tu; kuhakikisha hawanyamazishwi na vijana wa Jangwani na Twiga kutoka Dar es salaam. Mchezo huo utachezwa Septemba 29 saa 10 jioni, huku wenzao Polisi Tanzania watawakaribisha KMC saa nane mchana. Hii ni mechi ya kwanza na itaonesha mwanzo wa mwelekeo wa mabingwa hao wa zamani Yanga na zaidi itakuwa kuangalia namna gani benchi ghali za ufundi likiifanya timu hiyo kuwa hatari mbele ya wapinzani wao.
YANGA vs GEITA GOLD
Yanga watacheza mchezo wao wa kwanza katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Geita Gold ya mkoani Geita ambao utapigwa Oktoba 2 mwaka huu. Utakuwa mchezo wa kwanza kwa Geita Gold dhidi ya Yanga utakaochezwa saa moja usiku katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam. Je wageni wataisimamisha Yanga au Yanga wataonesha umahiri wao kusaka taji la Ligi Kuu? Itajulikana hapo.
MBEYA CITY vs MBEYA KWANZA
Nani ataibuka mbabe katika mechi hii? Jibu linasubiriwa ifikapo Oktoba 3 mwaka huu kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya. Hii itakuwa ‘derby’ ya pili katika jiji hilo baada ya ile ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Hakuna kingine unachoweza kusema kuwa hii itakuwa mechi ya kukata na shoka kwa sababu itahusisha timu za jiji moja na ambazo zinataka kutangaiziana ufalme wa soka. Ni kivutio kikubwa.
KAGERA SUGAR vs MBEYA CITY
Oktoba 16 mwaka huu Kagera Sugar watashuka dimba la Kaitaba kuchuana na Mbeya City. Saa nane mchana mashabiki watashuhudia umahiri wa timu zote mbili zenye majina makubwa katika mchezo wa soka nchini. Hii ni moja ya mechi kali nje ya vigogo wa soka wa Ligi Kuu Tanzania.
KMC vs YANGA
Saa kumi jioni ya Oktoba 19 mwaka huu ‘watumishi wa serikali’ KMC wataikaribisha Yanga katika pambano la kwanza baina yao. KMC watataka kuonesha kwanini walikuwa timu iliyowasumbua Yanga msimu uliopita. Kwahiyo litakuwa zoezi la kudhihirisha umwamba huku Yanga wakiwa na nia moja tu ya kupata pointi tatu muhimu.
SIMBA vs POLISI TANZANIA
Popote penye majina ya Yanga na Simba pana mvuto wake. Kwahiyo Oktoba 20 mwaka huu katika dimba la Benjamin Mkapa Simba watakuwa wenyeji wa ‘wacheza kwata’ Polisi Tanzania kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu. Hii itakuwa ni kama mechi ya Simba dhidi ya Metacha Mnata, ambaye alikuwa golikipa mahiri wa Yanga msimu uliopita. Itakuwa mechi ambayo Metacha atatkiwa kuonesha umhiri wake ili awakumbushe wadau wa soka kuwa yeye ni nyanda mzuri kati ya walipo Ligi Kuu. Mchezo huo utachezwa saa moja usiku.
KAGERA SUGAR vs MTIBWA SUGAR
Ndugu,jamaa na marafiki wanaozalisha sukari kwa wingi nchini Tanzania, watakuwa na kazi moja kuwaonesha nani ni mahiri kuliko mwenzake. Hawa ni ndugu ambao wanalima miwa huko Kagera na Morogoro. Ni mechi ya ndugu ambayo itakuwa kivutio kutokana na uhusiano uliopo kati ya timu hizo. Ni saa kumi jioni ndani ya dimba la Kaitaba mkoani Kagera. Na zaidi kocha wa Mtibwa Sugar Joseph Omog raia wa Cameroon ambaye amewahi kuzinoa Azam na Simba kwa nyakati tofauti atakiongoza kikosi chake siku hiyo.
YANGA vs AZAM FC
Ni saa moja usiku wa oktoba 30 ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Mtanange huu unatarajiwa kuwa wa kukata na shoka. Itakuwa mechi kati ya kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina na Yanga. Yanga wakiwa na kocha Nabi watakuwa na kazi ya kumuonesha umwamba Lwandamina na kudhihirisha kuwa wao ni watemi wa Ligi Kuu. Itakuwa mechi ya kukata na shoka, huku timu zote zikiundwa na wachezaji wengi wa kigeni. Itavutiia.
SIMBA vs COASTAL UNION
Sijui itakuwaje kwa rafiki yangu Nassoro Binslum ikiwa Caostal Union watachezeshwa na kuambulia kipigo kama cha msimu uliopita cha 6-0. Kilikuwa kipigo kikali sana, lakini msimu huu 2021/2022 wanaingia wakiwa na kocha Melo ambaye bila shaka atazuia ukali wa Simba. Mechi hii hutafsiriwa kuwa ni kama kaka na mdogo kwa vile kuna udugu wa karibu kati ya Coastal na Simba. Ni lugha za mashabiki, lakini uhalisi unaonesha kila mmoja atahitaji pointi tatu na heshima. Itasisimua.
YANGA vs RUVU SHOOTING
Haiwezi kuwa mechi kali sana lakini itakuwa na mvuto wa aina yake. kocha wa Ruvu Shooting Charles Mkwasa atakabiliana na waajiri wake wa zamani Yanga ambao watataka kuchukua pointi 3 kutoka kwake. Kwa kawaida mechi zao zinakuwa na mvuto,ushindani,ufundi na hekaheka nyingi. Bila shaka Yanga watazitaka pointi tatu kama ilivyo kwa wapinzani wao. Wengi wanasubiri Novemba 2 ifike ili waone matokeo.
SIMBA vs NAMUNGO
Hakuna namna unavyoweza kupuuza mechi kama hii. Simba watakuwa na kazi ya kuoneshana ubabe na wapinzani wao hawa. Labda ingekuwa ile timu ya zamani ya Kariakoo Lindi ambayo ilizitetemesha timu mbalimbali za Ligi Kuu na kuzinyima pointi katika uwanja wake wa nyumbani. Lakini Novemba 3 mwaka huu Namungo watakuwa na kibarua kigumu cha kuwanyamazisha Simba katika mchezo utakaochezwa saa moja usiku. Ndiyo, wakati huo uwanja wa Kassim Majaliwa utakuwa unawake taa na kuwapa nafasi wachezaji kuonesha umwamba. Namungo watakuwa wanapata uzoefu mwingine kucheza usiku.
TANZANIA PRISONS vs MBEYA KWANZA
Kama ilivyo mechi ya Mbeya City dhidi ya Mbeya Kwanza, ndivyo ulivyo ugumu wa pambano la Tanzania Prisons dhidi ya Mbeya Kwanza. Kwamba nani awe mbabe wa jiji la Mbeya? Hilo ndilo swali wanalotakiwa kujibu wachezaji na makocha ili kuwafurahisha wapenzi wao. Novemba 19 mwaka kila kitu kitajulikana, nani mbabe kati ya wazoefu Tanzania Prisons na wageni Mbeya Kwanza.
NAMUNGO vs YANGA
Saa kumi jioni ya Novemba 20 Yanga watakaribishwa katika dimba la Majaliwa mkoani Lindi. Mchezo utachezwa jioni hiyo badala ya usiku. Yanga watakuwa na nia ileile kuchukua pointi tatu muhimu mbele ya vijana wa Hemed Morocco. Je hili litawezekana vipi? Je wenyeji watakuwa hali gani? Bila shaka litakuwa pambano la kuvutia mno, kama ambavyo siku hiyo hiyo Mbeya City watakapowakaribisha Mtibwa Sugar katika dimba lao la Sokoine.
MBEYA CITY vs KMC
Itakapofika saa 12 na nusu jioni ya Novemba 27 ubao wa matokea utaonesha nani ameibuka mbabe kati ya timu hizi mbili. Wote ni ‘watumishi wa umma’ ambao watakuwa na kazi ya kuonesha nani anao uwezo zaidi kuliko mwingine. Mbeya City watakuwa na kibarua mbele ya timu ngumu hii kutoka Manispaa ya Kinondoni.
AZAM FC vs MTIBWA SUGAR
Mabwanyenye wa Chamazi watawakaribisha walima miwa wa Morogoro. Mtibwa Sugar. Azam FC watakuwa na kazi moja ya kuonesha kuwa ubora wao unalingana na jina lao pamoja na televisheni inayoonesha mechi za Ligi Kuu Tanzania.
MBEYA KWANZA vs YANGA
Ni nani hajui kuwa mechi hii itakuwa kivutio kikubwa si jijini Mbeya pekee? Kwa vyovyote vile wageni wa Ligi Kuu Mbeya Kwanza watakuwa na lengo la kuwaonesha ubabe Yanga, na kwamba wao wameingia Ligi hiyo kushindana sio kuwa wasindikizaji. Hapo ndipo tutashuhudia mvuto wa mechi hii ambapo Yanga watataka kuonesha umahiri na uzoefu wao kwenye ushindani. Ni saa kumi jioni ya Novemba 30 mwaka huu.
Simba VS GEITA GOLD
Kwa wageni Geita Gold watakuwa na kazi ya kuwaonesha Simba kuwa wamekuja kutetemesha vigogo wa Ligi Kuu. Ukizingatia Geita Gold wananolewa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije bila shaka watakuwa na mengi ya kuwaonesha Simba siku ya kwanza ya mwezi Desemba mwaka huu.
SIMBA vs YANGA
Ni saa 11 jioni ya Desemba 14 mwaka huu miamba ya soka Simba na Yanga watapepetana katika mechi za mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania. katika mchezo huo Simba watakuwa wenyeji huku Yanga wakiwa wageni nani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
MECHI NYINGINEZO
Kagera Sugar dhidi ya Simba itachezwa Kaitaba ifikapo Desemba 18 mwaka huu. Nao Azam FC watachuana na Mbeya City huku KMC wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar. Desemba 19 Yanga watakuwa wageni wa Tanzania Prisons saa kumi jioni.
Simba watapepetana na KMC jijini Dar es salaam ifikapo Desemba 24 yaani siku moja kabla ya noeli. Siku moja baada ya noeli Yanga watakuwa na kazi ya kuoneshana ubabe na Biashara United Kwa Mkapa jijini Dar es salaam. Kabla ya siku 7 baadaye katika uwanja huo huo watawakaribisha Dodoma Jiji saa moja usiku.
Comments
Loading…