in , , ,

MSHERY ATAPOTEA KAMA KABWILI?

Likitajwa jina la Jamal Malinzi kitu cha kwanza kinachokuja kichwani kwangu ni Serengeti boys ya mwaka 2017. Moja ya kikosi bora cha vijana ambacho nimewahi kukishuhudia kwenye maisha yangu ya mpira wa miguu hapa Tanzania.

Hii ndiyo Serengeti boys ilitoboa kufuzu michuano ya Afcon ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon mwaka 2017. Kikosi ambacho kilisheheni nyota wengi ambao tuliamini ni nyota ambao watakuja kuisaidia timu yetu ya taifa “Taifa Stars.

Taifa zima lilikuwa linalia kwa kutokuwa na mshambuliaji katili wa kati, lakini Bakari Shime alifanikiwa kutupa Yohana Oscar Mkomola kwenye kikosi chake cha Serengeti boys hii ya mwaka 2017. Yohana Oscar Mkomola kazi yake ilikuwa moja tu kufunga.

Kwake yeye alikuwa anafurahia kufunga kitu ambacho kilipelekea magoli yake kutupelekea sisi kushiriki Afcon ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 huko Gabon.

Unamkumbuka Ally Hamis Ng’azi ? Achana na huyo, unaukumbuka ufundi wa Shaban Zubery Ada  pale katikati ya uwanja? Wakati unajaribu kuwatafakari hao, kwenye tafakuri yako usimsahau Kelvin Nashon Naftali moja ya viungo bora sana.

Kikosi hiki cha Serengeti boys ya mwaka 2017 ndicho kikosi ambacho kilifanikiwa kutengeneza safu bora na imara ya ulinzi kwa sababu ilikuwa imesheheni mabeki wengi vipaji vikubwa sana.

Ndicho kikosi ambacho kilikuwa na Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Job na Ally Hussein Msengi. Huu ulikuwa ukuta wa “Berlin” yalihitajika maarifa makubwa sana kuupita ukuta huu.

Nyuma ya ukuta huu alikuwepo Ramadhani Kabwili. Kwa kipindi kile watu wengi waliamini huyu ndiye angekuja kuwa Juma Kaseja mpya. Umbo lake dogo  kwa wakati huo na uwezo wake wa kudaka ulifanya watu wengi waamini kuwa Ramadhani Kabwili ndiye atakuja kuwa Tanzania One kwa siku zijazo.

Leo hii ni mwaka 2024. Miaka saba imepita tangu Serengi boys hii ishiriki michuano hiyo ya Afcon ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon. Mpaka ninapoandika makala hii Ramadhani Kabwili hana timu ambayo anaichezea.

Ile ndoto ya Watanzania wengi kumuona Ramadhani Kabwili kama Tanzania One imeshafutika tayari. Ramadhani Kabwili hayuko tena kwenye soko la ushindani, kuna wakati mwingine ni sahihi kusema Ramadhani Kabwili amestaafu soka akiwa na miaka 24.

Wakati tunamfikiria Ramadhani Kabwili, tuendelee kumfikiria Abuutwalib Mshery huku tukiwa na tahadhali kubwa sana ya yeye kuwa kama Ramadhani Kabwili. Sitamani yatokee hayo hata siku moja lakini nafsi yangu ina wasiwasi sana.

Abuutwalib Mshery ni moja ya wachezaji ambao walitoa tumaini kubwa sana kwa Watanzania wengi sana kuwa ni moja ya magolikipa ambao watakuwa na msaada mkubwa sana kwenye timu yetu ya Taifa.

Huyu ndiye golikipa ambaye yuko Mtibwa Sugar alifanikiwa kupata nafasi ya kuwa golikipa namba moja wa Mtibwa Sugar mbele ya wakongwe kama Shabaan Kado na Said Nduda.

Pamoja na kufanikiwa kuwa golikipa namba moja wa Mtibwa Sugar, pia alifanikiwa kuwa nahodha wa klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 21 tu mbele ya wakongwe wengi ambao walikuwepo kwenye kikosi hicho.

Kuwa nahodha akiwa kwenye umri mdogo na kuwa golikipa namba moja mbele ya wakonge Shabaan Kado pamoja Said Nduda kilikuwa kitu kikubwa sana na Watanzania wengi walibaki kuwa na matumaini makubwa sana kwa Abuutwalib Mshery.

Leo hii yuko Yanga SC, sehemu ambayo kuna golikipa mkubwa wa kimataifa kutoka Mali , Diarra. Kwa kiwango cha Diarra inaonekana ni ngumu kwa Abuutwalib Mshery kupata nafasi ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu Yanga SC.

Swali kubwa linabaki. Golikipa wa kiwango cha Abuutwalib Mshery ataendelea kukaa benchi mpaka lini ? Yeye binafsi ameridhishwa na kukaa benchi ? Hajawahi kufikiria njia rahisi ya yeye kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kulinda kiwango chake ?

Naamini kama Taifa tunategemea mikono yake ambayo tulianza kuiamini tangu zamani. Ni muhimu kwa mikono yake kuendelea kulindwa kwa yeye angalau kutafuta timu ambayo ataweza kuchezea kwa mkopo ili kulinda kiwango chake kikubwa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

NATAMANI CHASAMBI AENDE AZAM FC

Jurgen Klopp

Jurgen  Klopp na ukocha wa makocha