Tanzania ilipelekwa kwenye kiwanja cha mbali sana kwa sababu Morocco wanayo machaguo mengi.
Ni kilometa nyingi sana kutoka jiji la Casablanca ndipo ilikochezwa mechi kati ya Timu ya Taifa ya Morocco na Tanzania hadi kwenye jiji lingine la Oudja katika mchezo wa Kundi E katika hatua ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026. Mashabiki wengi nyumbani Tanzania wangependa kuona vijana wa Taifa Stars waklipepetana na Morocco kwenye miji waliyozoea ya Rabat au Casablanca. Lakini hali ya mambo haikuwa hivi badala yake chama cha soka cha Morocco kimepelea mechi hiyo huko Oudja kwenye mji wenye baridi kali sana. kama tunavyojua barani Ulaya sasa hivi kuna hali ya hewa ya baridi, kwahiyo Morocco ni ukanda uleule kwa sababu inapakana na Hispania.
Hali ya hewa ya baadhi ya miji ya Morocco ni ya baridi sana na ndiyo hali waliyozoea wenyeji wengi katika nchi za Ulaya. Kama ungetaka kufananisha umbali wa uwanja uliozeleka na ule mgeni basi ungewaambia mashabiki na wadau wa mpira wa miguu Tanzania kuwa mechi haitachezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa badala yake inapelekwa kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza ama CCM Sokoine jijini Mbeya.
Viwanja hivi vingewasumbua wageni kwa umbali kisha kuwachosha zaidi kwa safari ndefu. Fikiria mechi iwe kati ya Tanzania na Misri kisha wanaambiwa mechi inachezwa kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya maana yake watalazimika kutua Dar Es salaam kisha kuanza safari nyingine kwenda uwanja wa ndege wa Songwe mkoani Songwe kisha warudi jijini Mbeya kwenye Dimba la Sokoine . kwa hakika hii ni safari ndefu ambayo tayari wapinzani wanakuwa wamechoshwa na unapowakuta uwanjani kiasi fulani nguvu zao zitapungua.
Kwa mazingira ya mechi iliyochezwa usiku wa kuamkia jumatano, Tanzania ilipelekwa kwenye kiwanja cha mbali sana kwa sababu Morocco wanayo machaguo mengi. Linapofika suala la uwanja wa kutumika Morocco wana kila sababu ya kuitangaza nchi yao kuwa wanavyo viwanja vizuri vya soka. Mfano si lazima ucheze Casablanca na Rabat, bali unapelekwa mji mwingine. Hii ni sawa na kusema si lazima upelekwe kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ama Uhuru jijini Dar Es salaam wakati unalo chaguo lingine la Sokoine, Jamhuri (Dodoma), CCM Kirumba (Mwanza) na kadhalika.
Je viwanja vya soka vina umuhimu gani?
Tanzania inasifika kuwa na mashabiki wengi wa soka. Baadhi ya wachambuzi kutoka nchi zingine wanatuambia huku Ulaya kwamba huenda nchi yetu inaabudu soka kama ilivyo Dini. Hali hiyo ni kama Brazil ambao wanaabudu soka kama vile Dini. Ukweli ni kwamba watanzania wanapenda sana mpira wa miguu na klabu zao, halafu wanapenda soka la Ulaya na nsehemu zingine kama chaguo la pili.
Hii maana yake ni kwamba suala la uwekezaji wa viwanja kwenye vya michezo ni muhimu zaidi kuliko kukalia michoro yetu ya ujenzi kwenye makabati huku hali halisi ikiwa tofauti. Kwenye sekta ya michezo namaanisha kila mchezo unatumika kama nyenzo ya kujitangaza duniani. Kila nchi inaweza kusifika kwa mchezo fulani, na hivyo unegeuka kuwa utalii.
Watalii mbalimbali wanaotembelea nchini wanategemea kupata burudani zingine ndogo kama michezo ya soka ili kustareheshwa zaidi. Kwa maana hiyo kwenye suala la viwanja wenzetu Morocco wametushinda katika machaguo yao. Tanzania chaguo la kwanza ni uwanja wa Benjamin Mkapa.
Chaguo la pili ni New Amaan Complex visiwani Zanzibar. Baada ya hapo hatuna chaguo lingine zaidi ya Uhuru Jijini Dar Es Salaam hata kama unatazamwa kama uwanja wa shughuli zingine za kijeshi lakini tunapaswa kubadilika, shughuli ni uchumi, gwaride ni usalama lakini lazima liendane na uchumi. Tunakzuaje uchumi wa nchi kupitia sekta ya michezo? Ndilo swali ambalo natamani kuona kila mtanzania akiwa anatafuta majibu.
Majiji yetu bila viwanja vikubwa ni aibu
Lazima tukiri na kuona aibu kidogo, kwenye Miji yetu mikubwa haina viwanja vyenye hadhi ya mashindano ya CAF. Si kwa sababu hatuna fedha, bali dhamira hafifu ya kukamilisha jambo hilo. Kwa mfano, Majiji kama Tanga, Mbeya, Mwanza na Arusha yalipaswa kuwa na viwanja vyenye hadhi ya Kimataifa na serikali inawajibika kutekeleza jambo hili.
Comments
Loading…