Moja ya watu ambao naamini kupitia ushindani mimi ni mmoja wao. Naamini uimara hutengenezwa kupitia ushindani. Ndiyo maana kwa soka la sasa ni kitu cha kawaida tu kumkuta kocha wa timu fulani akifanya usajili wa wachezaji wanaokaribiana uwezo tena wakiwa wanacheza eneo moja.
Ndiyo maana Pep Guardiola alimleta Riyad Mahrez kipindi ambacho Sane, Raheem Sterling na Bernardo Silva wapo. Wote ni wachezaji wa kiwango cha juu na wanacheza maeneo ambayo wanafanana ndani ya uwanja lakini Pep Guardiola hakuliona hili.
Yeye alitazama namna ya kuimarisha kikosi chake, namna ya kuwa na kikosi imara kuanzia uwanjani mpaka kwenye benchi. Kitu ambacho kingempa nafasi kubwa ya kutokuwa na wasiwasi kipindi ambacho timu imebanwa na inahitaji njia mbadala ya kupata matokeo.
Wachezaji ambao wapo kwenye benchi ni rahisi kuleta njia mbadala kwa sababu wana kiwango kikubwa kama wachezaji ambao wako ndani ya uwanja. Achana na kocha kuwa na njia mbadala kipindi ambacho timu inapitia wakati mgumu.
Kuwa na wachezaji ambao hawapishani sana viwango kuna saidia sana kumfanya mchezaji asibweteke kwa sababu akili yake itakuwa makini na ataongeza juhudi za kupigana kwa kuhofia kuwa kipindia ambacho atazembea nafasi yake inaweza kuchukuliwa na mchezaji ambaye yuko benchi mwenye kiwango kinachokaribiana na chake.
Hapa ndiyo ulikuwa mwanzo wa mimi kuunga mkono uamuzi wa Gadiel Michael na Beno Kalolanya kwenda Simba. Kwanza Simba walikuwa wanatengeneza kikosi kipana, kikosi ambacho kina wachezaji wanaokaribiana viwango kwenye kila eneo la uwanja.
Upana huu wa kikosi ungeipa nafasi kubwa Simba kuwa na njia mbadala kipindi ambacho timu inapopitia wakati mgumu kwenye mechi husika , ni rahisi kumwamsha mchezaji kutoka kwenye benchi akiingia uwanjani na akafanikiwa kuleta mabadiliko ambayo yanainufaisha timu.
Nilikubaliana na uamuzi wa Gadiel Michael pamoja na Beno Kakolanya kwenda Simba kwa sababu Mohamed Hussein “Tshabalala” pamoja na Aishi Manula walihitaji changamoto mpya ili kuondokana na kubweteka kwao katika kikosi cha Simba.
Kuna kipindi mashabiki wengi walikuwa wanalalamika kuhusiana na Aishi Manula kufungwa magoli ya kizembe. Inawezekana kipindi hiki alikuwa amebweteka kwa kuona kuwa hakuna golikipa ambaye angempa changamoto katika kikosi cha Simba.
Inawezekana alikuwa amechukulia hiki kitu cha kutokuwa na golikipa mwenye kiwango kinacho karibiana na chake katika hali ya kubweteka ndiyo maana watu wengi waliona ameshuka kiwango na akawa anaruhusu kufungwa magoli ambayo ni mepesi.
Ujio wa Beno Kakolanya niliutazama kwenye eneo hili, Aishi Manula alihitaji mtu ambaye angempa changamoto, mtu ambaye angemwambia kwa vitendo kuwa hatakiwi kulala Ila unatakiwa upigane usiku na mchana kwa ajili ya kufanya vizuri.
Beno Kakolanya kafanya kazi yake vyema sana mpaka sasa hivi, moja amekuja kuongeza upana wa kikosi cha Simba. Pili kahahakisha anampa changamoto Aishi Manula lakini kwa bahati mbaya wakati anamwamsha Aishi Manula, alitumia mikono yake na Beno Kakolanya kumlaza usingizini na kumficha.
Comments
Loading…