Filimbi ya mwisho ilipopulizwa kumaliza mchezo kati ya Arsenal na Manchester City hali ilikuwa mbaya upande wa kikosi cha Mikel Arteta. Takwimu zinaonesha kuwa Mikel Arteta amepambana mara nne na Pep Guardiola wakiwa makocha wa timu pinzani, ilionekana wote walikuwa na hisia za mshangao wa mchezo wenyewe hadi kufikia dakika ya 90.
Kama zilivyokuwa mechi zao tatu walizokutana, dhidi ya Burnley, Southampton na Everton, kikosi cha Arsenal kinaonekana kufurahia zaidi kinapopambana na Manchester City ya Pep Guardiola, lakini kikapoteza mchezo wenyewe.
Uchambuzi wa Tanzaniasports unaonesha kuwa kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la Carabao, kulikuwa na sifa nzuri za Mikel Arteta linapofika suala la mashindano ya mtoano. Tukirudi nyuma alipata ushindi wa mabao 4-1, katika mechi za mtoano alitolewa mara moja na timu ya Olympiakos mwaka mmoja uliopita kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Ulaya hatua ya 32.
Arsenal wana mwenendo uleule kwenye mechi za mtoano kama waliyocheza na Man City, iwe kwenye mashindano ya FA, Carabao au Europa League, kikosi chao kimekuwa na mchanganyiko wa chipukizi na wakongwe. Arteta anaonekana kuwapumzisha baadhi ya mastaa na kuwapa nafasi chipukizi wenye ubora kupigania hadhi ya timu hiyo.
Bernd Leno kuanza kikosi cha kwanza cha mechi za Ligi Kuu England ni jambo la kawaida kila anapokuwa imara kiafya na kuendelea kupangwa kwenye mashindano mengine ya Carabao na Europa League, ni mchezaji anayeipa faida Arsenal hasa tukikumbuka wakati wa hatua ya matuta kwenye uwanja wa Anfield ambako vijana wa Arteta walifanikiwa kutinga hatua ya nane bora.
Uamuzi wa kumweka benchi uliigharimu Arsenal ilipocheza dhidi ya Man City baada ya kumpanga golikipa wao Alex Runarsson. Makosa ya udakaji ya Runar yaliipa Man City kupata bao, jambo ambalo limetupiwa amcho ili kuona uwezo na ubora wake kama unafaa kuendelea kuichezea Arsenal. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 aliupromosha mchezo huo kwa kosa ambalo liliigharimu timu yake.
Tanzaniasports kwenye tathmini yake inaonesha kuwa kushindwa kumudu pasi,kutuliza mipira kulimlazimu kufanya makosa mara kwa mara kulifuta umahiri wake wa kupangua michomo ya washambuliaji wa Man City. Kuna wakati alifanya matukio ya kushangaza kwa kuondoa michomo mikali iliyoelekezwa langoni mwa Arsenal na kuipa uhai timu hiyo. Lakini makosa yaliyosababisha mabao likiwe lingine la tatu yaliharibu sifa ambazo angeibuka nazo siku ya mchezo huo.
Tofauti na kurejea kwa Gabriel Martinelli na machachari yake ya muda mfupi yaliyoibua matumaini kwa Arsenal, bado hayakuokoa timu hiyo kutoka kwenye kipigo. Martinelli alirejea uwanjani katika mchezo wa Kombe la Papa Yohane akiwa na kikosi cha chini ya miaka 21 cha Arsenal kilichopambana na Wimbledon, alionesha umakini na ufundi wa hali juu siku hiyo.
Kwahiyo ukawa mchezo ambao ulimpatia nafasi ya kurejeshwa kikosi cha kwanza msimu huu, wakati nahodha Alexandre Lacazette angeonekana anatupa mikono hewani kila Man City walipokuwa wanamiliki mpira. Hata hivyo kwa Martinelli alirudi nyuma kutafuta mipira hali ambayo iliipa uhai Arsenal na kumfanya beki wa Man City Zack Steffen kuwa na wakati mgumu kumdhibiti.
Martinelli ana uwezo wa kumiliki mpira na hana hofu yoyote anapokabiliana na mabeki wa timu pinzani, hilo ndilo linalotakiwa kutoka kwa mchezaji chipukizi. Kingine, alionesha uwezo wa kuipangua ngome ya Man City kwa chenga na kasi ndani ya boksi na kupiga mashuti kwa kutumia mguu wa kulia. Kila alipokosa kufunga kwenye majaribio yake alisikitishwa mno.
Baadaye alichagua kushambulia kutokea pembeni na kuingia ndani kwa kasi na chenga za maudhi upande wa kushoto kisha kupiga krosi kwa Lacazette aliyeandika bao la kusawazisha kuwa 1-1.
Bahati mbaya kwa Martinelli, mbinu zake za kushambuliaji ambazo ziliifanya Arsenal iwe hatari langoni mwa Man City ndizo zilizochangia kumwondoa kwenye mchezo mapema sana. Kukimbiza ndoto iliyopotea ni tabia ya kikosi cha Arteta. Hatua ya Martinelli kugongana na beki Zack Steffen dakika tano kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza ilisababisha atolewa nje. Ingawa yapo matumaini kuwa atapona haraka na kurudi uwanjani upo ushahidi kuwa Martinelli anaibua matumaini makubwa ndani ya kikosi cha Arsernal huku kocha wake Mikel Arteta akitambua hilo na kulizungumzia baada ya kumalizika mchezo huo.
“Lilikuwa tukio baya kwa Martinelli, aligongwa nyuma ya ugoko na kushindwa kuendelea na mchezo. Kipindi cha kwanza chote alikuwa nguzo ya Arsenal, alishambulia vizuri. Alisema yuko vizuri kiafya, hakuwa na tatizo hivyo alitaka kuendelea kucheza, lakini alipokuwa uwanjani hakuweza kucheza vizuri tena kama alivyoanza mwanzoni. Tulitakiwa kuchukua uamuzi wa kumtoa uwanjani ili kumlinda asipate madhara zaidi.” alisema Mikel Arteta.
Martinelli alirejea kama mwokozi wa Arsenal na kuonesha namna chipukizi wa timu hiyo wanavyoweza kuleta chachu ya ushindi dhidi ya timu pinzani katika mashindano yote msimu huu.
Katika mechi za EPL kazi aliyofanya Martinelli kwenye mchezo wao dhidi ya Man City huwa inafanywa na Bukayo Saka, lakini Joe Willock na Reiss Nelson wamekuwa wakifanya hivyo kwenye mashindano ya Europa League. Wachezaji hao wote wamekosolewa mara kadhaa juu ya viwango vyao kuwa chini kwenye mashindano. Hata hivyo Emile Smith Rowe katika mchezo dhidi ya Man City ni wazi Mikel Arteta ana chipukizi mwingine mwenye uwezo wa kuingia kikosi cha kwanza EPL.
Ndani ya dakika chache tu alipochukua nafasi ya kiungo mkabajai Mohamed Elneny wakati ubao wa matokeo ukionesha 3-1, kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 aliwashangaza wengi kwa namna alivyoweza kufuata pasi ya Nicolas Pepe. Ingawa hakupata pasi hiyo lakini aliwafanya benchi la ufundi waone vitu vyake ili waamue namna ya kumtumia ikiwemo mechi za EPL kuliko Carabao. Baadaye alifanya vitu vingine adimu katika eneo la penati la Man City baada ya kuteleza kufukuzia pasi ya Lacazette ili aweza kupifa shuti langoni mwa City,
Uchezaji wa Smith Rowe nao ulikuwa kivutio. Mbali ya hilo, baada ya kuingia uwanjani alifanya vitu adimu katika eneo la beki wa kulia na kati kabla ya kumwona Sead Kolasinac kumwachia kiokoa hatari langoni.
Uwezo wake wa kupokea na kutoa pasi, muono alionao katika mchezo, ufundi na kusoma mchezo ni vitu ambavyo alivionesha kwa muda mfupi na kuifanya Arsenal kubeba matumaini siku za usoni. Rowe ni mchezaji wa kitimu, jinsi alivyopataa na Dani Ceballos, Willock na Balogun lilikuwa jambo la kusisimua kutoka kwa kinda huyo.
Martinelli ameonesha namna gani Arteta anaweza kuwaamini chipukizi walioko kikosini mwake kucheza mechi za EPL. Makinda wengi wanacheza namna ambayo inatoa majibu kuwa wao ni kama lugha iliyosahaulika, lakini Martinelli na Smith Rowe wameamua kuipa umuhimu na kumkumbusha kocha wao ana vipaji vyenye kuweza kumpa matokeo ambavyo hajavitumia ipasavyo.
Baada ya kuwapanga chipukizi hao na wakongwe kwenye mashindano ya Europa League, EPL na Carabao, umefika wakati sasa Arteta kuwaamini na kuwakabidhi majukumu mazito kikosini ili wamletee matokeo mazuri licha ya umri wao kuwa mdogo.
Tukizingatia kuwa mashindano ya FA yapo mzunguko wa tatu, huku mtoano Europa unakaribia kuanza, ni wazi sera ya kupanga kikosi mchanganyiko inatakiwa kupunguzwa kwa sababu chipukizi wameonesha wanaweza kubeba majukumu wao wenyewe bila wakongwe.
Kadiri umri wao unavyoongezeka na mahitaki yao yanazidi kuwa makubwa. Ni vigumu kuendelea kuwakalisha jukwaani huku wakiwa na uwezo wa kubadili matokeo yao mabaya na kuwa mazuri. Pia inaweza kuchangia kuvutiwa kwenda timu zingine ambazo zitawahakikishia nafasi ya kucheza mechi nyingi .
Kama wanavyaominiwa wachezaji wakongwe klabuni hapo Leno na Pierre-Emerick Aubameyang (bila kujali bao alilojifunga dhidi ya Southampton) inawezekana imani hiyo ikaenda kwa chipukizi wengine kama Gabriel, Saka, Martinelli na Smith Rowe. Muda umewadia kwa sasa chipukizi kupewa nafasi walete furaha Arsenal kabla jua halijawachwea
Comments
Loading…