in , ,

MICHUANO YA KOMBE LA LIGI:

 

*Arsenal, Chelsea Man United safi

*Liverpool waponea tundu la sindano

*Spurs, Newcastle, West Brom nje

 

Awamu ya tatu ya mechi za Kombe la Ligi – Capital One Cup – imemalizika kwa klabu kubwa za Arsenal, Chelsea, Manchester United na Liverpool kuvuka, japokuwa ilibidi Liver waende hadi muda wa ziada na penati kuwashinda klabu ya Daraja la Pili ya Carlisle.

Arsenal waliotoka kupoteza mechi mbili – dhidi ya Chelsea kwenye Ligi Kuu ya England na dhidi ya Dinamo Zagreb kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, walifanikiwa kuwazima mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur kwa mabao 2-1.

Alikuwa kiungo mkabaji kutoka Ufaransa, Mathieu Flamini ambaye amekuwa akipigiwa simulizi za kuondoka Emirates aliyewatupa Spurs nje ya michuano hiyo kwa mabao mawili mazuri.

Akicheza kwa mara ya kwanza msimu huu, mahali pa kiungo mkabaji anayeaminiwa zaidi, Francis Coquelin, Flamini alifunga bao la kwanza baada ya kipa Michael Vorm kuutema mpira wa Alex Oxlade-Chamberlain na kuwainua washabiki wa Arsenal waliokuwa na kiu ya ushindi.

Hata hivyo, beki wa pembeni wa Arsenal, Calum Chambers alijifunga baadaya kubebeshwa majalo ya Nacer Chadli. Flamini alionesha umahiri wake tena kwa kuwapaisha Arsenal alipofunga kwa shuti kiufundi akiwa umbali wa yadi 20. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Flamini kuwafungia Arsenal mabao mawili kwenye mechi moja.

“Nafurahi kwa ajili ya timu na binafsi kadhalika. Nimesikia mengi kwenye vyombo vya habari lakini bado nipo hapa. Sina tatizo na yeyote kwenye klabu. Haiwezi kuwa rahisi pale unaposhindwa kucheza kila mechi, hivyo nilikuwa na kazi ya kufanya kuonesha naweza,” akasema Flamini aliyejawa furaha.

Mshambuliaji chipukizi aliyewika msimu uliopita kwa Spurs, Harry Kane alionekana kushindwa kurejelea njia zake, ambapo mpaka sasa hajaweza kufunga bao lolote kwa klabu. Jumatano hii alipata nafasi nzuri ya kufunga akiwa umbali wa yadi nane tu, lakini badala ya kuachia mkwaju, akazidi kuremba na kupoteza nafasi hiyo.
CHELSEA WATOA KIPIGO CHA 4-1

Ramires, akifunga bao la kwanza kwa Chelsea
Ramires, akifunga bao la kwanza kwa Chelsea

Chelsea walivuka vyema kuingia hatua ya nne baada ya kuwafunga Walsall 4-1. Chelsea walipata mabao yao kupitia kwa Ramires aliyefunga baada ya kupata pasi kutoka kwa mchezaji mpya, Robert Kenedy Nunes do Nascimento, maarufu zaidi kwa jina la Kenedy.

Mfaransa Loic Remy alifunga bao la pili na Walsall wakajibu mapigo pale James O’Connor alipocheka na nyavu kutokana na mpira wa adhabu ndogo wa Milan Lalkovic. Chelsea walipata bao la tatu kupitia kwa Kenedy, aliyevunja matumaini ya klabu hiyo ya Ligi Daraja la Kwanza.

Walsall walicheza kiushindani hasa lakini dakika ya 90 walilia tena baada ya Pedro kufunga kitabu cha mabao kwa Chelsea. Kenedy alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza na alivuta washabiki wengi kwa ufundi wake dimbani.

MANCHESTER UNITED MAMBO YAO SAFI

Wayne Rooney akiupitisha mpira katikati ya miguu ya golikipa, kufungua kitabu cha magoli kwa united
Wayne Rooney akiupitisha mpira katikati ya miguu ya golikipa, kufungua kitabu cha magoli kwa united

Manchester United waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwafunga Ipswich 3-0 wakicheza Old Trafford, ambapo nahodha wao, Wayne Rooney alipata bao la kwanza nyumbani msimu huu.

Anthony Martial, 19, aliyesajiliwa siku ya mwisho wa msimu kutoka Monaco kwa pauni milioni 36, aliendelea kucheka na nyavu kwa kufunga bao moja, huku jingine likifungwa na Andreas Pereira, 19, naye akifunga bao zuri kwa mpira wa adhabu ndogo, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kwa klabu hiyo.

LIVERPOOL WAHENYESHWA, LAKINI WAPENYA

live

Liverpool wamefanikiwa kuvuka hatua hii kwa mbinde, baada ya kupelekeshwa hadi muda wa ziada na penati na timu ndogo ya Carlisle, tena wakicheza nyumbani Anfield. Washabiki wa Liver walianza kuwazomea wachezaji pale dakika 90 za kawaida zilipokamilika, wakiongeza shinikizo dhidi ya kocha Brendan Rodgers.

Liver wameanza vibaya Ligi Kuu na walihitaji ushindi kwenye mechi ya jana, ili kufufua matumaini ya kusonga mbele vyema na kuwa vizuri kisaikolojia. Ndio walioanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wao mpya, Danny Ings aliyeungisha kwa kichwa wavuni majalo ya Adam Lallana.

Liverpool walivurugwa pale Derek Asamoah alipopiga mpira wa kima cha nyoka na kusawazisha, na tangu hapo Reds wakahangaika kupata bao la ushindi lakini ikashindikana. Kwenye penati, shujaa alikuwa kipa mpya wa Liverpool, Adam Bogdan, aliyeokoa penati tatu na kuwavusha.

Penati za Liverpool zilifungwa na James Milner, Emre Can na Ings wakati Lalana na Philippe Coutinho walikosa kwa kipa wa Carlisle, Mark Gillespie kuokoa.
MATOKEO MENGINE CAPITAL ONE CUP

 Lewis McGugan akishangilia bao lake aliyoifungia Sheffield Wednesday
Lewis McGugan akishangilia bao lake aliyoifungia Sheffield Wednesday

Katika mechi nyingine, Crystal Palace waliwakung’uta Charlton 4-1, MK Dons wakalala 0-6 walipowakaribisha Southampton wakati Newcastle waliendelea na mazongezonge yaokwa kufungwa 1-0 na Sheffield Wednesday.

Norwich wakiwa nyumbani waliwatoa nje ya mashindano West Bromwich Albion kwa mabao 3-0.

Ratiba ya mzunguko wa nne utakaochezwa Oktiba 27 na 28,  inaonesha kwamba Manchester City watachuana na Palace, Liverpool na Bournemouth, Manchester United na Middlesbrough wakati Everton watakwaana na Norwich.

Southampton watawakaribisha Aston Villa, Sheffield Wednesday watakuwa wageni wa Arsenal, Hull wakipepetana na Leicester wakati Stoke watawakaribisha Chelsea.

Matokeo mengine ya mechi za jana.
Matokeo mengine ya mechi za jana.

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Carneiro aondoka Chelsea

Tanzania Sports

Waingereza wanavyojenga soka ya Ufaransa