*Kijana aliyekulia Mbagala*
Huyu ni mchezaji maarufu sana wa Tanzania kwa miaka takribani miaka 10 sasa kutokana na uwezo wake wa kusakata soka. Samatta alizaliwa Desemba 23, 1992. Samatta ni miongoni mwa vijana waliokulia eneo la Mbagala lililopo jijini Dar es salaam .
USAJILI:
Alianza kucheza soka katika timu ya Kimbangulile ambayo inasifika kwa kulea vijana maeneo ya Temeke. Kimbangulile ni kama akademi ya wachezaji mbalimbali wenye vipaji. Baadaye alijiunga na klabu ya Mbagala Market ambayo ilikuwa ikipigania kupanda daraja hadi Ligi Kuu. Ni Mbagala Market ndiyo ilikitambulisha zaidi kipaji cha nyota huyo. Mwaka 2008 wakati Mbagala Market ikipanda Ligi ndipo mfanyabiashara mashuhuri Mohammed Dewji akainunua na kubadilisha jina ikaitwa African Lyon alikodumu hadi 2010. Akiwa klabu hiyo ndipo Simba walifanikiwa kumwona na kumsajili mwaka 2010. Hata hivyo Mbwana Samatta aligoma kujiunga na Simba bila kutekelezewa ahadi ya kununuliwa gari kwa mujibu wa mkataba. Simba walisubiri kwa muda wa miezi 6 lakini Samatta aligoma kabisa kuichezea klabu hiyo. Ndiyo baadaye alikubali kuichezea Simba baada ya kutimiziwa hadi yake.
REKODI:
- Ni mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya mchezaji bora afrika (Ligi za ndani). Tuzo hiyo ni kutokana na mafanikio aliyopata akiwa na klabu ya TP Mazembe ambayo ni mabingwa Afrika mwaka 2015.
*Samatta ni mtanzania wa kwanza kuwa mfungaji bora wa Ligi ya mabingwa Afrika.
*Samatta na Thomas Ulimwengu ni watanzania wa kwanza kucheza mechi za fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.
*Samatta ni mtanzania wa kwanza kufunga mabao katika michezo miwili ya fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika. Alifunga bao katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika nchini Algeria. Akafunga bao jingine katika mchezo wa marudiano wa fainali uliochezwa nchini DRC.
*Samatta na Ulimwengu ni watanzania wa kwanza kucheza kwenye mashindano ya klabu bingwa ya dunia. Walishiriki mashindano hayo mwezi Desemba mwaka jana nchini Japan ambapo bingwa ni Barcelona ya Hispania.
*Samatta ni mtanzania wa tatu kuteuliwa kwenye kikosi bora cha mwaka Afrika. Awali watanzania wengine waliowahi kuteuliwa katika kikosi bora cha mwaka ni Maulid Dilunga na Omari Mahadhi.
*Samatta ni mtanzania wa kwanza kusajiliwa na klabu ya Genk ya Ubeligiji. Pia atakuwa mtanzania wa kwanza kucheza Ligi kuu ya Ubelgiji.
*Samatta ni mchezaji wa pili wa TP Mazembe kutwaa tuzo ya mchezaji bora Afrika baada ya Tresor Mputu kutwaa tuzo hiyo mwaka 2009.
*Samatta ni mchezaji wa kwanza Afrika mashariki kutwaa tuzo ya mchezaji bora afrika.
ANAKOELEKEA:
Samatta amefichua kuwa ana kiu kubwa ya kuja kucheza Ligi Kuu Hispania (La Liga). Anasema Ligi hiyo imejaa vipaji na ufundi kuliko zingine. Hata hivyo hajasema ni klabu ipi anayopenda kuicheza huko Hispania. Kiufundi Samatta ni mchezaji mzuri mno kucheza namba 10, 11 au 7 (kama kiungo wa pembeni). Nafasi za kiungo wa pembeni zitampa mafanikio makubwa zaidi ya namba 9 aliyocheza kwenye mashindano ya klabu bingwa Afrika. Anafaa kwenye 4-3-3/5-3-2/4-4-2.
SERIKALI IFANYE NINI:
Rekodi inamtaja kama mchezaji wa kwanza. Lakini nini serikali inaweza kukifanya kuwapata akina Mbwana Samatta wengine
1.Kuboresha viwanja vya soka. Viwanja vingi vinamilikiwa na chama cha mapinduzi (CCM) haviko katika hali nzuri. Hivyo ili kupata wachezaji wazuri ni lazima hali ya viwanja ibadilike.
2.Elimu ya michezo inatakiwa kuendana na kuvumbua vipaji vinavyotakiwa kucheza soka moja kwa moja toka shuleni na kuendeleza vipaji. Vinahitajika vituo vya soka vyenye viwango kama cha Jakaya Kikwete Academy kilichopo Kidongo chekundu, jijini Dar es salaam. Elimu ya michezo ni pamoja na kuvifanya vyuo vya michezo kuwa sehemu ya kuvumbua na kuuza wachezaji kama inavyofanya klabu ya Azam fc ambayo kila mwaka husajili watoto chini ya miaka 15.
3.Serikali lazima ikubali kuboresha bajeti ya wizara ya habari, michezo na utamaduni. Mara nyingi wizara hii haina bajeti ya kujitosheleza. Pia ihakikishe maofisa michezo/utamaduni wa wilaya/mikoa wanakuwa sehemu ya kuvumbua vipaji vya soka. Kwamba serikali inaweza kuwa na Academy zake kila kanda ili kutengeneza vipaji vitakavyolinufaisha taifa kwa kuwauza kwenye klabu mbalimbali, kwani michezo ni sehemu ya ajira.
4.Makocha wenye viwango wanahitajika zaidi kwenye Academy kwani huko ndipo wanaanza kunolewa zaidi kisoka hivyo hakuhitaji watu wenye uwezo hafifu.