Michezo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imeanza kuchezwa hapo jana. Mechi nane za makundi manne zilichezwa hapo jana Jumanne na yalifungwa jumla ya mabao 20. Haya hapa ni matokeo ya michezo hiyo nane ya hapo jana.
WAWAKILISHI WA ENGLAND WACHEMSHA
Manchester United na Manchester City ambao walikuwa wakiiwakilisha England hapo jana wote walikutana na vipigo. Manchester United walifungwa 2-1 wakiwa ugenini dhidi ya PSV Eindhoven kwenye mchezo wa Kundi B. United ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa Memphis Depay.
Depay aliwahadaa walinzi wa timu yake ya zamani na kuifungia Manchster United bao zuri kwenye dakika ya 41. Hata hivyo bao hilo halikuweza kudumu hata kwa dakika chache. Hector Moreno alisawazisha kwa kichwa kutoka kwenye kona iliyopigwa na Maxime Lestienne.
Kipindi cha kwanza kilimalizika matokeo yakiwa 1-1. Kwenye dakika ya 57 Lestienne ambaye ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo akampigia krosi Luciano Narsingh ambaye pia alifunga kwa kichwa na kuwazamisha Mashetani Wekundu. Kwenye mchezo mwingine wa kundi hili Wolsfsburg wakiwa nyumbani waliwafunga CSKA Moscow 1-0.
Manchester City na wao walikutana na makali ya mabingwa wa Italia kwenye mchezo wa Kundi D. Wao pia walitangulia kupata bao kama jirani zao lakini Juventus walichomoa na kuwaongeza lingine na matokeo yakaisha 2-1. Giorgio Chiellini ndiye aliyewapatia bao Manchester City baada ya kujifunga kwenye dakika ya 57.
Bao la kusawazisha kwa upande wa Juventus lilifungwa na Mario Mandzukic akimalizia pasi kali kutoka kwa Paul Pogba iliyosafiri umbali wa takribani mita 35 huku bao la ushindi likifungwa na Alvaro Morata.
TIMU ZA HISPANIA ZADHIHIRISHA UBORA WA LA LIGA
Timu zote tatu kutoka Hispania zilizokuwa viwanjani zilishinda michezo yake kwa kishindo hapo jana huku kukiwa hakuna iliyoruhusu bao lolote kati ya timu hizo. Real Madrid ilishinda nyumbani 4-0 kwenye mchezo wake wa Kundi A dhidi ya Shakhtar Donetsk.
Karim Benzema alikuwa wa kwanza kufunga kisha Cristiano Ronaldo akafuata kwa kupiga hat-trick. Mchezo mwingine kwenye kundi hili uliwashuhudia PSG wakiwafunga Malmoe FF 2-0 kupitia Angel di Maria na Edinson Cavani.
Atletico Madrid wakiwa ugenini nao walishinda mchezo wao wa Kundi C kwa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Galatasaray. Alikuwa ni mshambuliaji hatari Antonie Griezman aliyefunga mabao yote mawili. Benifica nao waliwatandika FC Astana mabao mawili bila majibu kwenye kundi hili.
Sevilla wao walikuwa nyumbani wakiwakaribisha Borussia Moenchengladbach. Mabingwa hao wa Ligi ya Europa waliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri kwenye mchezo huo wa Kundi D ambalo wamo pia Manchester City na Juventus.