Baada ya kipigo kingine kutoka kwa Aston Villa cha mabao 2-1 ni dhahiri sasa Pep Guardiola anatakiwa kuwafukuza mastaa wake kikosini. Hapo alipo sasa ni pagumu, kwa sababu inakuwa mechi ya 9 kufungwa kati ya michezo 12 alizocheza. Katika michezo 12 ameshinda mchezo mmoja na kutoka sare miwili. Kwa matokeo ya jana dhidi ya Aston Villa ni dhahiri kwamba kocha wa Man City anatakiwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuwafukuza kati ya nyota watano hadi sita wa kikosi chake cha kwanza.
TANZANIA SPORTS inakuletea sababu za msingi za kufanyiwa mabadiliko ya kikosi hicho na hali ya hofu aliyonayo Pep Guardiola kutokana na kushindwa kufanya uamuzi kwenye kikosi chake.
Kuingiza damu changa za vijana
Kikosi cha Man City cha sasa kina nyota wengi walishinda mataji mbalimbali. Wachezaji walioshinda kuanzia EPL, Carabao hadi Ligi ya Mabingwa wamefika wakati wameishiwa makali na pumzi hivyo wanahitaji sura mpya ili kuendeleza mafanikio. Kuwa na kundi la wachezaji walioshinda mataji miaka saba mfululizo ni wazi wanahitaji kubadilisha kikosi hicho kwa kuingiza damu changa. Kila ukiangalia kikosi cha kwanza cha Man City utaona hakina mabadiliko yoyote, yaani kila siku ni kilekile.
Matokeo yake kila mchezo wamekuwa wakibanduliwa mabao na kupoyeza pointi. Kama mwenendo utazidi kua huu ni wazi Man City hawatakuwa kwneye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwahiyo maingizo ya vijana kama Savinho, Doku, James McAtee na Ricco Lewis na wengineo ni jambo muhimu sana kwa maslahi ya timu hiyo.
Ari hafifu, hawana njaa ya ushindi
Kwenye mchezo wao dhidi ya Aston Villa wachezaji wa Man City hawakuonekana kuwa na ari ya mchezo. Ni wachezaji wenye uzoefu mkubwa kwenye kusaka matokeo kwa ajili ya timu yao na wanaelewa umuhimu wa kutwaa makombe, lakini katika mchezo huo na Aston Villa hawakufikia hata robo ya sifa wanazotakiwa kuwa nazo. Timu ilionekana kuyumba, hakukuwa na ushirikiano wala kucheza kitimu.
Safu ya ushambuliaji ilikuwa na watu watano lakini bado hakukuwa na mbinu nyingi za kufanikisha hilo. Hawakuwa na mpishano ambao ungewapa mbinu za kupachika mabao. Ukizungumzia umiliki wa mpira walionekana kuwa wazuri sana, tatizo linakuja pale wanapopoteza mpira. Bila mpira miguuni wachezaji wa Man City walionekana kuwa mbali katika ubora wao na wala hawakuwa na juhudi za kusaka mpira zaidi kama ilivyozoeleka.
Umri unabisha hodi
Kwenye dirisha la usajili lililopita jambo moja la kushangaza lilifanywa na Pep Guardiola pamoja na menejimenti ya klabu kumrudisha Ilkay Gundogan kikosini kutoka Barcelona. Katika hali ya kujenga timu, alihitajika mchezaji ambaye ataongeza changamoto ya kupigania namba sio kujaza nafasi. Ilkay si kiungo mbaya lakini Man City ilihitaji mchezaji mwenye kuongeza kitu fulani kwa ajili ya kuokoa msimu wao.
Walijisahau kiasi kwamba umri wa wachezaji haukuwa ukiangaliwa kama ilivyokuwa kwa Ilkay Gundogan. Kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa, Bernado Silva na Gundogan hawakuwa kwenye kiwango cha kupangwa kikosi cha kwanza. Jitihada pekee amabzo zilionekana kwa Man City zilitoka kwa mawinga Jeremy Doku na Savinho, ambao uchezaji wao kila mara wanajaribu kutengeneza nafasi za kufunga au kusababisha madhara kwa timu pinzani. Mwelekeo wao kimbinu unapangua safu nyingi za ulinzi za timu pinzani lakini nyuma yao kuna mizigo mingi ambayo Pep Guardiola anatakiwa kuiondoa.
Kuzidiwa maarifa na kasi
Kasi ya wachezaji wa Man City imeshuka mno. Katika dirisha la usajili uliopita Aston Villa walimsajili Amada Onana kutoka Everton na Rogers kutoka Middlesbrough. Wachezaji hawa wawili wameifanya ngome ya kiungo ya klabu yao kuwa imara zaidi. Katika uimara huo wanacheza kwa nguvu na kasi muda mwingi wa mchezo hasa wanapokutana na timu kubwa kama Man City.
Kuna wakati unaona Man City walishindwa kukabiliana na kasi na nguvu za Aston Villa na kuifanya timu hiyo iwe imara eneo hilo na kuwashinda nguvu Man City. Uchezaji wa pasi za haraka na kasi uliokuwa ukioneshwa na Man City kwa sasa haupo na inaonekana wazi hata wachezaji hawataki kukikmbia kilometa nyingi. Utagundua kuwa timu imekuwa ikiyumba sababu ile hali ya kombinenga ya kila idara imeyeyuka. Ni jukumu la Pep Guardiola kurudisha kiwango cha mchezo cha Man City.
Comments
Loading…