Klabu ya Mashujaa wa Lake Tanganyika wameendeleza ushujaa wao kwa kuitoa klabu ya Simba katika kombe la CRDB federation cup. Wameitoa katika mechi ambayo iliishia katika mikwaju ya penati. Klabu ya Mashujaa ilishinda mechi hiyo na hatimaye na kuitoa klabu ya Simba. Mechi hii imeibua hisia kubwa sana kwa washabiki wa klabu ya Simba kwani wengi wameona kwamba kutolewa huko kunatokana na madhaifu ya uongozi uliopo madarakani katika klabu hiyo na wengi wao wamekuwa wanatoa maoni yao katika mitandao ya kijamii kwa hisia kali sana. Kipigo hiko kimepelekea hadi kuwepo kwa ziara ya mdhamini mkuu wa klabu bwana Mohammed Dewji hiyo kutembelea klabu hiyo na kuongea na wachezaji pamoja na benchi la ufundi ambalo liko chini ya kocha mkuu Benchikicha.
Mechi hiyo ilikuwa ina msisimko mkubwa sana kwanza imechezwa siku chache baada ya benki ya CRDB kutangaza kwamba watadhamini mashindano hayo kwa muda wa miaka 3 na mashindano hayo yakabadilishwa jina kutoka Azam federation cup na sasa yanakuwa ni CRDB federation Cup. Udhamini huo wa miaka 3 wenye thamani ya pesa za kitanzania Zaidi ya bilioni 3 na hilo litaongeza hamasa kwenye mashindano hayo. Pili msisimko mwingine umetokana na kwamba vilabu hivyo vilikutana mnamo Machi 15 mwaka huu wa 2024 katika mechi ya ligi kuu ya NBC katika uwanja wa Azam Complex ambapo klabu ya Simba ilishinda kwa jumla ya magoli 2 na klabu ya Mashujaa hawakupata hata goli moja. Magoli hayo yote mawili ya Simba yalifungwa na mchezaji wa kimataifa kutoka Zambia Clatous Chama ama mashabiki wa Simba hupenda kumuita “mwamba wa Lusaka” Mechi hiyo nayo ilizua mjadala mtandaoni kwani wakati mechi inaendelea mshabiki mmoja ambaye inasadikiwa kuwa alikuwa mshabiki wa klabu ya Simba aliingia uwanjani na kuelekea mahala ambapo alikuwepo golikipa wa klabu ya Mashujaa na kisha kuchukua taulo lake la kujifutia jasho na kukimbia kwa nguvu na kurudi nalo kwenye jukwaa la mashabiki. Baada ya kufanyika kwa kitendo hicho ndipo klabu ya Simba ikaweza kujipatia hayo magoli mawili na hatimaye kujipatia ushindi. Kitendo hicho kililaaniwa na mashabiki wa soka mitandaoni na kikanasibishwa na Imani za kishirikina.
Kwa historia ya hivi karibuni Klabu ya Mashujaa kwa namna Fulani ni mbabe wa klabu ya Simba kwani ina historia ya kuitoa klabu hiyo katiika hatua ya 64 bora ya mashindano ya shirikisho mnamo mwaka 2018. Mwaka huo klabu hiyo ilikuwa inashiriki ligi daraja la kwanza. Walishinda mechi hiyo baada ya kuichapa klabu ya Simba magoli matatu dhidi ya mawili ambayo yalikuwa yamefungwa na klabu ya Simba. Mechi hiyo ilichezwa mnamo Disemba 26 mwaka 2018 katika dimba la uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo jijini Dar es salaam.
Safari ya klabu ya Mashujaa wa Lake Tanganyika ni ndefu kwani ni klabu ambacho kimesota sana mpaka kufika katika hatua hiyo kwani imekaa sana katika ligi za chini. Imekaa katika ligi daraja la kwanza kwa misimu Zaidi ya 4. Timu hiyo ilifanikiwa kuiingia ligi kuu baada ya kushinda katika hatua ya mtoano (Play off matches) baada ya kushika nafasi ya tatu katika ligi daraja la kwanza ambayo kwa sasa inaitwa Championship ambapo walifanikiwa kuingia kibabe kwa kuwatoa klabu nguli cha soka cha kutoka jijini Mbeya yaani Mbeya City FC. Waliwatoa Mbeya City kwa kuwafunga kote yaani wakiwa nyumbani na wakiwa ugenini. Walianza mechi yao ya mtoano wakiwa kigoma ambako waliwafunga wapinzani wao na wakawafuata ugenini jijini Mbeya wakawafunga huko huko na waliporudi walipokewa kwa shangwe kubwa sana. Ikumbukwe klabu hiyo ina historia ya kuwahi kuifunga klabu kongwe nchini ya Simba katika kombe la FA na kuwaduwaza mashabiki wa soka nchini. Baada tu ya kuingia ligi kuu klabu hiyo ilitangaza kwamba imevunja mkataba na aliyekuwa kocha wake Meja Abdul Mingange na kisha kumchukua Mohammed Bares kama kocha mkuu wa klabu hiyo ambaye ndiye yuko na klabu hiyo mpaka sasa.
Katika maandalizi yake ya msimu uongozi wa klabu hiyo halikadhalika ulizindua jezi ambazo wanazitumia kwa msimu huu wa ligi na uzinduzi wake uligusa hisia za wadau wengi wa soka katika mitandao ya kijamii. Picha za uzinduzi wake zilisambaa sana katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Mechi yake ya kwanza katika ligi kuu msimu huu walianzia nyumbani na ama kweli walionyesha uhai kidogo kwani waliweza kuwahamasisha mashabiki wengi kujitokeza kwenda kuwashangilia katika uwanja wao wa nyumbani na dalili zaonyesha itakuwa ni mojawapo ya timu chache ambazo zitakuwa zina mechi zenye msisimko hususani katika mechi za nyumbani kwani ina mtaji wa mashabiki wengi nyuma yake.
Klabu hiyo ni mojawapo ya vilabu ambavyo kama vikijipanga vizuri zinaweza kuwa ni vilabu tishio hapa nchini. Viongozi wa klabu hiyo wanatakiwa wajipange na kuwa na mpango endelevu wa kuifanya kwanza klabu hiyo ijitanue kwa idadi ya mashabiki na matawi katika maeneo mbalimbali ya nchi pili wawe na kikosi ambacho kitakuwa na matokeo mazuri ambayo kitawafanya mashabiki wazidi kuwa na imani na klabu hiyo na kuendelea kuisapoti tatu wawe na maono ya kuja kubeba ubingwa katika misimu ya karibuni kwani nina imani wana rasilimali zote zinazohitajika katika kujipanga na kuja kuwafanya wawe ni mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania.
Comments
Loading…