AINA ya usajili wa klabu yoyote ndiyo unaonesha malengo yake. Pia usajili huo unaonesha kuwa uongozi unajua mapengo au idara ambazo zinatakiwa kuimarisha katika timu. Usajili wa Arsemal katika majira ya kiangazi hiki upo katika maeneo ya kiungo mkabaji, beki wa kati, na safu ya ushambuliaji.
Maeneo hayo yameonesha kuwa kocha Mikel Arteta na benchi zima limeona ipo haja ya kuimarisha zaidi. Pengine wanatoa majibu juu ya sababu iliyowafanya wakose ubingwa. Katika mahojiano na Podcast ya Denilson ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Arsenal, mshambuliaji Gabriel Jesus alisema kila kitu kilibadilika mara baada ya kuumia William Saliba. Alisema mfumo ulibadilika, kila mchezaji alijikuta akitakiwa kubadilika kutokana na mfumo wa Mikel Arteta.
Kwa maana hiyo Arsenal iliingia katika mfumo mpya kwakuwa haikuwa na beki mbadala mwenye kiwango cha juu. Maneno ya Gabriel Jesus yanajibiwa sasa na benchi la ufundi ambalo limemsajili beki wa kati kuongeza nguvu. Hata hivyo kikosi cha Arsenal huenda kiaongezewa nguvu kwa kusajiliwa wachezaji wapya katika maeneo mawili; kipa na mabeki wa pembeni.
Zipo taarifa kuwa Arsenal inamfukuzia golikipa David Raya ili aingie kikosi kuimarisha eneo la golikipa. Arsenal imecheza kwa msimu mzima ikiwa na kipa Aaron Ramsdale ambaye bila kumung’unya maneno aliibeba timu kwa kuokoa michomo mingi. Lakini naye ni mchezaji anayehitaji kupata changamoto ya ushindani wa namba. Ili timu iwe bora lazima ushindani wa kila nafasi uwe wa juu. Golikipa wa Arsenal ammekuwa tegemeo na hapumzika vya kutosha kwa sababu waliokuwepo hawana hata ile nusu ya ufanisi wake.
Ramsdale pia amefanikiwa kuboresha uchezaji wake kwani hapo nyuma alikuwa na changamoto ya kucheza katika mfumo wa kisasa ambao unamtaka golikipa kuwa mchezaji wa 11 ndani ya dimba akiwa beki wa mwisho. Ufundi huo anao Andre Onana ambaye husogea hadi 26 kutoka langoni mwake na kushiriki upigaji wa pasi za kuandaa mashambulizi akiwa na mabeki wake. Mara kadhaa Arsenal kulitokea makosa wakati wa kurudishiana pasi au kupiga pasi za kuipanga timu kuelekea lango la adui. Makosa hayo yaliwahi kuwafungisha na hivyo kamera nyingi zikaelekezwa kwa Aaron Ramsdale. Ni muhimu benchi la ufundi kukubali kuwa eneo la golikipa kuna pengo ambalo linatakiwa kuzibwa kwa kuongezewa ushindani.
Eneo la pili ni mabeki wa pembeni; kulia na kushoto. Alexandr Zinchenko ni beki mzuri ambaye anafaa kuceza winga pia, lakini anahitajika Yule mwenye uwezo wa kudhibiti wapinzani na kulinda eneo la kushoto mwa Arsenal. Kwahiyo beki wa kushoto ni eneo ambalo linapaswa kulengwa.
Upande wa kulia bado hakuna ufanisi katika kupanda mbele au kuandaa mashambulizi. Ni eneo ambalo beki wa kulia wa sasa anatakiwa kupata ushindani utakaomwimarisha au kumtoa. Beki wa kulia anatakiwa kuwa ngangari na mwenye kutumikia mfumo wa Mikel Arteta wa kushambulia kuanzia nyuma.
Ikiwa kocha huyo ataendelea kubaki na wachezaji waliopo katika maeneo hayo bila shaka anaweza kuumizwa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa ambako kuna wachezaji wakali na wenye ujuzi wa hali ya juu.
Kimsingi mapengo hayo mawili yanatakiwa kufanyiwa kazi ikiwa timu inataka kuendeleza cheche za kupigania ubingwa, kwani wapinzani wao wanazidi kujiimarisha na watataka kuwatupa nje ya kinyang’anyiro cha ubingwa.
Comments
Loading…