Baada ya tetesi za kuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter alikuwa anawindwa kwa rushwa, maofisa wake sita wamedakwa alfajiri jijini Zurich, Uswisi.
Maofisa hao, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Fifa, Jeffrey Webb wametiwa nguvuni na polisi wa Uswisi kwa maombi ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Kamata kamata hiyo iliandaliwa kifundi na kukamilishwa alfajiri katika hoteli walimokuwa wamefikia wajumbe hao, kabla ya mkutano wa uchaguzi wa rais wa Fifa uliopangwa kufanyika Ijumaa hii.
Kumekuwa na habari kwamba Blatter hukwepa kwenda Marekani tangu miaka minne iliyopita akihofia kudakwa na FBI waliokuwa wanachunguza kashfa za mlungula zinazonuka ndani ya shirikisho hilo kuhusiana na uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022 nchini Urusi na Qatar.
Blatter anawania kuchaguliwa kwa muhula wa tano, amekuwa akipingwa na wengi lakini kadiri muda unavyokwenda wapinzani wake wamejitoa.
Webb ndie mkuu wa Fifa kwa maeneo ya Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean. Wengine waliokamatwa ni Eduardo Li wa Costa Rica, Eugenio Figueredo wa Uruguay na yule wa Brazil, Jose Maria Marin.
Askari polisi wa Uswisi walikuwa bado maeneo ya hoteli hiyo hadi saa mbili asubuhi (saa nne kwa saa za Afrika mashariki) japokuwa kamata kamata ilidhaniwa kumalizika. Blatter hajadakwa.
Li alitakiwa kuhudhuria mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Fifa Ijumaa hii wakati Marin aliyetolewa hotelini kwa mlango wa pembeni ni mjumbe wa Kamati ya Fifa ya Klabu na polisi walikuwa wamebeba sanduku lake dogo jeusi na vitu vingine vyake kwenye mifuko ya plastiki.
Mkutano wa maofisa wa ngazi za juu wa Fifa wanatarajiwa kuanza mkutano kwenye makao makuu ya shirikisho hilo, huku Wizara ya Sheria ya Marekani kitarajiwa kutoa taarifa juu ya zoezi hilo baadaye.
Polisi walianza zoezi la kukamata maofisa hao kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya Baur au Lac usiku wa manane wa Jumanne na inadhaniwa kwamba Marekani wataomba kibali ili maofisa hao wasafirishwe hadi huko kushitakiwa.
Wizara ya Sheria ya Uswisi imesema kwamba wanaoshikiliwa wanachunguzwa kwa madai ya kupokea rushwa kati ya mapema miaka ya ’90 na siku za karibuni, kiasi hicho kikiwa ni zaidi ya dola milioni 100.
Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke alitembelea hoteli hiyo kwa muda mfupi JUmatano hii kabla ya kuondoka bila kusema lolote.
“Tumeona taarifa kwenye vyombo vya habari na tutatafuta ufafanuzi juu ya suala hili baadaye,” alieleza msemaji wa Fifa baadaye.
Baada ya wapinzani wake waliokuwa wakimtuhumu kwa utawala mbovu kujitoa, Blatter amebaki kuchuana na Mwana wa Mfalme wa Jordan, Ali bin al-Hussein kwenye uchaguzi wa Ijumaa. Wasaidizi wa Prince Al-Hussein nao wanakutana kujadili athari za tukio la ukamataji maofisa wa Fifa.