De Gea hatoki bila Ramos kuja
Manchester United wamezuia dili la kumpeleka golikipa wao, David De Gea Real Madrid hadi watakapopewa beki wa kati, Sergio Ramos.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa United, Ed Woodward, anasimamia suala hili binafsi na anasema hataondoka Old Trafford kirahisi.
Kana kwamba kumtaka Ramos haitoshi, Man U wanamtaka pia kipa chaguo la pili wa Madrid, Keylor Navas, ikimaanisha kwa kumwachia De Gea United wapewe wachezaji wawili.
Hata hivyo Real Madrid wanasisitiza kwamba Ramos atabaki na kuna uwezekano akasaini mkataba mpya wakati wowote.
Tayari Madrid wamemwachia kipa wao namba moja, Iker Casillas kwenda Porto nchini Ureno, ikionesha kwamba wanajiamini kumpata De Gea ambaye ni raia wa Hispania na amepata kucheza Atletico Madrid.
Wakati kocha wa Manchester, Louis van Gaal akimsifu kipa wake, bado hana uhakika iwapo atakuwa kwenye ndege kwenda na wenzake kwenye ziara nchini Marekani kujiandaa na msimu mpya.
Madrid pia wanazungumza na Espanyol kwa ajili ya kumsajili kipa wao, Kiko Casilla, japo klabu hiyo inataka kiasi kikubwa cha ada, kwenye euro milioni 10 ambazo Madrid hawataki kutoa, bali euro milioni sita na nane.
United nao hawajakaa kimya juu ya hatima ya lango lao, japo wanaye Victor Valdes waliyempata kutoka Barcelona akiwa mchezaji huru.
Wanawafikiria kipa wa Slovenia anayecheza Atletico Madrid, Jan Oblak, kipa wa Ajax, Jasper Cillessen na Hugo Lloris wa Tottenham Hotspur kuziba pengo la De Gea iwapo ataondoka.