in , , ,

Manchester City, United zalipua

*Arsenal hali ngumu, Liverpool yalala pia

 

Klabu hasimu za Jiji la Manchester zimeendelea kuchanja mbuga kwenye Ligi Kuu ya England, kwa kuziadhibu Arsenal na Liverpool.
Wakati Manchester United wamefikisha pointi 55 kwa kuwalaza Liverpool mabao 2-1, jirani zao Manchester City wamekusanya pointi 48 baada ya kuwaadhibu Arsenal mabao 2-0.
Arsenal walioingia uwanjani kwa kujiamini, hasa katika kiungo baada ya kurejea kwa Abou Diaby aliyekuwa majeruhi, walianzia mguu mbaya.
Kwa muda mwingi wa dakika 90 walicheza 10 tu, kwani beki wao, Laurent Koscielny alipewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Koscielny aliadhibiwa kwa kumshika, kumvuta na kumwangusha Edin Dzeko ndani ya eneo la hatari wakati akitaka kufunga.
City walipewa penati, iliyopigwa na Dzeko mwenyewe, ikafika miguuni pa golikipa Wojciech Szczesny kabla ya kugonga mlingoti wa goli, kurudi kati na kudankwa kwa ustadi na golikipa huyu aliyekuwa amegeukia langoni mwake tayari.
Ilikuwa ngumu kwa Arsenal kucheza watu 10, ambapo haikuwachukua muda ‘Citizens’ kuwafunika wapinzani wao, kwani James Milner na Edin Dzeko walifunga mabao dakika ya 21 na 32.
City nao walipata zahama ya kadi nyekundu, kwani nahodha wao, Vincent Kompany alitolewa nje dakika ya 75 kwa kumkabili vibaya Jack Wilshere aliyekuwa akielekea langoni kwa kasi.
Hata hivyo, kocha wa City, Roberto Mancini anasema watakata rufaa dhidi ya kadi nyekundu ya Kompany, huku Arsene Wenger akikiri kwamba timu yake ilionesha udhaifu na penati dhidi ya kitendo cha Koscielny ilikuwa sahihi. Alisema ataangalia mkanda wa video juu ya ukabaji wa Kompany, akiwa pia hashabikii kadi dhidi yake.
Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 31 kwa klabu hiyo ya Manchester kuwafunga Arsenal nyumbani kwao.
Mara ya mwisho kwa ushindi wa vijana hao wa Estlands ilikuwa Oktoba 4, 1975, pale Asa Hartford, Joe Royle na Rodney Marsh walipofunga na kuwazidi Arsenal mabao 3-2 katika uwanja wa Highbury.
Kipigo hicho kimewachanganya Arsenal, kikiwaacha na pointi zao 34 katika nafasi ya sita, na wanakutana na Chelsea Jumapili ijayo. 
Jumatano hii wanakwaana na Swansea katika marudio ya mechi ya Kombe la FA, baada ya kutoshana nguvu 2-2 kwenye mchezo uliopita Liberty Stadium.
Jijini Manchester kwenyewe, mambo yalikuwa Old Trafford, ambapo Liverpool walizidiwa kipindi cha kwanza na kuonekana kuwa na nguvu dakika za mwisho, lakini wakashindwa kupata walau pointi.
Lilikuwa pambano lililosubiriwa kwa hamu, likichukuliwa kuwa vita kati ya wapachika mabao wawili mashuhuri, Robin van Persie wa United na Luis Suarez wa Liverpool.
Alikuwa Van Persie aliyewaamsha washabiki wa United vitini dakika ya 19 kwa bao la kiufundi mbele ya mabeki wa Liverpool.
Kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko, Liverpool wakimwingiza nyota wao mpya, Daniel Sturridge, waliyemsajili kutoka Chelsea Januari hii.
Hata hivyo, walikuwa Man U tena waliocheka dakika tisa tu za mwanzo, baada ya mpira wa kichwa wa Patrice Evra kumparaza nahodha wa United, Nemanja Vidic na kuzama langoni mwa Liverpoo.
Baada ya mchezo, Evra alinukuliwa akilalamika ‘kupunjwa’ bao lake, akisema angekuwa mshambuliaji mwingine angepewa. Hili lingekuwa bao lake la tano.
Sturridge aliyesajiliwa kwa pauni milioni 12 alianza kulipa fadhila kwa kufunga bao, lakini alikosa nafasi nyingine muhimu ya kuweka kimiani bao la pili.
United walikalia kiti wakiwa na pengo la pointi 10, wakiomba City wafungwe, lakini likawa dua la kuku lisilompata mwewe, pengo likarudia pointi saba.
Liverpool wanaweza kujipa moyo kwamba ushindi wa United dhidi yao ni mwembamba, hasa kwa klabu ambayo ni mpinzani wake wa jadi tangu kale.
Hata hivyo, pengo la pointi 25 kati ya mahasimu wawili hao linaacha maswali mengi juu ya utani wenyewe, na kudhihirisha kwamba bado Liverpool wana kazi ngumu kufika kwenye kilele cha jedwali la ligi.
Pengine vijana hao wa Brandan Rodgers walikuwa kimya mno, wakikosa ubunifu wa kufungua vyumba na kutanua uwanja, wakaja kushituka baada ya Man U kutangulia kwa mabao hayo.
Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Stoke mbendembende kwa Chelsea

Woga wa penati AFCON