*Ni $117 milioni isipomaliza nne bora
Shinikizo dhidi ya Kocha Mkuu wa Manchester United, David Moyes linazidi.
Imetangazwa kwamba wasipomaliza katika nafasi nne za juu, watapata hasara ya dola milioni 117.
Wataalamu wa uhasibu wamekokotoa na kubaini kwamba kwa sasa licha ya mwenendo mbaya wa klabu hesabu zipo vizuri lakini zitatumbukia nyongo mwakani.
Inakadiriwa kwamba hasara itaanzia dola milioni 67 awali, lakini hali inaweza kuwa mbaya hadi kufikia hadi dola milioni 117 mapema mwakani.
Timu hii iliyoachwa na Sir Alex Ferguson mwishoni mwa msimu uliopita na kumpendekeza Mskochi mwenzake Moyes amrithi inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Hata baada ya kuambulia suluhu dhidi ya Arsenal Jumatano hii ambayo baadhi ya washabiki walifurahi kuliko wangefungwa, imewaacha pointi 11 nyuma ya vinara wa ligi hiyo.
Mashetani Wekundu hao wamebakisha mechi 12 kabla ya msimu kufungwa na wana mechi tatu dhidi ya timu zilizo nafasi tano za juu, nazo ni kati yao na Liverpool na Manchester City zote zikichezwa Old Trafford na dhidi ya Everton kule Goodison Park.
Kutokana na msimu uliopita Man U kufanya vyema walijizolea dola milioni 70, kati ya hizo 50 zikitokana na haki za kurushwa matangazo na 20 kwa mapato ya mechi za nyumbani.
Hata hivyo, hasara hiyo inaweza kupungua iwapo watafuzu kucheza Ligi ya Europa lakini mapato ya ligi hiyo ndogo yenye mechi nyingi ni pungufu sana.
Taarifa hizo zinakuja wakati nyingine zikionesha kwamba katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2013/14 hali ya fedha imekuwa nzuri na mipango ni kuongeza mapato kutoka dola milioni 603.97 hadi dola milioni 698.
Comments
Loading…