*Man City wameanza vyema UCL
*Leicester wafufukia Ubelgiji
Manchester United wameanza vibaya michuano ya Ligi ya Europa kwa
kukubali kichapo cha 1-0 nyumbani kwa Feyenoord wakati jirani zao
wakichanua kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
United wanaofundishwa na Jose Mourinho walicheza vibaya huku mchezaji
ghali zaidi duniani, Paul Pogba akishindwa kabisa kuonesha makali yake
kwenye kiungo, ikiwa ni mechi ya pili mfululizo kukosa kiwango.
Kocha alifanya mabadiliko manane katika kikosi kilichokung’utwa na
Manchester City kwenye Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo Anthony
Martial alipewa nafasi kuonesha makali lakini akawa ‘cha mtoto’.
Zlatan Ibrahimovic ambaye kwa sasa ndilo tegemeo kubwa kwa United
kwenye ushambuliaji aliingizwa kipindi cha pili kuwanusuru lakini
jahazi likazama tu.
Alikuwa ni Tonny Vilhena aliyepigilia msumari jeneza la Mashetani
Wekundu hao, akiwapa bao Feyenoord dakika 11 tu kabla ya mchezo
kuanza. Kichapo hicho kinamaanisha kwamba United wamepoteza mechi zote
nne za Ulaya walizocheza Ulaya na hii ni mara ya kwanza. Haileti picha
nzuri sana kwa Mourinho.
Matokeo mengine Ligi ya Europa
Katika mechi nyingine za ligi hiyo ndogo ya Ulaya AZ Alkmaar
walikwenda sare ya 1-1 na Dundalk; Southampton wakawafyatua Sparta
Prague 3-0; FK Qarabang wakaenda nguvu sawa na Slovan Liberec
walipofungana 2-2.
Upande mwingine Rapid Vienna waliwafunga KRC Genk 3-2; Sassuolo
wakawaminya Athletico Bilbao 3-0; Viktoria Plzen wakatoshana nguvu na
Roma 1-1 huku Astra Giurgiu wakilala nyumbani kwa 2-3 wakiwa wenyeji
wa FK Austria.
Waisraeli Maccabi Tel Aviv walilala kwa 3-4 walipowakaribisha Zenit
Saint Petersburg kutoka Urusi; Apoel Nic waliwashinda FC Astana 2-1;
BSc Young wakalala 0-1 wa Olympiakos huku FSV Mainz wakitoshana nguvu
1-1 na Saint Etienne.
Manchester City wawararua Monchengladbach
Wakati kilio kikienda Manchester United, jirani zao Manchester City
walikuwa tayari kwenye kicheko, kwani walitoka kuwararua Borussia
Monchengladbach wa Ujerumani 4-0.
Sergio Aguero aliendeleza makali yake kwa kufunga mabao matatu
(hat-trick) kwenye mechi hiyo, ikiwa ni hat-trick ya pili msimu huu.
Ilikuwa mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) chini ya kocha
Pep Guardiola. Aguero alifunga baada ya mlinzi Aleksandar Kolarov
kumtilia majalo kabla ya kufunga kwa penati kutokana na mchezaji
mwenzake, Ilkay Gundogan kuchezewa rafu.
Bao la tatu lilikuwa tamu, kwani alimzunguka kipa Yann Sommer kabla ya
kucheka na nyavu mbele ya washabiki wachache 32,000 hivi, idadi hiyo
ikitokana na mechi hiyo kuahirishwa kwa siku moja na kuwavurugia
ratiba wenyeji hao hao Etihad.
Kelechi Iheanacho aliyeingia kipindi cha pili alifunga bao, akiachia
kiki kali kutoka umbali wa yadi 12. Mechi hiyo ilishuhudia washabiki
wa City wakizomea wakati Wimbo wa UCL ukipigwa, kitendo
kilichomkasirisha Guardiola aliyewataka wabadilike na wakati. Mechi ya
awali iliahirishwa kutokana na mvua kunyesha.
Matokeo mengine UCL
Katika mechi nyingine za siku hiyo ya pili ya michuano ya UCL ni
kwamba Tottenham Hostpur walishindwa kutumia vyema nafasi ya kucheza
nchini mwao, wakakubali kisago cha 2-1 kutoka kwa Monaco wa Ufaransa.
Spurs ambao walicheza kwenye Uwanja wa Taifa wa England – Wembley
kutokana na uwanja wao wa White Hart Lane kuwa mdogo walizidiwa nguvu
na Wafaransa.
Real Madrid walidhihirisha ubora wao kwa kuwatandika Sporting Lisbon
2-1 huku mabingwa watetezi wa England, Leicester nao wakichanua.
Vijana hao wa Claudio Ranieri wakicheza ugenini walishinda 3-0 dhidi
ya Club Brugge nchini Ubelgiji.
Ranieri alimsifu Riyad Mahrez kwa kufunga mabao mawili, moja la
penati, akisema kwamba mchezaji huyo wa Algeria aliamshwa na Wimbo wa
UCL kurudi kwenye makali yake ya msimu uliopita, baada ya kuianza EPL
akisuasua. Bao jingine la Leicester lilifungwa na Marc Albrighton.
Bayern Leverkusen walikwenda sare ya 2-2 na CSKA Moscow; Legia Warsaw
wafyatuliwa 6-0 na Borussia Dortmund; Porto wakaenda sare ya 1-1 na FC
Copenhagen; Juventus wakabanwa 0-0 na Sevilla wakati Lyon
wakiwachakaza Dinamo Zagreb 3-0.