in , , ,

MAN U v ARSENAL JUMAPILI

 

Zimebaki raundi 12 pekee kuelekea ukingoni mwa Ligi Kuu ya England msimu huu. Jumapili hii Manchester United walio kwenye nafasi ya tano kwenye jedwali la EPL watakuwa wenyeji wa Arsenal wanaoshikilia nafasi ya tatu.

Arsenal walio nyuma kwa alama mbili pekee dhidi ya vinara wa Ligi hiyo Leicester City wenye alama 53 pengine ndio wanaopewa nafasi ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo wa hapo Jumapili.

Ingawa Washika bunduki hao wa London hawajapata kuibuka na ushindi wowote kwenye mchezo wa EPL ndani ya dimba la Old Trafford tangu Septemba 2006 lakini wanatazamiwa kuwapa wakati mgumu wenyeji wao kwenye mchezo huo.

Licha ya kupata matokeo mabaya kwenye michezo yao miwili ya mwisho dhidi ya Hull City waliotoka sare tasa na ule waliopokea kipigo cha 2-0 kutoka kwa Barcelona, lakini pengine ushindi walioupata dhidi ya Leicester kwenye mchezo wao wa mwisho wa EPL unawapa nguvu vijana wa Wenger kuelekea mchezo wa Jumapili.

Manchester United wao wameshindwa kuibuka na ushindi kwenye michezo miwili mfululizo ya EPL dhidi ya Chelsea ulioisha kwa sare ya 1-1 na ule wa dhidi ya Sunderland walioambulia kipigo cha 2-1.

Hata hivyo matokeo ya ushindi wa 3-0 kwenye mchezo wa FA dhidi ya Shrewsbury wikiendi iliyopita na ule wa Europa walioshinda 5-1 dhidi ya Midtjylland Alhamisi pengine yanawapa vijana wa van Gaal matumaini kuelekea kibarua chao cha Jumapili.

Kitakwimu Arsenal wapo mbele mno dhidi ya Manchester United kwenye EPL msimu huu. Vijana hao wa Arsene Wenger wamewaacha nyuma wapinzani wao hao kwa alama 10 kwenye jedwali la ligi hiyo.

Alex Oxlade-Chamberlain, majeruhi
Alex Oxlade-Chamberlain, majeruhi

Wapo mbele pia kwenye idadi ya mabao ya kufunga wakiwa wamefunga mabao 41 kwenye michezo yote 26 ya EPL dhidi ya yale 33 ya Manchester United kwenye idadi hiyo hiyo ya michezo.

Kwa upande wa vikosi wenyeji Manchester United watawakosa nyota kadhaa muhimu akiwemo nahodha Wayne Rooney kutokana na majeraha. Wengine ni Fellaini, Phil Jones, Shaw, Young na Bastian Schweinsteiger.

Kuna mashaka pia kuwa David De Gea, Antonio Valencia, Matteo Darmian, Anthony Martial na wengine waliotoka kwenye majeraha hivi karibuni huenda wakashindwa kupatikana kwa ajili ya mchezo huo.

Arsenal pia wanao wachezaji kadhaa majeruhi akiwemo Oxlade-Chamberlain aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya Barcelona. Wamo pia Santi Carzola, Jack Wilshere na Mikel Arteta. Pengine kutokuwepo kwa wachezaji hao hakuna nafasi ya kuharibu mipango ya Arsene Wenger juu ya mchezo wa Jumapili.

Kiufundi kuna uwezekano mkubwa Arsene Wenger akatumia mbinu tofauti na zile zilizompatia ushindi wa 3-0 alipokutana na wapinzani wake hawa mara ya mwisho Oktoba mwaka jana.

Kwenye mchezo huo Arsene Wenger aliwaacha wapinzani watawale mchezo huo huku vijana wake wakijihami zaidi na kufanya mashambulizi ya kustukiza. Ingawa Manchester United walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 62 lakini bado Arsenal wakaibuka na ushindi.

Pengine alilazimika kutumia mbinu hizo kwa kuwa United walionekana kuwa imara kwa kiasi fulani wakati ule. Lakini kwa kuwa kwa sasa vijana hao wa van Gaal wanaonekana kutetereka huenda Arsene Wenger akahitaji kutumia mbinu za kutawala mchezo.

Hata hivyo haitaweza kuwa rahisi kwa vijana wa Arsene Wenger kutawala mchezo huo. Hii inatokana na ukweli kwamba vijana wa van Gaal ndio vinara wa wastani umiliki wa mpira kwenye EPL msimu huu. Pengine wataendeleza makali yao kwenye aina hiyo ya mchezo.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Fifa mageuzi makubwa

Tanzania Sports

Leicester mbele kwa mbele