Manchester City wamejihakikishia hawaondoki patupu msimu huu, baada ya
kutwaa Kombe la Ligi, maarufu kama Capital One Cup.
Vijana wa Manuel Pellegrini hawakuwa na kazi rahisi ya kumpa kombe
kocha wao kabla ya kumuaga mwishoni mwa msimu, kwani walilazimishwa
sare ya 1-1 na Liverpool kwenye Uwanja wa Taifa wa Wembley.
Ilibidi waingie kwenye changamoto ya mikwaju ya penati, na ni hapo
kocha Pellegrini alipata raha na karata aliyocheza ya kuendelea
kumtumia kipa Willy Cabalero aliyecheza mechi na dakika zote za
michuano hiyo.
Baada ya kuchabangwa 5-1 na Chelsea kwenye mechi ya Kombe la FA
majuzi, washabiki walionelea kwamba kipa huyo wa Argentina mwenye umri
wa miaka 34 angetupwa kando ili kipa namba moja, Joe Hart arejee
kwenye lango.
Hata hivyo, Pellegrini atakayempisha Pep Guardiola kiangazi kijacho
hapo Anfield, alisema kwamba kuliko amwache Cabalero afadhali
wasilipate kombe hilo, na Jumapili hii alibaki na kipa wake huyo,
kisha baada ya mechi akasema yeye ni mtu wa kusimamia maneno yake.
Caballero alikuwa kipa kwenye kikosi cha Malaga ya Hispania
kilichokuwa kikifundishwa na Pellegrini, kisha alipoajiriwa kuwafunza
Man City akaamua kumsajili. Hata hivyo, hajafanya vyema sana kwenye
mechi za EPL, na Hart amekuwa ndilo chaguo la kwanza mara nyingi.
Wakati Hart akiwa benchi, Cabalero aliokoa penati tatu, ambapo City
walishindwa kwa penati 3-1. Caballero aliokoa penati za Lucas,
Philippe Coutinho na Adam Lallana . katika muda wa kawaida,
Fernandinho alifunga kwa upande wa City muda mfupi baada ya mapumziko
lakini makosa ya mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Raheem Sterling
yaliwazawadia bao Liver kupitia kwa Coutinho aliyesawazisha dakika ya
83.
Katika penati, Fernandinho aligonga mwamba kwa mkwaju wa kwanza wa
City, wakati penati za Jesus Navas, Sergio Aguero na Yaya Toure
zilizama nyavuni. Pamoja na kwamba anatemwa na ‘The Citizens’, tangu
aingie Etihad 2013, Pellegrini amewapatia makombe matatu.