Manchester City wamerejea kwenye uongozi wa Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kuwafunga Southampton 3-1.
Kocha wao, Manuel Pellegrini atakuwa amefarijika, hasa kutokana na kupokea kichapo cha 4-1 kwenye mechi iliyotangulia kutoka kwa Liverpool, wakati huu ambapo kuna tetesi kwamba wamiliki wa City wanataka kumwajiri kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola badala yake. Mabao ya City yalifungwa na Kevin De Bruyne, Phabian Delph na Aleksandar Kolarov. Saints walifunga kupitia kwa Shane Long.
Katika mechi nyingine, waliokuwa wakikalia kiti hicho kwa wiki moja, Leicester walikwenda sare ya 1-1 na waliokuwa nafasi ya pili, Manchester United, kwenye mechi ambayo mshambuliaji wa Leicester, Jamie Vardy amevunja rekodi kwa kufunga bao katika mechi 11 mfululizo.
United walisawazisha dakika ya 45 kupitia kwa kiungo wake Mjerumani, Bastian Schweinsteiger lakini walishindwa kupata bao la ushindi ambalo lingewawezesha kupanda hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.
Mshambuliaji namba moja wa United, Wayne Rooney ameonekana bado kushindwa kurejea kwenye kiwango chake cha miaka iliyopita, ambapo ilibidi kocha Louis van Gaal amtoe uwanjani kipindi cha pili, ikiwa ni mara ya pili tu kwa kocha huyo kufanya hivyo kwa nahodha wa kikosi chake.
Katika mechi nyingine, Aston Villa wakicheza nyumbani walilala kwa Watford kwa 3-2, Bournemouth wakatoka sare ya 3-3 na Everton, Crystal Palace wakawatandika Newcastle 5-1 ambapo kocha wa Newcastle, Steven MClaren alidai kwamba wachezaji wake wanashindwa kwenda kwa viwango vinavyotakiwa.
Sunderland wameanza kuzinduka baada ya kuwafunga Stoke 2-0 na kujiondoa kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja. Wapo chini ya kocha mpya, Sam Allerdyce ambaye kabla ya mechi alisema kwamba hawezi kuwahakikishia wadau kwamba hawatashuka daraja.
Leo Arsenal wapo ugenini kuwakabili Norwich, ambapo walisafiri kwa kutumia ndege ya kukodi japokuwa ni umbali wa dakika 14 tu, jambo lililowakasirisha wanaharakati wa mazingira na wadau wengine waliosema ni ufujaji wa fedha.