*Walinda heshima kwa kuwakandika 2-1
Pamoja na kuelekea kuachia ubingwa, Manchester City wamedhihirisha ubabe kwa mahasimu jirani zao, Manchester United.
Wakicheza ugenini katika dimba la Old Trafford, City wanaofundishwa na Mtaliano Roberto Mancini walipata mabao mawili dhidi ya moja la wapinzani wao.
Vijana wa Alex Ferguson ndio walioanza mpira kwa kasi, lakini ndani ya nusu saa ya kwanza City walibadilisha mwelekeo na kukamata udhibiti.
Hata hivyo, hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzake, japokuwa City walikuwa na kila sababu ya kuwa mbele.
Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili ziliwatosha City kuandika bao la kwanza, kupitia kwa James Milner aliyeachia kiki kali mbele ya msitu wa mabeki wa United na wachezaji wa City na kumpoteza maboya kipa David Da Gea.
Milner alipokea mpira huo kutoka kwa mchezaji wa zamani wa Arsenal, Samir Nasri, aliyetamba jana lakini hakuwa na bahati ya kuzifumania nyavu.
Mashetani Wekundu walighadhabika kwa kufungwa, wakatia shinikizo kwenye lango la City hadi kilipoelekeweka, japo kwa muda, dakika ya 58.
Bao lilitokea baada ya kipa Joe Hart kuwa ametokea kwa karibu mpira wa adhabu ndogo wa Robin van Persie, lakini ukampita juu na kukutana na beki wa United, Phil Jones aliyeuekeza wavuni, ukimgonga mgongoni nahodha wa City, Vincent Kompany.
Adhabu ndogo hiyo ilitolewa na mwamuzi Mike Dean, baada ya Yaya Toure kumfanyia rafu ya kizembe Rafael Da Silva, ilhali angeweza kuokoa mpira ambao haukuwa eneo la hatari.
Mancini aliyetangulia kusema timu nyingi hufungwa na Man U kwa sababu hucheza kwa kuogopa na kujijenga kisaikolojia kwamba lazima watafungwa, aliingiza silaha yake hatari dakika ya 71.
Huyo alikuwa Sergio Aguero, ambaye msimu uliopita alipachika bao lililopeleka ubingwa Etihad kwa mara ya kwanza tangu miaka 47 iliyopita.
Na dakika sita tu baada ya hapo, raia huyo wa Argentina alionesha makali yake, kwa kuwacharura mabeki kabla ya kutundika mpira kambani.
Alipokea pasi ya Toure aliyerekebisha makosa yake ya awali, naye akawachambua mabeki wapinzani na licha ya kusukumwa na kukwatuliwa hakwenda chini, bali akamtazama Da Gea na kukwamisha gozi la ng’ombe kona ya juu ya goli.
Mfungaji aliyepunguzwa kasi wa United, Robin van Persie naye alijaribu kufurukuta kwa kila namna na kila kona, lakini hakufanikiwa kupata bao.
Nahodha wa Manchester City, Vincent Kompany anasema mchezo huo na watani wao wa manchester siku zote ni maalumu sana kwetu, na kwa hakika washabiki wetu watasherehekea kwa muda mrefu.
Mancini alisema kwamba kitu pekee kitokanacho na mechi hiyo ni furaha ya ushindi dhidi ya mahasimu wao.
Hata hivyo, alisitiza mbio za ubingwa zimeshaisha na kwamba jambo la muhimu ni kushika nafasi ya pili, wala si kupunguza zaidi pengo la pointi 12 lililosalia kati yao.
Ferguson alisema lilikuwa pambano gumu lenye kukamiana kwingi baina ya timu mbili kubwa zaidi nchini, na akamsifu Aguero kwa umaliziaji wake mzuri aliouzoea.
United wamebakiwa na pointi zao 77 kutokana na mechi 31 wakati City wana pointi 65 kwa idadi hiyo hiyo ya mechi. Chelsea wanafuatia kwa pointi 58, sawa na Tottenham Hotspurs huku Arsenal wakiwa na pointi 56 katika nafasi ya tano. Spurs wamecheza mechi moja zaidi ya wenzake wote hao.
Comments
Loading…