*Ronaldo na rekodi ya mabao 501
Timu mbili za England, Manchester City na Manchester United zimewafutia Waingereza machungu ya kufungwa kwa Arsenal na Chelsea kwenye mechi za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Wakati Manchester City walifanikiwa kupata bao la ushindi dakika za lala salama dhidi ya Borussia Monchengladbach, kocha wao, Manuel Pellegrini amesema vijana wake bado hawajaiva na wameshinda kwa bahati tu.
City wakicheza ugenini walionekana kuwa dhaifu na kuruhusu bao dakika ya 54 kupitia kwa Lars Stindl, aliyeupiga mpira kiupande upande na kumzidi nguvu kipa Joe Hart, ambaye kabla ya hapo aliokoa penati.
Mönchengladbach walipata penati hiyo baada ya Nicolás Otamendi kumchezea vibaya Raffael, ambaye alikwenda kuipiga mwenyewe na kuokolewa na Hart kwenye kona ya chini kushoto mwa goli.
Otamendi alirekebisha makosa yake ya kusababisha penati kwa kusawazisha bao katika dakika ya 64 kabla ya Sergio Aguero kufunga penati dakika ya mwisho wa mchezo. Penati hiyo ilitolewa baada ya Aguero kuchezewa vibaya na Fabian Johnson kutokana na mpira wa kona.
City wamefungwa mechi tatu kati ya nne walizocheza kwenye michuano yote, ikiwa ni pamoja na kwenye Ligi Kuu walikopoteza kwa West Ham na Tottenham Hotspur na kwenye UCL wakapigwa na Juventus.
Matajiri hao wa Manchester wamebaki katika nafasi ya tatu kwenye kundi lao baada ya mechi mbili, wakiwa na pointi sawa na Sevilla, lakini wapo nyuma ya Juve kwa pointi tatu. Kipa wa kimataifa wa England, Joe Hart ndiye alikuwa nyota wa mchezo, akiokoa mabao kadhaa ya wazi.
Ushindi wa Jumatano hii ni wa tatu tu katika mechi 12 za UCL kwa City na unawapa matumiani ya kuvuka kwenye hatua ya makundi ikiwa wataendelea kupata ushindi kwenye.
MANCHESTER UNITED WAWAPIGA WOLFSBURG
Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester United wamepata ushindi wa kwanza kwenye UCL, ambapo wakicheza nyumbani Old Trafford, walifanikiwa kutoka nyuma kwa 0-1 na kuwashinda Wolfsburg wa Ujerumani 2-1.
Washabiki wa United walionesha wasiwasi, pale Daniel Caligiuri alipomalizia wavuni mchakato wa pasi sita mfululizo na kuandika bao la kwanza kwa wageni dakika ya nne tu ya mchezo, wakati ambapo washabiki wengine hawakuwa wametulia hata vyema vitini mwao
Ilibidi United waliotawala mchezo kwa asilimia 54 wasubiri kwa nusu saa hadi walipofanikiwa kupata penati baada ya mfungaji wa Wolfsburg kuunawa mpira kwenye eneo la hatari na Juan Mata akaikwamisha wavuni kusawazisha mambo.
Chris Smalling aliwapatia United bao la ushindi katika dakika ya 53, akimalizia pasi ya Mata kwa kuutia mpira kimiani kwa mguu wa kulia kutoka katikati ya boksi la penati na kuutuliza kona ya kulia upande wa chini wa goli.
Kocha Louis van Gaal alisema ulikuwa mchezo mgumu kutokana na jinsi Wajerumani walivyojipanga na kutengeneza nafasi, na kwamba hata baada ya kupata bao la pili ilikuwa ni mateso kwa sababu wachezaji walikuwa wamechoka.
Katika kundi hili, timu zote nne zina pointi tatu, kwani kila moja imeshinda mechi moja kati ya mbili zilziochezwa. CSKA Moscow Jumatano hii waliwafunga PSV Eindhoven 3-2 wakati PSV walishawafunga United kwenye mechi ya kwanza.
CRISTIANO RONALDO AJA NA REKODI MPYA
Cristiano Ronaldo amefikisha rekodi ya mabao 501 tangu aanze kucheza mpira wa kulipwa, akifikia hatua hiyo kwenye ushindi dhidi ya Malmo nchini Sweden, pale waliposhinda 2-0, mabao yote yakifungwa na Ronaldo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alifunga bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya Isco. Ronaldo, 30, alipachika la pili akimalizia mpira wa Lucas Vazquez aliyeingia kipindi cha pili.
Kwa mabao hayo, Ronaldo amemfikia mchezaji wa zamani wa Real, Raul ambaye akiwa klabuni hapo alifunga mabao 323, ambayo Ronaldo aliyafikia jana. Alisema alikuwa mwenye furaha kubwa kwenda Sweden na kuendelea kufunga mabao.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United alikofunga mabao 84 na Sporting CP alikofunga matatu, alisema kitu muhimu kwake na kwa wenzake ni timu kupata ushindi na kwamba mchezo huo ulikuwa mgumu, lakini walifanikiwa kuwadhibiti wapinzani wao.
Katika mechi ya kwanza ya kundi lao, Madrid waliwafyatua Shakhtar Donetsk 4-0, ambapo Ronaldo alifunga mabao matatu. Paris St-Germain wanashika nafasi ya pili kwenye kundi hilo kwa tofauti ya mabao tu, kwani wameshashinda dhidi ya Shaktar mara mbili kwa 3-0.
Raul, ambaye sasa anachezea New York Cosmos, alifunga mabao 323 katika mechi 741 alizochezea Real kati ya 1994 na 2010. Hata hivyo, Ronaldo amecheza mechi 308 tu na ana kila dalili za kuvuka rekodi hiyo kwa mbali. Alijiunga Real Julai 2009 akitoka United.
Ronaldo ndiye mfungaji anayeongeza kwa mabao mengi katika historia ya mashindano hayo, akiwa amefunga mabao 82, matano zaidi ya Lionel Messi wa Barcelona ambaye sasa ameumia na hivyo atakuwa na nafasi finyu ya kumfikia kwa kipindi hiki.
Katika mechi nyingine za UCL Jumatano hii, FC Astana walikwenda sare ya 2-2 na Benfica wakati Juventus waliwafunga Sevilla 2-0.