Ni dhahiri makocha wengi sasa wanatokana na kichwa cha Pep Guardiola akiwa amewajenga kifalsafa na mbinu na kuwavutia kupenda mtindo wa uchezaji wa timu zake…
ZIPO habari nyingi kuhusu umahiri wa Arrigo Sacchi. Yule bingwa wa kufundisha mpira aliyetikisa Ulaya akitokea Italia. Kuna mwingine Johan Cruyff, Mholanzi aliyewaleta mapinduzi Barcelona kupitia La Masia wakatikisa na soka la Tikitaka. Kuna akina Alex Ferguson, Arsene Wenger,Zinedine Zidane na wengine wengi wenye mafanikio lakini jina la Pep Guardiola limezidi kusambaa barani Ulaya kama moto wa kifuu. Pep Guardiola amezidi kusambaza falsafa ya mpira na kutengana viwango vipya vya utandazaji kabumbu kama alivyofundishwa na Johan Cruyff alipokuwa Barcelona kama mchezaji na akatekeleza mtindo huo akiwa Barcelona B.
TANNZANIASPORTS katika tathmini ya utendaji wa makocha imebaini kuwa wimbi kubwa la wapinzani na wanafunzi wa Pep Guardiola kuzidi kuibuka. Wapinzani wanataka kuwachukua makocha wanaofanya kazi na Pep Guardiola, huku wapo wanafunzi wake wa mpira wa miguu na ukocha wakiibuka kuwa makocha wazuri na wanaotegemewa kwa kizazi kijacho. Guardiola anaelekea kulishika zaidi soka la Dunia kwa upande wa kutengeneza makocha wa kileo ambao wanafundisha soka maridadi na kuachana lile la nguvu. Katika tathmini yetu tumeibaini karibu makocha saba ambao wanafundisha timu za Ligi Kuu mbalimbali duniani walikuwa wanafunzi wa Pep Guardiola au kuwa wasaidizi wake.
ENZO MARESCA
Huyu ni kocha wa karibuni ambaye ameondoka katika kikosi cha Manchester City baada ya kutwaa mataji matatu msimu huu. Maresca amekubali dau la kujiunga na klabu ya Leicester City ambao wameshuka daraja hivyo atakiongoza kikosi hicho kupambana ili kurudi EPL. Maresca ni sehemu ya mafanikio ya Guardiola, hivyo inalekea wapinzani wake nao wamenyakua msaidizi huyo wakiwa na matumaini ya kuona kandanda safi likichezwa Leicester City. Matarajio ya Leicester City bila shaka yoyote kuona soka safi likipigwa katika klabu yao na washabiki wa timu hiyo wanaamini “soka la Guardiola limefika uwanja wa King Power”
MIKEL ARTETA
Kati ya makocha ambao wamefanya vizuri msimu uliomalizika ni Mikel Arteta. Kabla ya kujiunga na mchezaji mwenzake wa zamani wa Arsenal, Edu Gaspar alikuwa kocha msaidizi wa Manchester City. Mikel Arteta alikuwa sehemu ya mafanikio ya Pep Guardiola ambaye alimchukua ili kuimarisha uwezo wa benchi lake kuifahamu EPL na mienendo yake. Wakati fulani Pep Guardiola amewahi kuviambia vyombo vya habari kuwa Mikel Arteta anaipenda sana Arsenal kiasi kwamba wakati akiwa msaidizi wake walipoifunga alikuwa hashangilii mabao yao. Gaurdiola alidai Mikel ni mnazi wa Arsenal kiasi kwamba ushindi wao dhidi ya Washika Bunduki hao ulikuwa unamuumiza moyo. Hata hivyo ni Mikel Arteta ndiye alikuja kumtikisa Pep Guardiola kwenye EPL msimu 2022/2023. Vita vya kuwania ubingwa vilikuwa vikubwa huku akiwa amewasajili wachezaji wawili Gabriel Jesus na Alexandre Zinchenko kutoka Man City walioimarisha kikosi chake. Ingawa Mikel Arteta aliukosa ubingwa katika mechi za mwisho lakini shughuli aliyoonesha na umahiri wake ilikuwa moto wa kuotea mbali. Hivyo kamari ya Arsenal kumpora Guardiola msaidizi wake huenda ingelisemwa ni kumdhoofisha. Lakini imedhihirika kuwa ufundi na soka analofundisha Mikel Arteta ni sawa na lile linalofundishwa Man City. Pasi nyingi, kumiliki mpira mwingi na kuutawala mchezo kwa dakika zote 90 au 120. Hapa Guardiola apewe maua yake.
ERIC TEN HAG
Kabla ya kutua Manchester United alikuwa kocha wa Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Lakini kabla ya kutua Ajax alikuwa kocha msaidizi wa Pep Guardiola pale Bayern Munich. Hii ina maana Ajax Amsterdam walichukua ufundi wa Guardiola na kuupeleka katika kikosi chao. Ten Hag alifanya kazi nzuri akiwa na kikosi hicho na kutamba kwenye Ligi ya Uholanzi. Sasa Eric Ten Hag ni kocha wa Manchester United, ikiwa na maana ileile hata magwiji wa Old Traford wanatarajia kuona soka maridadi likitaradadi katika klabu yao. Eric Ten Hag katika msimu wake wa kwanza amemaliza akiwa na taji la Carabao. Man united imebadilika na inacheza mpira mzuri unaofundishwa na mwanafunzi wa Pep Guardiola.
XABI ALONSO
Akiwa klabu ya Bayrn Munich alipata ujuzi kutoka kwa Pep Gaurdiola. Xabi Alonso alikuwa kiungo mahiri klabuni hapo, na akawa anaendelea na mafunzo ya ukocha huku akiwa mchezaji. Kwa sasa Xabi Alonso ni kocha wa Bayer Leverkusen ya BundesLiga. Ameiongoza timu hiyo hadi nusu fainali ya Europa League ambako alitolewa na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho akiwa na kikosi cha AS Roma. Bayer Leverkusen imekuwa timu inayozidi kupaa zaidi kutokana na ufundi wa Xabi. Umahiri wake katika ukocha unatokana na mchango mkubwa aliopata kutoka kwa Pep Guardiola.
XAVI HERNDEZ
Barcelona ni mabingwa wa La Liga msimu huu. Wametwaa ubingwa huo wakiwa chini ya mwanafunzi wa zamani wa Pep Guardiola. Mwanafunzi huyu Xavi Hernandez alikuwa mhimili wa kikosi cha Pep Guardiola kilichokuwa na mafanikio makubwa La Liga na Barani. Xavi ameiinua Barcelona iliyokwua tia maji na kuifanya iwe imara licha ya matatizo ya kiuchumi. Ni wazi jicho la wapinzani linaona tena ufundi wa Guardiola katika ufundishaji wa Xavi Hernandez.
VINCENT KOMPANY
Alikuwa nahodha wa Manchester City. Katika mafanikio ya Man City yalikuwa na kila juhudi zake huku akiwa anafanya mafunzo ya ukocha. Tangu alipoondoka Man City na kurudi kwao, Kompany amekuwa akijihusisha na ukocha zaidi. Sasa msimu ujao atakuwa mmoja wa makocha waliopikwa na Pep Guardiola atakapokiongoza kikosi cha Burnley kwenye EPL. Burnley wameanza mazoezi ya msimu mpya mapema mwezi huu wa Juni na falsafa ya ufundishaji wake ni ileile inayotumiwa na Guardiola. Kitu cha kufurahisha Kompany anao mwongozo wake aliotumia wakati anatua Burnley ilipokuwa Ligi daraja la kwanza; anasajili wachezaji waliopo chini ya miaka 26 tu. Huyu ni zao lingine la Pep Guadriola. Ni dhahiri makocha wengi sasa wanatokana na kichwa cha Pep Guardiola akiwa amewajenga kifalsafa na mbinu na kuwavutia kupenda mtindo wa uchezaji wa timu zake.
Comments
Loading…