‘Mzunguko’ wa makocha waendelea
*Ancelotti amrithi Mourinho Real Madrid
Panga pangua ya makocha katika klabu kubwa za Ulaya imeendela, ambapo katika hatua ya karibuni kabisa, aliyekuwa Kocha wa Paris Saint-Germain, Carlo Ancelotti ametimkia Real Madrid.
Ancelotti anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mreno, Jose Mourinho aliyeondoka Bernabeu na kujiunga na Chelsea, alikopata kufanya kazi, kabla ya kukosana na mmiliki, Roman Abramovich.
Ancelotti aliwapatia PSG ubingwa msimu uliopita nchini Ufaransa, lakini aliomba aondoke, maana Real Madrid walishawasiliana naye na kutaka ajiunge nao, baada ya Mourinho kutofautiana nao.
Katika mfululizo huo, Laurent Blanc anachukua nafasi ya Mwitaliano huyo PSG. Mourinho alichukua nafasi ya Rafa Benitez aliyekuwa kocha wa muda Chelsea, ambaye amehamia Napoli ya Italia.
Ancelotti, 54, amesaini mkataba wa miaka mitatu wakati Mfaransa Blanc, 47, amesaini mkataba wa miaka miwili tu. PSG kwa muda mrefu wamekuwa wakimuwinda kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, lakini huwatolea nje, akisema bado ana kazi ya kufanya Arsenal, wanaofikiria kumwongezea mkataba wake utakapomalizika mwakani.
Blanc amepata kuchezea timu za Montpellier, Auxerre, Barcelona, Inter Milan na Manchester United wakati wa kipindi chake cha uchezaji, na alikuwa timu ya taifa ya Ufaransa iliyotwaa Kombe la Dunia 1998 na Euro 2000.
Akiwa kocha, Blanc aliwaongoza Bordeaux kutwaa ubingwa wa Ufaransa mwaka 2009, kabla ya kushika usukani wa timu ya taifa lake kati ya mwaka 2010 na 2012.
Sasa anaingia PSG inayotokea kuwa moja ya klabu kubwa Ulaya, baada ya kuchukuliwa na kampuni kubwa ya Falme za Kiarabu ya Qatar Sports Investments Agosti 2011.
Mabadiliko mengi ya ukocha ni Pep Guardiola aliyekuwa Barcelona kujiunga na Bayern Munich ya Ujerumani na nafasi yake ilichukuliwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita na Tito Vilanova ambaye anasumbuliwa na saratani ya koo.
Kocha wa Everton, David Moyes amechukua nafasi ya Alex Ferguson Manchester United aliyeng’atuka na kujiunga kwenye Bodi ya Wakurugenzi Old Trafford. Paolo Di canio amechukua nafasi ya Martin O’Neil Sunderland na alifanikiwa kuwaokoa kushuka daraja.
Comments
Loading…