in , , , ,

Mahrez mwanasoka bora wa mwaka

Riyad Mahrez


* Kombe la FA ni Man U na Crystal Palace

Mshambuliaji wa Leicester, Riyad Mahrez ametwaa taji ya mwanasoka bora
wa mwaka, huku timu yake wakiukaribia ubingwa wa England.

Mahrez (25) alitangazwa na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kutwaa
tuzo hiyo, akiwa amefunga mabao 17 na kutoa usaidizi kwa mengine 11
katika mechi 34 za Ligi Kuu ya England.

Mchezaji huyu wa kimataifa wa Algeria analizidishia Bara la Afrika
sifa kwa kutoa wachezaji mahiri, ama moja kwa moja wenye uraia wa
mataifa ya Afrika au wenye asili ya huko. Kura kwa ajili ya tuzo hiyo
hupigwa na wanasoka wa kulipwa.

Kiungo wa Tottenham Hotspur, Dele Alli, 20, alitajwa kutwaa Tuzo ya
PFA kwa Mwanasoka Mdogo. Mahrez alikuwa akikabiliwa na ushindani
kutoka kwa mshambuliaji wa Spurs, Harry Kane, kiungo wa Arsenal, Mesut
Ozil na yule wa West Ham, Dimitri Payet sambamba na wachezaji wa
Leicester, Jamie Vardy na N’Golo Kante.

Alikabidhiwa zawadi yake katika Hoteli ya Grosvenor jijini hapa, saa
chache tu baada ya kufunga kwenye mechi dhidi ya Swansea ambapo
waliibuka na ushindi wa 4-0. Wanatakiwa kupata pointi tano tu
kujihakikishia ubingwa.

Mahrez ameitoa tuzo hiyo kwa heshima ya wachezaji wenzake, akisema
kwamba bila wao hangeweza kufanya makubwa wala kuitwaa. Lakini pia
anasema ni kwa ajili ya kocha wake, Claudio Ranieri na wafanyakazi
wengine wa timu hiyo inayoushangaza ulimwengu kwa kasi yake ya ghafla.


KOMBE LA FA: MAN UNITED WATINGA FAINALI

Zaha
Zaha

Manchester United wametinga hatua ya fainali ya Kombe la FA, baada ya
kuwazidi nguvu Everton kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa wa
Wembley.

Alikuwa ni Mfaransa Anthony Martial aliyesajiliwa kiangazi kilichopita
aliyefunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi, na kukatiza ndoto
a kocha Roberto Martinez kuwapoza washabiki wanaotaka afurushwe kwa
kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu.

Matokeo hayo yamekuwa faraja kwa kocha Loui van Gaal wa Man United
aliye kwenye shinikizo la kufukuzwa pia, lakini inaelezwa kwamba
kutwaa kikombe hicho hakutabadili sana upepo, Jose Mourinho akipigiwa
upatu kuchukua mikoba yake.

Marouane Fellaini aliwafungia United bao la kwanza, ambao lazima
wamshukuru sana golikipa wao, David de Gea aliyeokoa kiustadi penati
ya mmoja wa washambuliaji wazuri na wenye nguvu, Romelu Lukaku katika
dakika ya 57.

Everton hawakuonesha moto na walizomewa wakati nusu ya kwanza
ilipomalizika, lakini dakika 15 kabla ya kipindi cha pili kumalizika
walisawazisha, pale mpira wa Gerard Deulofeu kumparaza Chris Smalling
na kutinga nyavuni.

Ilikuwa mechi iingie katika muda wa nyongeza, lakini Ander Herrera
alipata mpira na kuupeleka kwa Martial aliyetulia vyema kabla ya
kumshinda maarifa kipa wa Everton, Joel Robles.

Sasa United watakutana na Crystal Palace kwenye mtanange wa fainali
kwenye uwanja huo huo wa Wembley Mei 21. Palace walifanikiwa kuwazidi
nguvu Watford kwa mabao 2-1 kwenye nusu fainali nyingine.

Yannick Bolasie haliwafungia Palacekwa kichwa mapema dakika ya sita tu
baada ya Damien Delaney kushindwa kufagia ipasavyo mpira wa kona wa
Yohan Cabaye. Watford waliompoteza kiungo wao muhimu, Etienne Capoue
kwa kuumia kwenye mechi hiyo, walisawazisha kupitia kwa Troy Deeney
kutokana na kona ya Jose Manuel Jurado.

Haikuwa rahisi kwa Palace kushinda mechi hiyo, lakini vijana wa Alan
Pardew walipambana na kuhakikisha wanaipata nafasi ya fainali kwa mara
ya kwanza katika miaka 26 pale Connor Wickham alipoichukua vyema
majalo ya Pape Souare na kuutia mpira wavuni.

Fainali hiyo ya mwezi ujao ni marudio ya fainali ya 1990 pale Palace
waliooneshana kazi na United, wakaenda sare ya 3-3 kwenye mechi ya
mkondo wa kwanza kabla ya United kuja kushinda 1-0 kwenye mechi ya
marudiano. Siku hizi hakuna marudiano, bali ni dakika za nyongeza
kisha penati.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

AZAM YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO

Tanzania Sports

Leicester ‘shoka’ moja ubingwa