in , , ,

MAENEO MUHIMU KWENYE MECHI YA LIVERPOOL NA REAL MADRID

Fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya hii hapa, fainali hii itazikutanisha timu za Liverpool ya nchini England na timu ya Real Madrid kutokea nchini Hispania ambao ni mabingwa watetezi. Yafuatayo ni maeneo muhimu ya kuyaangalia katika mechi hii.

Ulevi wa timu hizi kwenye Ligi ya Mabingwa utatia ugumu wa mchezo?

Hapana shaka kwa sababu zinakutana timu ambazo ulevi wao mkubwa ni michuano hii ya Ulaya, damu huchemka na wehu uingia akilini mwa kila mchezaji wa timu hizi linapokuja suala la Ligi ya mabingwa barani ulaya. Real Madrid wanatafuta kombe lao la kumi na mbili (12) wakati Liverpool wakitafuta kombe lao la sita (6), hivo ugumu wa mechi hii unaanzia hapa kwa timu zote kuonekana kama ni timu ambazo huwa zinakuwa na hamasa kubwa ya kupigana zinapokuwa katika ligi ya mabingwa baraani Ulaya.

Hamasa kubwa ipo kwa Real Madrid ambao wanatafuta kuweka alama ya kukumbukwa kama timu iliyochukua kombe hili la ligi ya mabingwa Mara tatu mfululizo. Hii itawapa nguvu kupigana ili kuweka rekodi hii, na itasababisha ugumu wa mechi kwa sababu Liverpool watasimama kuhakikisha rekodi hii haiwekwi mbele yao.

Eneo la ulinzi la timu zote.

Mwanzoni mwa msimu Liverpool ilikuwa na mapungufu mengi sana katika eneo la kuzuia. Lakini usajili wa Van Djik umekuwa na msaada mkubwa kwa sababu hakuna makosa binafsi katika eneo hili la nyuma na amekuwa kiongozi mzuri katika eneo hili la nyuma la Liverpool, mpaka sasa hivi Liverpool wamepata clean sheets (6) katika michezo kumi na mbili (12) msimu huu wakati Real Madrid wamepata Clean sheets 3 katika michezo 12 ya ligi ya mabingwa msimu huu na wakifungwa magoli 12.

Kipi kinasababisha ionekane ukuta wa Real Madrid kuwa mbovu?
 
Sehemu kubwa ambayo Real Madrid huruhusu magoli ni sehemu ya beki wa kushoto anapocheza Marcelo. Muda mwingi Marcelo huonekana katika eneo la mpinzani kuliko katika eneo la kujilinda ndiyo maana magoli mengi hupitia kwake.

Eneo la kiungo kwa timu zote likoje?

Eneo hili limebeba watu ambao hawaangaliwi sana lakini ndiyo watu ambao wamebeba mipango ya timu zote mbili.

Casemiro, amekuwa akilinda mabeki wake vizuri na hii imekuwa ikiwapa nafasi Toni Kroos na Luka Modric kusogea mpaka eneo la mbele kutengeneza nafasi.

Wakati Liverpool wana James Milner ambaye amehusika katika utoaji wa pasi nyingi za mwisho wa magoli msimu huu wa Ligi ya mabingwa akiwa na pasi nane (8) za mwisho.

Kushuka kwa BBC na Kupanda kwa Utatu mtakatifu wa Liverpool.

Mpaka sasa Firmino, Salah na Mane wamefunga magoli 29, wakati Mara ya mwisho kwa Benzema, Bale na Ronaldo (BBC) kufunga magoli mengi kwenye michuano hii ya Ulaya ilikuwa msimu wa mwaka 2013/2014 walipofunga magoli 28 kwa pamoja.

Kipi kimesababisha kushuka kwa BBC?

Majeraha ya Mara kwa Mara ya Gareth Bale yamerudisha nyuma maendeleo ya BBC pamoja na kushuka kwa kiwango cha Karim Benzema ambaye msimu huu amekuwa na msimu wa kupanda na kushuka.

Wakati BBC wakishuka, Muunganiko wa Firmino, Salah na Mane umekuja katika sehemu kubwa na imekuwa muunganiko ambayo unatisha zaidi msimu huu.

Kuna nafasi ya Mohammed Salah kuwang’ara?

Nafasi ni kubwa sana. Kwanini? Moja ya sababu ambayo nimeielezea inayosababisha RealMadrid kufungwa ni eneo lao la kushoto kuwa dhaifu kwenye suala la kujilinda.

Hivo hii itampa nafasi Mohammed Salah kuwa huru eneo hili kwa sababu Marcelo atakuwa anatumia muda mwingi mwa mchezo katika eneo la mpinzani kuliko eneo lake.

Ronaldo ana nafasi kubwa ya yeye kung’ara pia?

Hapana shaka, kwa sababu moja ya silaha ambazo humfanya ang’are zitakuwepo. Silaha zenyewe ni Marcelo na Carvajal ambao wamekuwa ni chachu kubwa ya mashambulizi kwa Real Madrid. Kitu kingine kitakachompa nafasi kubwa ya yeye kupigana zaidi kwenye mechi hii ni kuweka rekodi ya mchezaji wa kwanza kuchukua kombe la ligi ya mabingwa mara tano, hii itamfanya apigane ili aweke alama ambayo itakuwa historia kwa dunia nzima.

Mchezo utaisha vipi?

Mchezo huu una nafasi kubwa ya kumalizika kwa magoli mengi ambayo timu zote zitafungana na hii ni kwa sababu ya mechi tatu zilizopita za timu hizi, mechi hizi zimeonesha timu hizi zinaweza kufungwa magoli kipindi ambapo presha kubwa inapokuwa kwao. Timu zote zinawachezaji ambao wanauwezo wa kutia presha ndiyo maana kuna nafasi kubwa ya mchezo huu kumalizika kwa magoli mengi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Tumemkaribisha Rais nyama inayotoka kwenye ng’ombe asiye na Afya

Tanzania Sports

Tatizo lilianza kwenye chozi la Salah