*watembelea Makao makuu ya PSPF
*wafanya mazungumzo na Mkurugenzi mkuu Bw Adam Mayingu
Mabosi wa Mabingwa wa Kombe la FA wa England, Arsenal, waliopo nchini kwa ziara ya kikazi wameanza kutikisa, ambapo kampuni nyingi zinataka ushirikiano na klabu hiyo.
Maofisa waliopo nchini ni pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo na Ushirikiano, Sam Stone na Meneja Maendeleo na Ushirikiano, Daniel Willey wanatarajiwa kukutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jumanne hii.
Tayari kampuni kubwa zaidi ya 20 zimetaka ushirika na Arsenal, na majadiliano ya kibiashara yanatarajiwa kuanza mara moja, kuona ni katika maeneo gani na kwa mfumo upi watashirikiana.
Katika ziara hiyo inayoratibiwa na Imani Kajula ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa EAG Group, benki mbalimbali zimetaka kufanya biashara na Arsenal, lakini pia Quality Group, kampuni inayomilikiwa na Rais wa Yanga, Yusuf Manji.
Stone amewaambia waandishi wa habari Jumatatu hii jijini Dar es Salaam kwamba wamejizatiti na japokuwa wamekuja kibiashara, milango ipo wazi iwapo kuna kampuni za michezo zinazotaka kushirikiana nao na kwamba zinaweza kunufaika.
Ujumbe huo umetua nchini huku hali ya hewa kisoka kwa klabu na timu ikiwa shwari, baada ya Arsenal kuwafunga Manchester City mabao 2-0 Jumapili hii kwenye Uwanja wa Etihad unaomilikiwa na mabingwa hao watetezi wa England.
Mabao ya Santi Cazorla na Olivier Giroud yakichanganywa na ulinzi mahiri wa kitimu, vilitosha kuzikonga nyoyo za washabiki wa Arsenal ndani na nje ya England, ambapo nchini Tanzania pia washabiki wao walionekana wakitamba mitaani, licha ya kwamba ilikuwa usiku.
Stone alisema jijini Dar Jumatatu kwamba wanaichukulia Tanzania kwa umuhimu mkubwa, kutokana na ukubwa wake kijiografia, mvuto wa watu wake kwenye soka na uwapo wa kampuni kubwa na zinazoweza kushirikiana na Arsenal.
Tayari Arsenal wana uhusiano na kampuni na taasisi nchini Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini na Nigeria.
Comments
Loading…