*Ilikuwa ni ofa ya kumnunua Sterling
*Man United wamtaka Romelu Lukaku
Liverpool, kwa mara nyingine wamekataa katakata kumuuza mshambuliaji wao wa kati, Raheem Sterling anayetakiwa na klabu kadhaa.
Liver wamekataa rasmi ofa ya pauni milioni 40 kwa ajili ya Mwingereza huyo aliyekwishakataa mkataba mpya Anfield ambao ungemfanya alipwe pauni 100,000 kwa wiki.
Sterling (20) pia anatakiwa na Arsenal na Real Madrid, ikidaiwa kwamba bei yake ya uhamisho huenda ikafika pauni milioni 50. Wiki iliyopita Liver walikataa ofa ya pauni milioni 25 na nyongeza nyingine kutoka kwa City.
Sterling aliyesema anataka kuchezea timu zinazotwaa makombe alijiunga na Liverpool akitoka QPR mwaka 2010 na mkataba wake unamalizika 2017.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers ameshasema anatarajia mchezaji huyo abaki Anfield hadi mwisho wa mkataba wake, lakini ikiwa hivyo ataondoka akiwa mchezaji hutu, hivyo Liver hawatatengeneza fedha yoyote kwake.
Man City sasa wanaandaa ofa kwa ajili ya kiungo wa Arsenal, Jack Wilshere, 23. Wanatarajia kutoa ofa ya awali ya pauni milioni 30.
Manchester United wameamua kumfuata mshambuliaji wa kati wa Everton na Ubelgiji, Romelu Lukaku, 22, baada ya kuonekana dalili za kumkosa yule wa Atletico Madrid, Mario Mandzukic, 29.
Wakati huo huo, United wametuma barua kuwauliza Real Madrid juu ya uwezekano wa kumsajili beki wao wa kati, Raphael Varane, 22. Walitoa maombi hayo wakati wakijadiliana juu ya uhamisho wa kipa David De Gea kwenda Madrid lakini Real wamesema beki huyo hauzwi.
Kocha wa Man United anafikiria kutoa ofa ya pauni milioni 10.2 kwa ajili ya kumpata beki wa pembeni wa Monaco, Fabinho.
Juventus wapo katika mazungumzo na Chelsea juu ya uwezekano wa kumsajili kiungo wa Brazil, Oscar, 23, kwa pauni milioni 18.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Manchester City, Carlos Tevez, 31, amewaambia Juventus angependa kurudi Argentina kuchezea Boca Juniors.
Juventus wanaonekana kujiandaa vyema kukabili pengo hilo kwa kufanya mazungumzo na Atletico Madrid kwa ajili ya kumsajili Mario Mandzukic, 29.
Tottenham wametuma ofa kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Newcastle Yohan Cabaye, 29, aliye kwa mkopo Paris St-Germain.
Galatasaray wameingia kwenye mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie, 31 na yule wa Schalke, Klaas-Jan Huntelaar, 31.
Hata hivyo, Galatasaray hawatamudu kumlipa Van Persie mshahara wa £240,000 kwa wiki anaopata sasa Old Trafford, hivyo huenda itabidi akubali punguzo la mshahara au abaki United kwa mwaka wake wa mwisho.
Chelsea wanaelekea kumuuza kipa wao mkongwe, Petr Cech, 33, kwa wapinzani wao, Arsenal kutokana na matakwa ya raia huyo wa Jamhuri ya Czech. Jose Mourinho atamgeukia kipa wa QPR na England, Rob Green, 35, ili kusaidiana na kipa namba moja, Thibaut Courtois.
Southampton wamesema kwamba kiungo wao, Morgan Schneiderlin, 25 anayetakiwa na Manchester United na Arsenal ana thamani ya pauni milioni 24.