*Wakishinda mechi zilizobaki ni mabingwa
Liverpool wameonesha dhamira yao ya kutwaa ubingwa wa England baada ya kukwea kileleni kwa kuwafyatua Tottenham Hotspur 4-0 kwenye dimba la Anfield.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alisema kwamba sasa kikosi chake kinaweza kuhimili misukosuko ya kulitafuta taji hilo wakati mwenzake wa Spurs, Tim Sherwood amekalia kuti kavu.
“Bado kuna pointi nyingi za kutafuta na nyingine hazitapatikana kw atimu zote kabla ya msimu kuisha, hata hivyo hatuhisi shinikizo lolote japokuwa naona walio kwenye nafasi nzuri ya kuwa mabingwa ni Manchester City,” anasema Rodgers.
Spurs walianza mchezo hovyo, huku beki Younes Kaboul akijifunga dakika ya pili tu ya mchezo, kabla ya Luis Suarez, Philippe Coutinho na Jordan Henderson kupachika mabao yao na kuwapatia Reds ushindi wa nane mfululizo katika ligi kuu.
Everton waliokabwa vilivyo na Fulham jijini London walipata ushindi baadaye sana wa mabao 3-1 na kujiweka nafasi nzuri ya kutafuta nafasi ya nne, na Jumapili ijayo wanawakaribisha Arsenal kwenye dimba lao la Goodison Park.
Liverpool sasa wamefikisha pointi 71 baada ya michezo 32 wakiwazidi Chelsea kwa pointi mbili na Man City kwa pointi tatu lakini Man City wana mechi mbili mkononi.
Bado kuna mechi zinakuja Anfield baina ya Liverpool na City na pia Liverpool na Chelsea, kwa hiyo hatima ya ubingwa kwa Liverpool ipo mikononi mwao wenyewe na watatakiwa kushinda mechi zote walizobakisha..
Arsenal wanashika nafasi ya nne kwa poini 64 wakifuatiwa na Everton wenye pointi 60 lakini Everton wana mchezo mmoja mkononi. Spurs wapo nafasi ya sita wakati Manchester United wamekuwa kama wamelogewa kwenye nafasi ya saba kwani ni muda mrefu wamebaki hapo, washinde, wafungwe au watoke sare. Wana pointi 54 tu.
Mkiani mwa msimamo wa ligi wapo Fulham wenye pointi 24 licha ya kupewa wachezaji wengi wazuri kwa mkopo Januari mwaka huu. Sunderland wana pointi 25 na Cardiff wamefikisha pointi 26. Hata hivyo Sunderland wana mechi mbili mkononi.
Comments
Loading…