Mabingwa wapya wa England – Liverpool wanasema kwamba kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa England (EPL) si kwamba wamefikia kilele cha mafanikio, bali ndio kwanza linawapa njaa kubwa ya kupigania ubingwa zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Liverpool, Tom Werner, anasema kwamba baada ya ‘mali iliyopota’ miaka 30 iliyopita kupatikana wiki jana, yaani kombe hilo, sasa wanajawa hasira na kuwa kama simba aliyeonja nyama na ikawa kama inataka kumponyoka.
Akizungumza kutoka nyumbani mwake, Cape Cod, Massachusetts, bosi huyo alionekana akiwa amenyanyua juu bilauri ya mvinyo, huku ujumbe ukisambaa kutoka kwake kwenda kwa wakurugenzi wenzake na kutoka kwao kwenda kwake. Wakurugenzi na wamiliki wenza wake ni John W Henry na Mike Gordon.
Hayo yalianza tangu pale Liverpool walipojihakikishia ubingwa wakiwa wametulizana, baada ya Chelsea kuwanyoa mabingwa watetezi, Manchester City 2-1 Alhamisi ya wiki jana. Kipenga cha mwisho kilipopulizwa pale Stamford Bridge na kusubiri kwa miaka 30 kwa Liverpool kutwaa ubingwa kumalizika, prodyuza huyo wa televisheni na mfanyabiashara mkubwa alinyanyua simu yake.
Alifanya hivyo ili kumshukuru yule aliyeonekana kuwa nyuma ya mafanikio hayo makubwa, na si mwingine bali Kocha Mjerumani Jurgen Klopp aliyekijenga kikosi kwa miaka takriban mtano, akikiimarisha mwaka hata mwaka bila kuogopa kufukuzwa, hadi akatwaa ubingwa wenyewe baada ya kitisho cha EPL msimu huu kufutwa kwa sababu ya virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
“Nilituma ujumbe kwa Jurgen (Klopp) mara baada ya mechi kumalizika, naye akanitumia salamu tamu kabisa. Nilitaka tu kukushukuru. Nilitaka kuonesha shukurani za dhati toka moyoni mwangu kwa kazi yake ngumu na kujitolea kwake kwa hali ya juu. Nilitaka kuonesha nilivyoguswa na kujituma kwake kwa ajili ya klabu. Ni mtu wa kipekee kabisa, naona heshima kwamba ni kiongozi wetu,” Werner ananukuliwa akisema.
Anaongeza kwamba Klopp ni mtu ambaye hupenda sana kutuma ‘emoji’, na kwamba katika majibu yake zilikuwapo kadhaa. Anasema kati ya hizo alizomtumia wakati akijibu chat yake ni ile ya moyo.
Kutokana na janga la Covid-19, ilimaanisha kwamba wamiliki hao wa Liverpool walikuwa umbali wa maili 3,000 kutoka kwenye eneo ambalo sherehe za kutwaa ubingwa zilikuwa zikifanyika – Formby Hall Golf Resort and Spa, Liverpool. Hafla iliendelea hadi saa za mapema za Ijumaa, Klopp akionesha umahiri wake wa kusakata dansi.
Kusafiri kwa kukatiza kwa anga juu ya Bahari ya Atlantiki haikuwa moja ya mawazo ya wamiliki wala klabu na wadau wengine, ikizingatiwa kanuni za karantini na kujitenga ambazo bado zinafuatwa sehemu mbalimbali duniani.
Umbali huo, hata hivyo, kwa upande mwingine uliamsha hisia kali lakini za furaha na fahari kwao; kwamba mfupa uliokuwa umewashinda wengi kabla, sasa ulikuwa umetafunwa na kumezwa barabara.
“Tungependa sana kuwa Liverpool wakati huu war aha na fahari kubwa, lakini haikuwezekana na lazima tusubiri hadi serikali itoe kibalio cha kusafiri. Virusi vinadhibiti hilo. John, Mike na mie tumekuwa makini sana juu ya haja ya kujitenga lakini katika muda fulani hvi karibuni tunadhani tutaweza kuwa pamoja. Tulikuwa tuklijadiliana kwa simu karibu muda wote wa jioni ya Alhamisi, tukitumiana meseji,” Mwenyekiti Werner anasema.
Mmiliki mwenza huyo anasema kwamba japokuwa siku yenyewe ya ubingwa imepita, hadhani kwamba manjonjo yake yamekwenda nayo na kwamba klichopita ni tarehe ambayo ni ya siku muhimu kihistoria kwa klabu na washabiki aliosema anafurahishwa na uvumilivu wao, uungaji mkono wao kwa wachezaji na uaminifu katika kipindi chote cha miaka 30 ya kusubiri kumrejesha ‘mwali’ ndani.
“Katika miaka 20 ijayo, washabiki hawatakumbuka nyakati ngumu za Covid-19 na msimu wa 2019/2020. Watakumbuka tu kwamba Liverpool walitwaa ubingwa na watakumbuka kwamba tulistahili kushinda kikombe hicho.
“Nilipotazama mechi dhidi ya Crystal Palace usiku mwingine, nilivutiwa na kufurahishwa na vipaji vya wachezaji wengi tofauti. Michango ya Mohamed Salah na Sadio Mane, mpira ule wa adhabu ndogo wa Trent Alexander-Arnold na bao la Fabinho.
“Ilionekana kana kwamba wachezaji hawa hawangeweza kukataliwa. Kutwaa kombe hili huku kukiwa na mechi saba bado kuchezwa, inamanisha kwamba tumetawala hasa. Tunakaribia kufikisha kipindi cha misimu mitatu bila kupoteza mechi ya ligi nyumbani. Kama ningekuambia Julai mwaka jana pale Fenway Park in Boston nilikokuwa – kwamba wakati huu muhimu ungetokea sie kuwa mabingwa kwa tofauti kubwa jinsi hii ya alama ungedhani kwamba sikuwa na akili timamu. Ni mafanikio ya kwanza, pongezi kwa Jurgen na timu,” anasema huku akifurahia.
Ilikuwa kama ndoto Oktoba 2010 pale FSG (wakati ule wakiitwa New England Sports Ventures) walipokamilisha ununuzi wa klabu ya Liverpool kwa pauni milioni 300. Klabu ilikuwa katika hali mbaya mno – ndani na nje ya uwanja. Kulikuwapo madeni makubwa na mgawanyiko baina ya wamiliki wa awali – Tom Hicks na George Gillett waliofikia kutoelewana kwa hali ya juu.
Kwenye Jukwaa la Kop, kuna bango lililoandikwa ‘Unity Is Strength’, lakini Liverpool wana wimbo maarufu waliouzoea mno wa ‘You Will Never Walk Alone’. Moja ya viwango vya juu vya Klopp kinaweza kuoneshwa katika ukweli kwamba anaamini kombe si lake mwenyewe na wachezaji, bali pamoja na wafanyakazi wote wa klabu hiyo.
Klopp alipokea ubingwa kwa furaha kubwa, akiwashukuru wachezaji na wafanyakazi wote kwa mchango wao. Vijana wake walicheza soka ya aina yake, wakienda mechi 18 wakishinda zote na mechi 44 bila kupoteza mchezo.
Liverpool wametenga pauni milioni 60 kwa ajili ya kukarabati na kuongeza nafasi kwa washabiki kwenye jukwaa la Anfield Road, ikimaanisha baada ya kukamilika wataingia watazamani takriban 61,000. Kazi hiyo imecheleweshwa kwa miezi 12 kutokana na Covid-19.