Safari ya miaka 28, ni safari ndefu sana. Na inawezekana ilikuwa safari ambayo ilikuwa na masimango mengi ndani yake.
Safari ambayo ilizalisha njaa kubwa sana kwa mashabiki , viongozi na wachezaji wa Liverpool. Njaa ya miaka 28!.
Njaa ambayo ilionekana inaweza ikakomeshwa mwaka 2014. Brendan Rogders aliwapa imani kubwa Liverpool kuwa wanaweza wakabeba ubingwa wa ligi kuu ya England.
Na inawezekana isingekuwa makosa binafsi ya Steven Gerald kumfanya Demba Ba kufunga goli lilioua ndoto yake na ndoto ya wana Liverpool, basi Liverpool wangechukua.
Lakini habari ilikuwa tofauti kabisa na mategemeo ya waliowengi. Manchester City alichukua ubingwa mbele yao.
Ikawa mwisho wa matumaini ya Liverpool. Hawakuweza tena kuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda kikombe hiki cha ligi kuu ya England.
Baada ya kuondoka kwa Luiz Suarez, Liverpool ilibaki uchi rasmi. Ikaonesha wazi kuwa hii ilikuwa Liverpool ya Luiz Suarez.
Haikuwa na uwezo tena wa kupigania kuwa bingwa, imepita miaka minne tangu Liverpool kuonekana wanauwezo wa kubeba ligi kuu ya England.
Leo hii tena kwa mara pili ndani ya miaka 28 Liverpool inaonekana inauwezo mkubwa wa kubeba ligi kuu ya England.
Tena kipindi hiki iko tofauti kabisa na kipindi cha Brendan Rodgers. Kipindi cha Brendan Rogders ilimaliza msimu ikiwa imeruhusu magoli 50.
Kipindi hiki ni tofauti sana , mpaka sasa vijana wa Jurgen Klopp wameruhusu magoli 8 tu mpaka sasa hivi.
Timu bingwa ni yenye safu imara ya ulinzi. Hiki kitu Jurgen Klopp alikiona. Aliamua kukifanyia kazi ipasavyo.
Alimaliza pesa nyingi kumleta Van Djik kwa gharama kubwa. Gharama ambayo kila mtu alishangaa. Ilikuwa ni nadra sana kwa beki kununuliwa kwa bei ya mshambuliaji.
Hiki ndicho alichokifanya Jurgen Klopp, alikuwa anajua kipi alichokuwa anakifanya, ndiyo maana alinyamaza kimya.
Hakusita tena kwenda sokoni na kumchukua golikipa kwa bei ya mshambuliaji. Soko lilimshangaa na yeye akawashangaza ndani ya uwanja.
Van Djik na Allison wamekuwa chachu ya Liverpool mpaka sasa hivi kufikia hii hatua ambayo wengi wanaona kuna mwangaza mbele ya macho yao.
Nuru inaonekana tena kwenye uwanja wa Anfield baada ya miaka 28 ya kuishi ndani ya Giza. Kipindi hiki wanamatumaini makubwa sana ya kushinda.
Timu yao inauwiano mzuri sana uwanjani tofauti na kipindi chochote ndani ya miaka 28 ya mateso yao. Magoli yanayofungwa na kina Salah hulindwa vizuri na kina Allison.
Maana halisi ya timu imara nà bora inaonekana kwa sasa ndani ya kikosi cha Jurgen Klopp. Na inawezekana akawa shujaa mkubwa ambaye atakumbumwa na vizazi vingi vya Liverpool.