*De Gea na Sterling warudi klabuni kwao lakini …
*Arsenal sasa wawageukia Pedro na Arturo Vidal
Liverpool wameendeleza kasi zao za usajili kama ilivyokuwa kiangazi kilichopita na lengo likionekana ni lile lile la kuziba pengo la mshambuliaji wao wa kati waliyemuuza Barcelona, Luis Suarez.
Kocha Brendan Rodgers bado hajapata ufumbuzi wa safu ya ushambuliaji licha ya kusajili kadhaa tangu mwaka jana. Hivi sasa klabu imeamua kutoa dau hata kama ni pauni milioni 32.5 zilizo kwenye kifungu cha mkataba wa Christian Benteke na klabu yake ya Aston Villa.
Kocha Brendan Rodgers anayelekea kusalimika kufutwa kazi kwa kufanya vibaya msimu uliopita, anatarajia kuwasilisha ofa mezani kwa Villa kwa ajili ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 24.
Hadi wiki iliyopita, Rodgers alikuwa amefikisha idadi ya wachezaji wapya sita aliosajili alipomwingiza Anfield beki wa kulia wa Southampton na England, Nathaniel Clyne. Anayefuatia anaelezwa kuwa ni Benteke aliyefunga mabao 49 katika mechi 101 tangu atue Villa Park kutoka Genk kwa pauni milioni saba miaka mitatu iliyopita.
Tangu ang’are amekuwa akitakiwa na Arsenal, Tottenham Hotspur na Liverpool licha ya nyakati fulani kuwa nje kutokana na majeraha. Inadaiwa kwamba angependelea zaidi kujiunga na Liverpool klabu yake ikimruhusu.
Wakifanikiwa kumsajili kwa kima hicho, Liverpool watakuwa wametumia pauni milioni 80 kiangazi hiki pekee. Wengine waliosajiliwa ni Roberto Firmino, James Milner, Danny Ings, Joe Gomez na Adam Bogdan.
Mchezaji wa Liverpool aliyeachwa baada ya mkataba wake kumalizika, Mwingereza Glen Johnson yupo kwenye mazungumzo na West Ham juu ya kujiunga nao kwa ajili ya kazi ya beki ya pembeni.
Mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling anatarajiwa kurejea Anfield kwa ajili ya mazoezi kabla ya kuanza msimu mpya lakini kuna hati hati iwapo atasafiri na klabu kwenda Bangkok.
Sterling, 20, anatakiwa na klabu kadhaa, wakiwamo Manchester City walio tayari kuongeza dau lakini Liverpool wamekuwa wakisisitiza kwamba hauzwi. Amekataa kuongeza mkataba na klabu hiyo japokuwa alipewa ofa ya mshahara wa pauni 100,000 kwa mwezi. Man City wanatafakari kutoa pauni milioni 50 wanazotaka Liver.
Kipa Mhispania wa Manchester United, David De Gea, 24, amerejea England kwa ajili ya mazoezi ya kabla ya msimu licha ya ripoti kueleza kwamba atajiunga na Real Madrid msimu ujao.
Kocha Louis van Gaal ametunisha misuli kumzuia kuondoka hadi hapo Madrid watakapokubali dili la kumwachia mlinzi Sergio Ramos atinge Old Trafford. Hata hivyo, De Gea alishawaambia wenzake kwamba msimu ujao atakuwa Madrid.
Na kutokana na utata huo, tayari Manchester United wanafikiria kupeleka ofa kwa Stoke ili kumpata kipa wao, Asmir Begovic anayetakiwa pia na Chelsea kwa ajili ya kuziba pengo la Petr Cech aliyehamia kwa mahasimu wao, Arsenal.
Washika Bunduki hao wa London wametuma ulizo juu ya uwezekano wa kumpata winga wa kimataifa wa Hispania na Barcelona, Pedro ambaye msimu uliopita amecheza mechi 35, lakini kati ya hizo 20 akitokea benchi kutokana na kuwa nyuma ya ‘mapacha watatu’, Lionel Messi, Neymar na Luis Suarez.
Pedro, 27, ambaye hajapata kuchezea klabu nyingine zaidi ya Barca, amechezea Timu ya Taifa ya Hispania mechi 51. Liverpool pia wanaelezwa kumtaka mchezaji huyu aliyetwaa Kombe la Dunia 2010 na lile la Ulaya 2012.
Mkataba wake unataka pauni milioni 110 ili aondoke kabla ya 2019 lakini hilo linazungumzika, ndiyo maana Arsenal wameanza mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo.
Arsenal pia wanaelezwa kwamba wataendelea na mipango ya kumsajili kiungo wa Juventus na Chile, Arturo Vidal, 28, baada ya Juve kutia nia ya kumuuza kwa dau kubwa na kutafuta mchezaji wa bei ya chini kidogo ili wabakiwe na kitita cha kazi nyingine kutoka Arsenal.
Southampton wanatarajia kukamilisha usajili wa mlinzi wa Ubelgiji, Toby Alderweireld, 26, ambaye msimu uliopita alicheza hapo kutoka Atletico Madrid huku kukiwa na kifungu cha kuwaruhusu kumnunua kwa pauni milioni 6.8 tu. Inadaiwa Atletico walikuja kufuta kifungu hicho, lakini kisheria wanabanwa bado.
Tottenham Hotspur wanadaiwa kukubaliana na Atletico Madrid juu ya kumnunua mchezaji huyo kwa pauni milioni 11.5. Saints wanajiandaa kufungua kesi kupinga kupokwa mchezaji wanayeona ni haki yao.