Baada ya mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea kutimua vumbi wikiendi hii kwenye viwanja mbalimbali huku macho na masikio ya karibu kila mshabiki wa soka Tanzania yakielekezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam ambapo Yanga watakuwa wakimenyana na Azam FC siku ya Jumamosi.
Mchezo huo utakuwa wa upinzani mkubwa na wenye kusisimua kwa kuwa utazihusisha timu mbili za juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara huku kila moja ikiwa na rekodi ya kushinda michezo yake yote mitano ya mwanzo hivyo kujikusanyia jumla ya alama zote 15.
Yanga waliwafunga Coastal Union, Tanzania Prisons, JKT Ruvu, Simba na kisha Mtibwa Sugar. Azam walipata ushindi kwenye michezo yao dhidi ya Tanzania Prisons, Stand United, Mwadui FC, Mbeya City halafu Coastal Union.
Tofauti ya mabao ndiyo inayowaweka Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa wamefunga jumla ya mabao 13 na kuruhusu bao moja pekee ambalo lilifungwa na Michael Aidan wa JKT Ruvu kwenye mchezo wa mzunguko wa tatu. Azam walio kwenye nafasi ya pili wamefunga mabao 9 na kufungwa mabao mawili mbaka sasa.
Itakumbukwa timu hizi zilipokutana kwenye michezo miwili ya mwisho hakuna iliyofanikiwa kuona lango la mwenzie. Mwezi Julai zilikutana kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Kagame ambapo dakika tisini zilimalizika kwa sare ya bila mabao na Azam wakaibuka na ushindi kwa mikwaju ya penati na kutinga hatua ya nusu fainali.
Mwezi Agosti ni Yanga waliopata ushindi dhidi ya Azam kwa mikwaju ya penati vilevile kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana kwa mara nyingine. Pengine uhaba huu wa mabao kwenye michezo baina ya timu hizi unakwenda kuisha Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwenye viwanja vingine, Simba watakuwa wageni wa Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Wekundu hao wa Msimbazi ambao wapo kwenye nafasi ya 3 wakiwa na alama 12 wanahitaji kujikusanyia alama tatu kwenye mchezo huo ili matokeo yoyote ya mchezo baina ya Yanga na Azam yaweze kuwa na manufaa upande wao.
Michezo mingine ya Jumamosi itakuwa kati ya Majimaji dhidi ya African Sports huko Songea, Ndanda FC watacheza na Toto Africans ndani ya dimba la Nangwanda Sijaona, Mtwara, Stand United wataikaribisha Tanzania Prisons kwenye dimba la Kambarage jijini Shinyanga na Coastal Union watawaalika Mtibwa Sugar kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga.
Jumapili kutakuwa na michezo miwili, mmoja utakuwa kati ya Mgambo Shooting na Kagera Sugar utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani na mwingine utazihusisha Mwadui na JKT Ruvu kwenye dimba la Mwadui Complex huko Shinyanga.