in , , ,

Ligi Bora ya Tanzania Imetupeleka AFCON

Tanzania imefuzu fainali za michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo itafanyika mwakani nchini Morocco, nilikuwepo uwanjani na nimefurahishwa na namna ambavyo watanzania walijitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu ya Taifa pamoja na jinsi ambavyo walikua wakiwahamasisha wachezaji uwanjani waendelee kupambana.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) imekuwa mojawapo ya ligi zinazozidi kukua kwa kasi barani Afrika, ikiwa ni daraja muhimu linalounganisha ndoto za wachezaji wa Kitanzania na mafanikio ya kimataifa. Katika mafanikio haya, hatuwezi kupuuza mchango wa ligi hii katika kufanikisha safari ya Taifa Stars kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka ujao wa 2025 pale nchini Morocco. Mafanikio haya yanaakisi mambo mengi mazuri yanayoendelea katika mfumo wa ligi, wachezaji, walimu, usimamizi, na mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Moja ya mambo ambayo naweza kusema tunapaswa kujivunia kama Taifa ni mchango mkubwa wa Ligi Kuu ambayo ni bora inayopelekea kuwa na wachezaji wengi wa ndani wanaoimarika kila msimu. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo wachezaji wa kigeni walihodhi nafasi nyingi muhimu katika klabu, hivi sasa wachezaji wa Kitanzania wanapata nafasi kubwa ya kuonesha uwezo wao na hapa huwezi kuacha kuwataja wachezaji kama Feisal Salum , Mudathir Yahya , Shomari Kapombe na wengine wengi ambao wamekua na kiwango bora kila siku ambao mchango wao katika klabu zao umewezesha timu ya taifa kuwa na kikosi imara.

Ukuaji wa wachezaji wa ndani unachangiwa na uwekezaji pia katika klabu zetu ambazo zinashiriki ligi kuu ya Tanzania pamoja na mikakati imara ya kuhakikisha kuwa tunakua programu za kukuza vipaji na hapa ndipo ambapo unakuta Ligi Kuu ya Vijana kuanzia chini ya miaka 17 na ile ya chini ya miaka 20.

Katika miaka ya karibuni, walimu wazawa wa Kitanzania wamepata nafasi ya kuonyesha uwezo wao wa kufundisha timu kubwa. Mfano halisi ni Juma Mgunda, ambaye ameweza kufundisha vilabu vikubwa kama Simba Sc na sasa yuko Namungo huku bado akifanya majukumu yake kwenye benchi pia la timu ya taifa ya Tanzania.

Niseme tu kuwa uwepo wa walimu wazawa katika benchi la ufundi umechangia si tu kuboresha viwango vya vilabu bali pia kuinua soka la kitaifa kwa kutengeneza wachezaji wenye nidhamu, mbinu bora, na uwezo wa kushindana kimataifa kwani walimu wazawa wanaelewa vyema utamaduni, changamoto, na malengo ya wachezaji wa Kitanzania. Tofauti na walimu wa kigeni ambao mara nyingine wanahitaji muda mrefu kuzoea mazingira, walimu wa ndani wameonyesha uwezo wa kuchukua nafasi kubwa katika maendeleo ya ligi na Taifa Stars.

Usimamizi wa Ligi Kuu ya Tanzania umeimarika sana, ukiongozwa na Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kupitia usimamizi thabiti, ligi imevutia wadhamini wakubwa kama Azam Media, NBC, na CRDB ambao mchango wao wa kifedha umeimarisha klabu na ligi kwa ujumla. Pesa zinazopatikana kupitia udhamini na mapato ya matangazo zimewekezwa katika miundombinu, usajili wa wachezaji bora, na maendeleo ya ligi.

Aidha, usajili wa wachezaji wa kigeni umeimarishwa, ambapo sasa wachezaji wa nje wanaosajiliwa wanatakiwa kuwa na viwango vya juu ili kuchangia ubora wa ligi.

Safari ya kufuzu AFCON haikamiliki bila mchango wa Watanzania wote, kuanzia mashabiki hadi viongozi wa soka. Watanzania wameonyesha mshikamano mkubwa, wakijitokeza kwa wingi kuunga mkono Taifa Stars katika mechi za kufuzu. Sauti zao viwanjani, kuanzia Benjamin Mkapa hadi uwanja wa ugenini, zimekuwa chanzo cha hamasa kubwa kwa wachezaji.

Mashabiki wa soka Tanzania wana nafasi kubwa katika maendeleo ya mchezo huu. Kujaa kwa viwanja, hasa wakati wa mechi muhimu, si tu kunaleta mapato kwa vilabu na TFF bali pia kunawaweka wachezaji katika mazingira ya ushindani yanayofanana na yale ya kimataifa. Hamasa ya mashabiki imekuwa chachu kubwa ya kuongeza viwango vya wachezaji, huku wakitambua kuwa wanawakilisha nchi nzima.

Kufuzu kwa Taifa Stars kwa mara nyingine kunatoa nafasi kwa Watanzania kutafakari mchango wao kwa soka. Wengi wameanza kutambua kuwa mafanikio haya si juhudi za wachezaji pekee, bali ni matokeo ya ushirikiano wa wadau wote. Vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu vina jukumu la kutoa wachezaji bora, mashabiki wana jukumu la kutoa hamasa, na viongozi wa soka wana jukumu la kuandaa mazingira bora.

Ni wazi kuwa sasa Watanzania wameanza kutambua kuwa mafanikio ya Taifa Stars ni ya kila mmoja. Hii imejidhihirisha kwa jinsi walivyoshirikiana kusherehekea ushindi wa Taifa Stars dhidi ya timu kubwa kama Guinea katika mchezo ambao ulikua ni lazima kwa Tanzania kushinda ili kufuzu AFCON. Umuhimu wa mshikamano huu ni wa kihistoria, na ni ishara ya nia ya Watanzania kuinua soka la kitaifa.

Huu ni wakati wa Watanzania wote kushirikiana kwa pamoja kuendeleza mafanikio haya. Kupitia ligi yetu bora, tunaweza kuota ndoto kubwa zaidi – kuona Taifa Stars si tu ikishiriki AFCON bali pia ikishinda taji hilo siku moja. Hili linawezekana ikiwa kila mmoja atatambua umuhimu wake katika maendeleo ya soka.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Taifa Stars

Hongera Tanzania Kufuzu AFCON, Mko Vizuri Sana

Ukuta wa Simba utaamua ubingwa msimu huu

Umaarufu au Ubora wa Ligi Kuu Tanzania?