*Diego Costa ashitakiwa*
Leicester wametanua pengo baina yao na wengine wanaosaka ubingwa wa
England, kwa kuwafunga Newcastle wenye kocha mpya, Rafa Benitez.
Vijana hao wa Claudio Ranieri sasa wamefikisha pointi 63 katika mechi 30.
Hizo ni pointi tano zaidi ya Tottenham Hotspur, 11 zadu ya Arsenal na
12 zaidi ya Manchester City.
Lilikuwa ni bao zuri la Shinji Okazaki lililowapatia The Foxes
ushindi, huku wakiwa wamebakisha mechi nane tu. Wao na Spurs wamecheza
mechi moja zaidi ya Arsenal na Man City hata hivyo.
Newcastle walibadilika na kuwa wazuri kuliko siku zilizopita, ambapo
nusura wapate mabao kupitia kwa Ayoze Perez na Moussa Sissoko.
Kwa kufungwa huko, Newcastle wapo nafasi moja tu kutoka mkiani mwa
ligi, lakini Benitez amesema kwamba ana imani watafanikiwa kubaki Ligi
Kuu ya England (EPL).
Kabla ya mechi hiyo, Ranieri βThe Tinkermanβ alikataa kwamba vijana
wake ndio wanaopewa nafasi zaidi ya kutwaa ubingwa wa England.
Hata hivyo, wakati mechi ikiendelea, Mtaliano huyo aliwageukia
washabiki wa nyumbani katika King Power Stadium akiwataka waongeze
sauti na kushangilia kwa nguvu, wakati huu wanapokaribia kufuzu kwa
mashindano makubwa ya soka Ulaya.
Pamoja na Newcastle, wengine walio katika hatari ya kushuka daraja ni
Aston Villa wenye pointi 16, Norwich na Sunderland wenye pointi 25
kila mmoja.
DIEGO COSTA ASHITAKIWA
Mshambuliaji wa kati wa Chelsea, Diego Costa ameshitakiwa rasmi kwa
kosa la utovu wa nidhamu kwenye mechi dhidi ya Everton.
Katika mechi hiyo ya Kombe la FA ambapo Chelsea walitupwa nje kwa
kufungwa 2-0, Costa (27) alipewa kadi nyekundu, baada ya kuonekana
kumngβata Gareth Barry.
Mhispania huyo alitolewa nje katika dakika ya 84 kwenye dimba la
Goodison Park, ambapo Chelsea walifungwa na mchezaji wao wa zamani
waliyemkataa, Romelu Lukaku.
Chama cha Soka (FA) kimeamua kumshitaki Costa kwa tabia yake, ambapo
amekuwa akilaumiwa mara kwa mara kwa anavyowachezea rafu na kuwatukana
wachezaji wa timu pinzani, ambapo mara nyingi waamuzi huwa hawaoni
wala kumuadhibu.
Costa anatakiwa hadi Alhamisi ya Machi 17 mwaka huu awe amejibu
mashitaka yake. Amepewa pia hadi Jumatano hiii kuwasilisha kwa FA
maelezo juu ya ishara mbaya aliyowatolea washabiki wa Everton wakati
akitoka nje muda wa mapumziko.