in , ,

LA LIGA WIKIENDI HII

 

 

*Atletico na kibarua cha Eibar

*Barca kuwatembelea Levante dhaifu

*Real Madrid dhidi ya Granada

 

La Liga itaendelea kutimua vumbi wikiendi hii ambapo michezo kadhaa itapigwa katika viwanja tofauti. Ni michezo ya raundi ya 23 ambapo mabingwa watetezi Barcelona wanaongoza jedwali la ligi hiyo wakiwa na alama 51 (wana mchezo mkononi) mbele ya Atletico Madrid wenye alama 48.

Real Madrid wao wanashika nafasi ya 3 wakiwa na alama 47. Kwenye makala hii tunatazama michezo tofauti ya wikiendi hii inayozihusisha timu hizo tatu za juu zinazotazamiwa kuendelea kupambana vikali kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Atletico Madrid ambao wikiendi iliyopita walikutana na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Barcelona watakuwa nyumbani kesho Jumamosi kukipiga dhidi ya Eibar wanaoshika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.

Mchezo huu hauwezi kuwa rahisi kwa Atletico kwa namna yoyote ile. Vijana hao wa Diego Simeone ambao hawakushinda mchezo wowote kati ya michezo minne iliyopita (kwenye mashindano yote) watarajie upinzani mkali kutoka kwa Eibar.

Hii inatokana zaidi na Atletico kulazimika kuwakosa nyota muhimu wa kikosi cha kwanza kama walinzi Juanfran, Diego Godin na Filipe Luiz wanaotumikia adhabu ya kadi nyekundu. Wengine ni viungo Tiago Mendez na Augusto ambao ni majeruhi.

Ingawa Eibar wamepoteza michezo mitatu kati ya minne iliyopita lakini ikumbukwe vijana hao kutoka jijini Basque wamefunga magoli manne kwenye michezo miwili ya mwisho ya ugenini.

Screen Shot 2016-02-05 at 19.32.55

Hili linaashiria kuwa wana uwezo wa kutumia vizuri kukosekana kwa walinzi muhimu wa Atletico na kufunga mabao kwenye dimba la Vincente Calderon hapo kesho.

Mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo FC Barcelona Jumapili watawatembelea Levante kwenye dimba la Ciutat de Valencia. Levante inayonolewa na mwalimu Rubi inashika mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imekusanya alama 17 pekee.

Mbali na kuburuza mkia Levante ni timu inayoongoza kwa utovu wa nidhamu. Imekusanya jumla ya kadi za manjano 76 na kadi nyekundu 4 kwenye michezo yote. Kuna uwezekano mkubwa kuwa hili linaweza kuwagharimu na wakajikuta wanacheza pungufu.

Ikumbukwe kwenye michezo miwili ya mwisho wapinzani wa Barcelona walipokea kadi tatu nyekundu kutokana na mtindo wa Barca wa kutawala mchezo na vipaji binafsi vya wachezaji wao vinavyopelekea wapinzani kuwachezea madhambi. Matarajio ya Levante kuwazuia Barca kushinda mchezo huo ni madogo.

Real Madrid walio chini ya mchezaji wao hodari wa zamani Zinedine Zidane watakutana na Granada siku ya Jumapili. Timu hiyo tangu iwe chini ya kocha huyo imeshinda michezo mitatu kati ya minne na kutoa sare moja.

Granada ni moja kati ya timu dhaifu pia kwa sasa iliyo katika ukanda wa kushuka daraja. Real Madrid ambao wiki iliyopita waliwafumua Espanyol mabao sita kwa sifuri wana nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo wa Jumapili dhidi ya vijana wa mwalimu José Ramón Sandoval.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

LIGI KUU BARA: SIMBA YAUA TANO, YANGA YADONDOKA TENA

Tanzania Sports

Yanga yawaadhibu JKT-VPL