Ligi Kuu ya Hispania itaendelea, baada ya Mahakama Kuu kubatilisha mgomo uliopangwa na wachezaji na shirikisho la soka kuondoa marufuku yake.
Wikiendi hii ilikuwa ikutane na matukio mawili; moja likiwa uamuzi wa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) kuahirisha mashindano yote ya soka na pili wachezaji kuanza mgomo wao.
Katikati ya sakata hili ni haki za wadau katika mapato yanayotokana na kurushwa kwa matangazo ya televisheni kwa mechi.
Mahakama Kuu ilitangulia kutangaza kwamba mgomo wa wachezaji ni batili na mara RFEF nayo ikaondoa uamuzi wake wa kuahirisha mashindano yote.
Uamuzi huo ungeathiri kwa kiasi kikubwa La Liga ambayo imebakiza mechi mbili mbili kwa kila timu, fainali ya Kombe la Mfalme, ambapo Barcelona wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa na kombe hilo kwani wamefika fainali.
Barcelona wanaongoza ligi kuu kwa tofauti ya pointi nne mbele ya Real Madrid wakati watacheza fainali ya Copa del Rey na Athletic Bilbao Mei 30.
RFEF na Chama cha Wanasoka wa Hispania (AFE) hawakubaliani na uamuzi wa serikali wa kubadili mfumo wa klabu kupewa mapato ya haki za televisheni.
Kwa sasa, Barcelona na Real ndio pekee wenye haki ya kujadiliana haki hizo na kampuni mbalimbali na wanachuma nusu ya mapato yote.
Serikali imeamua kwamba klabu za La Liga zigawane sawa mapato yote, lakini wachezaji wanataka mgawo uende mbali zaidi hadi kwa klabu za madaraja ya chini, ili wachezaji wao nao wafaidi na kupanda kisoka na kiuchumi.
Chama cha Taifa cha Soka ya Kulipwa (LFP) chenye dhamana na ligi za madaraja mawili ya juu kinaunga mkono sheria hiyo na kinachukua hatua za kisheria kuzuia kusimamishwa kwa ligi.
RFEF imesema ipo tayari kwa majadiliano na serikali, lakini yenyewe imekaa kimya pasipo kutoa majibu yoyote.
Uamuzi wa kusitishwa kwa soka ni matokeo ya ubishani juu ya nani hasa anasimamia soka ya Hispania na ni hatima ya mvutano wa muda mrefu juu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na matangazo ya televisheni.
Barca na Real hawataki kuona utaratibu huo ukibadilika, kwani unawafaidisha na ndiyo maana huweza kusajili wachezaji wa kimataifa na kuitawala soka ya nyumbani na Ulaya pia.
Rais wa LFP, Javier Tebas alikuwa ametangaza nia yake ya kufungua shauri mahakamani kupinga kuahirishwa kwa ligi hiyo, akisema kwamba kungeweza kusababisha hasara ya pauni milioni 36 katika mapato ya mechi kila siku.
Mechi muhimu zilizobaki ni baina ya Atletico Madrid na Barcelona; Espanyol na Real Madrid Jumapili hii.
Mei 23 May ndio mechi za mwisho wa ligi, ambapo kati ya hizo Barcelona watacheza dhidi ya Deportivo huku Real Madrid wakivaana na Getafe.