in , ,

KWA HERI GEOFREY BONY NDAJE , NGOJA NILIFUTE CHOZI LANGU

Asubuhi jua likiwa linachomoza kutoka mashariki , matawi ya miti
yakiwa yanapepea taratibu na kutoa hewa nzuri, ndege zikiwa zinatoa
milio ya kufurahia upepo wa mti.

Hii yote ni kuonesha Mungu huachilia furaha na huzuni kila mawio na machweo.

Kwenye maisha kama hujawahi kupata huzuni au furaha basi utakuwa bado
hujaanza kuishi.

Mungu alivyoachilia nuru na upepo Kwa ndege asubuhi ya leo, aliamua
kuachilia giza zito kwa wapendasoka na wanamichezo kwa kumchukua
Geofrey Bony Ndaye.

Mioyo yetu ilitawalwa na ubaridi Kwa sekunde kadhaa, macho yetu
yakabaki yanatoa machozi bila kuamini kilichotokea.

Safari yake ilianzia Tukuyu Stars njia zake zikazidi kufunguka mpaka
alipoenda Prisons ambapo ndiyo ikawa njia ya kwake kwenda Kariakoo
kucheza kwenye moja ya timu kubwa sana Afrika Mashariki na Kati Yanga.

Utaanzaje kusahau namna ambavyo Goefrey Bony alivyoufanya mpira kuwa rahisi?

Hakuna sifa kubwa kwa mchezaji yoyote duniani kama kuitumikia timu ya
Taifa, ndoto hii Geofrey Bony ilikuwa nyepesi kwake kwa sababu ya
miguu bora iliyokuwa inautumikish a mpira uwanjani.

Leo hii Taifa zima linalia, linasononeka moyoni, mauti yamemfika
mmoja wa watu ambaye ni ngumu kumsahau.

Kuondoka kwa Geofrey Bony kumetuacha na huzuni kubwa sana mioyoni
mwetu pamoja na funzo kubwa sana kwetu sisi kuwa duniani hatujaja
kukaa ila niwapitaji, hivo tujiandae siku yoyote tutakapohitajika
kurudi kwenye makao yetu

Ndoto zake za kuwa kocha kwa siku za baadaye zimezimwa kwa siku
moja.Hakuna nuru tena kwenye ndoto zake zote ambazo hakufanikiwa
kuzitimiza.

Giza limetawala kwenye kila kitu ambacho alikipanga, majonzi
katuachia sisi pamoja na familia yake .

Tanzania ilimpoteza Buriani, leo hii tumenyang’anywa Bony. Mungu yote
haya kayaruhusu kwa mapenzi yake mema.

Bony kalitumikia soka akiwa kama mchezaji na alitakiwa kuwa lango la
wengine kulitumikia soka letu lakini ukurasa umefungwa na ukurasa
umefunguliwa.

Soka la Tanzania litakukumbuka daima, pumzika kwa amani Bony ,Chozi
langu nalifuta taratibu Kumbukumbu zako zikiwa zinabaki kichwani
mwangu na kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kukuona wakati unacheza.

Bwana alitoa, Bwana alitwaa.Jina lake lihidimiwe

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MAZURI YA 1992 YAMESHASAHULIKA, TUNAISHI MABAYA YA 2012

Tanzania Sports

Jinamizi kwa kipa aliyekula uwanjani