*Timu zinalingana kwa kila kitu
Matokeo ya sare ya 1-1 baina ya Cameroon na Guinea Bissau na vile vile kati ya Ivory Coast na Mali kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Jumamosi hii, yameacha timu zikiwa zinalingana kwa kila kitu.
Timu zote hizo nne zimecheza mechi mbili na kwenda sare zote, hivyo kuwa na pointi mbili na uwiano wa mabao ya kufungwa na kufunga kuwa sifuri kwa kila timu, hivyo kwamba hakuna wa kumcheka wala kumwogopa mwenzake.
Cameroon watacheza na Ivory Coast Jumatano hii kwenye mechi ya mwisho wakati Guinea Bissau watakamatana na Mali, ambapo Yaya Toure wa Ivory Coast ameapa kwamba siku hiyo ndipo watu watawaona ‘Tembo’ wa kweli.
Cameroon walionekana kuanza mechi vyema Jumamosi hii na washabiki wake wakalipuka kwa ngoma wakiwa wamejifunga vibwebwe pale Benjamin Moukandjo alipopiga kona na kuitumbukiza moja kwa moja wavuni dakika ya 13, lakini Ibrahima Traore akasawazisha kwa Bissau alipofyatua kombora kutoka yadi 20 dakika ya 42.
Cameroon wanaofundishwa na Volker Finke wamepata kutwaa kombe hili mara nne, lakini tangu 2002 hawajalichukua.
Katika mechi nyingine, Mali walikuwa wakisubiri kwa hamu mchezo umalizike, kwani baada ya kupata bao kupitia kwa Bakary Sako dakika ya saba tu, Ivory Coast walionekana kukosa majibu, lakini Max Gradel akawatoa kimasomaso kwa kufunga bao dakika nne kabla ya kipenga cha mwisho.
Hata hivyo, Ivory Coast walijihisi wanyonge kutokana na kunyimw a penati baada ya mshambuliaji mpya wa Manchester City, Wilfried Bony kuonekana kuchezewa vibaya na Molla Wague, lakini pia Kolo Toure aligonga mwamba kwa mpira wake wa kichwa.
Kwa muda mrefu Tembo hao walionekana kupelekeshwa ndivyo sivyo na vijana wa Mali, ambapo wakati fulani Sambou Yatabare alikuwa mwiba kwao. Kocha wa Ivory Coast, Herve Renard alionekana kukasirika muda wote wa mchezo, hasa waliponyimwa penati.
Jumapili hii Kongo Brazzaville wanapepetana na Burkina Faso wakati Gabon wapo na wenyeji, Guinea ya Ikweta. Kwenye kundi hilo A Kongo wanaongoza wakiwa na pointi nne, Gabon wanafuatia wakiwa nazo tatu, wenyeji wana mbili na Wabukinabe wana moja tu.
Comments
Loading…