*Chelsea na Stoke, Liverpool na vibonde
WASHIKA Bunduki wa London, Arsenal wamezawadiwa kukabiliana na timu ya League One ya Coventry katika raundi ya nne ya Kombe la FA.
Hiyo ni zawadi baada ya vijana hao wa Arsene Wenger kuwafunga wapinzani wao wakubwa wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur 2-0 na kuwatupa nje ya michuano hiyo.
Arsenal watakuwa nyumbani kwa mechi hiyo ambapo msimu uliopita walitolewa katika raundi ya tano na Blackburn na mara ya mwisho kwa Arsenal kutwaa kombe hilo ni 2005.
Chelsea watakuwa wenyeji wa Stoke wakati Manchester City au Blackburn watacheza na ama
Bristol City au Watford kutegemeana na matokeo ya marudio ya jozi mbili hizo kwa vile zilitoka sare katika mechi ya awali.
Mechi hizo zitachezwa kati ya Januari 25 na 26 ambapo baada ya Swansea kuwachapa Manchester United na kuwafungisha virago, watacheza dhidi ya Birmingham City, Bristol Rovers au Crawley.
Mabingwa watetezi Wigan watawaalika Crystal Palace ikiwa watavuka dhidi ya MK Dons kwenye maruadiano baada ya Jumamosi kwenda sare ya 3-3.
Everton wanaofundishwa na Roberto Martinez watacheza na klabu ya League One, Stevenage wakati kocha mpya Ole Gunnar Solskjaer wa Cardiff atawasafirisha vijana wake kwenda kucheza dhidi ya Bolton Wanderers.
Liverpool waliowafunga Oldham 2-0 watacheza na ama Bournemouth au Burton wa League Two.
Hull City watasafiri kucheza na Southend wa League Two wanaofundishwa na kocha wao wa zamani, Phil Brown.
Mechi nyingine ni Sunderland vs Kidderminster au Peterborough, Southampton vs Yeovil, Huddersfield vs Charlton au Oxford.
Ratiba inaonesha pia kwamba ama Port Vale au Plymouth watacheza na Brighton wakati
Nottingham Forest watakabiliana na Ipswich au Preston.
Rochdale ni dhidi ya ama Macclesfield au Sheffield Wednesday huku Sheffield United wakitifuana na ama Norwich au Fulham.
Kocha wa Southend, Brown, amekaririwa akisema kwamba kwa jinsi mashindano hayo yalivyo na yanavyochanganya vibonde na timu kubwa, hakuna anayeweza kuandika mada kwamba ni nini hasa.
“Moja ya malengo yangu nilipofika Southend lilikuwa kuvutia na kujaza mashabiki uwanjani, sasa kwa kuwa tumepangwa dhidi ya timu ya Ligi Kuu ya Hull, nadhani nitajaza mashabiki,” akasema mwalimu huyo aliyeondoka Hull 2010.
Hadi hatua hii ya nne kuna timu mbili zisizokuwa za ligi zinazoendelea kupeta kwenye mashindano haya.
Kocha wa Aston Villa, Paul Lambert alidai mashindano haya hayana umuhimu sana na klabu zingeweza kuondokana nayo.
Kocha wa Arsenal, Wenger alipata kudharau michuano ya jinsi hii na alikuwa akipanga vikosi dhaifu akisema hayana maana lakini siku hizi anapanga nyota.
Hata hivyo, aliyekuwa Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alisema kwamba ni mashindano muhimu kwa sababu yanasaidia klabu kujaza vikombe kwenye mashubaka yao badala ya kuwa na ukame wa kugombea lile la ligi kuu pekee.
Klabu nyingi sasa zinayaheshimu, na pamekuwapo matukio ya klabu ndogo kuzifunga zile kubwa.
Comments
Loading…